The chat will start when you send the first message.
1Makabila yote ya Israeli yakamjia Daudi huko Hebroni na kumwambia, “Sisi tu mwili wako na damu yako.
2Zamani, wakati Sauli alikuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyeiongoza Israeli vitani. Naye Bwana alikuambia, ‘Wewe utawachunga watu wangu Israeli, na utakuwa mtawala wao.’ ”
3Wazee wote wa Israeli wakamwendea Mfalme Daudi huko Hebroni, mfalme akafanya mapatano nao huko Hebroni mbele za Bwana , nao wakampaka Daudi mafuta kuwa mfalme wa Israeli.
4Daudi alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kutawala, naye akatawala Israeli kwa miaka arobaini.
5Huko Hebroni alitawala Yuda kwa miaka saba na miezi sita, na katika Yerusalemu alitawala Israeli yote na Yuda kwa miaka thelathini na tatu.
6Mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu kuwashambulia Wayebusi walioishi humo. Wayebusi wakamwambia Daudi, “Wewe hutaingia humu, kwani hata vipofu na viwete wanaweza kukufukuza.” Walidhani, “Daudi hawezi kuingia humu.”
7Hata hivyo, Daudi akaiteka ngome ya Sayuni, Mji wa Daudi.
8Siku ile, Daudi akasema, “Yeyote ambaye atawashinda Wayebusi, atatumia huo mfereji kuwafikia hao ‘viwete na vipofu’ ambao ni adui za Daudi.” Ndiyo sababu wanasema, “ ‘Vipofu na viwete’ hawataingia kwenye jumba la ufalme.”
9Ndipo Daudi akafanya makao ndani ya ngome na kuiita Mji wa Daudi. Akajenga eneo linalozunguka kuanzia Milo kuelekea ndani.[#5:9 maana yake Boma la Ngome]
10Daudi akazidi kuwa na nguvu zaidi na zaidi, kwa sababu Bwana Mungu wa majeshi alikuwa pamoja naye.
11Basi Hiramu mfalme wa Tiro akawatuma wajumbe kwa Daudi, wakiwa na magogo ya mwerezi, maseremala na waashi, nao wakajenga jumba la kifalme kwa ajili ya Daudi.
12Naye Daudi akafahamu kuwa Bwana amemwimarisha kuwa mfalme juu ya Israeli na ameinua ufalme wake kwa ajili ya Israeli, watu wake.
13Baada ya Daudi kuondoka Hebroni, akajitwalia masuria zaidi na wake huko Yerusalemu, nao wana wengi wa kiume na wa kike walizaliwa kwake.
14Haya ndiyo majina ya watoto waliozaliwa kwake huko: Shamua, Shobabu, Nathani, Sulemani,
15Ibihari, Elishua, Nefegi, Yafia,
16Elishama, Eliada na Elifeleti.
17Wafilisti waliposikia kuwa Daudi amepakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli, wakapanda na jeshi lao lote kwenda kumsaka, lakini Daudi akapata habari hizo, naye akateremka kwenye ngome.
18Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kusambaa kwenye Bonde la Warefai,
19kwa hiyo Daudi akamuuliza Bwana , “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?”
Bwana akamjibu, “Nenda, kwa maana hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.”
20Ndipo Daudi akaenda Baal-Perasimu, na huko akawashinda Wafilisti. Akasema, “Kama mafuriko yanavyofurika, Bwana amewafurikia adui zangu mbele yangu.” Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Baal-Perasimu.[#5:20 maana yake Bwana Afurikaye]
21Wafilisti wakaziacha sanamu zao huko, naye Daudi na watu wake wakazichukua.
22Wafilisti walikwea kwa mara nyingine na kusambaa katika Bonde la Warefai.
23Kwa hiyo Daudi akamuuliza Bwana , naye akamjibu, “Usipande moja kwa moja, bali wazungukie kwa nyuma na uwashambulie mbele ya miti ya miforosadi.
24Mara utakaposikia sauti ya kutembea kwenye vilele vya miti ya miforosadi, nenda haraka, kwa sababu hiyo itamaanisha kuwa Bwana ametangulia mbele yako kupiga jeshi la Wafilisti.”
25Basi Daudi akafanya kama Bwana alivyomwagiza, naye akawaangusha Wafilisti njia yote kuanzia Geba hadi Gezeri.[#5:25 Kwa Kiebrania mji huu uliitwa Gibeoni (taz. 1Nya 14:16).]