2 Wakorintho 1

2 Wakorintho 1

Salamu

Mungu wa faraja yote

3Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote.

4Yeye hutufariji katika taabu zetu, ili tuweze kuwafariji walio katika taabu yoyote kwa faraja ambayo sisi wenyewe tumepokea kutoka kwa Mungu.

5Kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi maishani mwetu, hivyo ndivyo faraja yetu inavyofurika kupitia kwa Kristo.

6Ikiwa tunataabika, ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu; tukifarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu, iwaleteayo saburi ya mateso yale yale yanayotupata.

7Nalo tumaini letu kwenu ni thabiti, kwa sababu tunajua kwamba kama vile mnavyoshiriki mateso yetu, ndivyo pia mnavyoshiriki faraja yetu.

8Ndugu wapendwa, hatutaki mkose kujua kuhusu zile taabu tulizopata huko jimbo la Asia. Kwa maana tulilemewa na mizigo sana, kiasi cha kushindwa kuvumilia, hata tulikata tamaa ya kuishi.

9Kwa kweli, mioyoni mwetu tulihisi tumekabiliwa na hukumu ya kifo, ili tusijitegemee sisi wenyewe bali tumtegemee Mungu afufuaye wafu.

10Yeye ametuokoa kwenye hatari kubwa ya kifo, na atatuokoa tena. Kwake yeye tumeweka tumaini letu kwamba ataendelea kutuokoa,

11kama vile mnavyoungana kusaidiana nasi katika maombi. Hivyo wengi watatoa shukrani kwa niaba yetu kwa ajili ya baraka za neema tulizopata kwa majibu ya maombi ya wengi.

Paulo aahirisha ziara

12Basi haya ndio majivuno yetu: Dhamiri yetu inatushuhudia kwamba tumeishi katika ulimwengu kwa utakatifu na uaminifu unaotoka kwa Mungu, na hasa katika uhusiano wetu na ninyi. Hatukufanya hivyo kwa hekima ya kidunia bali kwa neema ya Mungu.

13Kwa maana hatuwaandikii mambo ambayo hamwezi kusoma au kuyaelewa. Natumaini kwamba,

14kama vile mlivyotuelewa kwa sehemu, mtakuja kuelewa kwa ukamilifu ili mweze kujivuna kwa ajili yetu, kama na sisi tutakavyojivuna kwa ajili yenu katika siku ya Bwana Yesu.

15Kwa kuwa nilikuwa na uhakika wa mambo haya, nilitaka nije kwenu kwanza, ili mpate faida mara mbili.

16Nilipanga kuwatembelea nikiwa safarini kwenda Makedonia, na kurudi tena kwenu nikitoka Makedonia, ili mnisafirishe katika safari yangu ya kwenda Yudea.

17Nilipopanga jambo hili, je, nilikuwa kigeugeu? Au ninafanya mipango yangu kwa hali ya mwili, ili niseme, “Ndiyo, ndiyo” na “Siyo, siyo” wakati huo huo?

18Hakika kama Mungu alivyo mwaminifu, maneno yetu kwenu hayajakuwa “Ndiyo” na “Siyo”.

19Kwa kuwa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, ambaye mimi, Silvano, na Timotheo tulimhubiri kwenu, hakuwa “Ndiyo” na “Siyo”, bali kwake yeye siku zote ni “Ndiyo”.[#1:19 yaani Sila]

20Kwa maana ahadi zote za Mungu zilizo katika Kristo ni “Ndiyo”. Kwa sababu hii, ni kwake yeye tunasema “Amen” kwa utukufu wa Mungu.

21Basi ni Mungu atufanyaye sisi pamoja nanyi kusimama imara katika Kristo. Alitupaka mafuta

22kwa kututia muhuri wake na kutupatia Roho wake mioyoni mwetu kuwa rehani kwa ajili ya kututhibitishia yote aliyotuahidi.

23Namwita Mungu awe shahidi wangu kwamba sikurudi Korintho kwa sababu niliwahurumia ninyi.

24Si kwamba tunatawala imani yenu, bali twatenda kazi pamoja nanyi ili mfurahi, kwa sababu ni kwa imani mwasimama imara.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.