2 Timotheo 4

2 Timotheo 4

Maagizo ya mwisho

1Nakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu watu walio hai na waliokufa wakati wa kuja kwake na ufalme wake, kwamba:

2Hubiri Neno; kuwa tayari wakati ufaao na wakati usiofaa; karipia, kemea na utie moyo kwa uvumilivu wote na kwa mafundisho mazuri.

3Maana wakati utakuja watu watakapokataa kuyakubali mafundisho yenye uzima. Badala yake, ili kutimiza tamaa zao wenyewe, watajikusanyia idadi kubwa ya walimu watakaowaambia yale masikio yao yanatamani kusikia.

4Watakataa kusikiliza kweli na kuzigeukia hadithi za uongo.

5Bali wewe, vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiza wajibu wote wa huduma yako.

6Kwa maana mimi sasa ni tayari kumiminwa kama sadaka ya kinywaji, nayo saa yangu ya kuondoka imetimia.

7Nimevipiga vita vizuri, mashindano nimeyamaliza, imani nimeilinda.

8Sasa nimewekewa taji la haki ambalo Bwana, Mwamuzi wa haki, atanitunukia siku ile: wala si mimi tu, bali pia wote ambao wamengoja kwa shauku kudhihirishwa kwake.

Maelekezo ya binafsi

9Jitahidi kuja kwangu upesi

10kwa sababu Dema, kwa kuupenda ulimwengu, ameniacha na ameenda Thesalonike. Kreske ameenda Galatia, na Tito ameenda Dalmatia.

11Ni Luka pekee aliye hapa nami. Mtafute Marko uje naye, kwa sababu ananifaa sana katika huduma yangu.

12Nimemtuma Tikiko huko Efeso.

13Utakapokuja, niletee lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa, na vile vitabu vyangu, hasa vile vya ngozi.

14Iskanda yule mfua chuma alinitendea ubaya mkubwa. Bwana atamlipa kwa ajili ya yale aliyotenda.

15Wewe pia ujihadhari naye kwa sababu aliyapinga maneno yetu vikali.

16Katika utetezi wangu wa mara ya kwanza, hakuna hata mmoja aliyeniunga mkono, bali kila mmoja aliniacha. Naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo.

17Lakini Bwana alisimama upande wangu akanitia nguvu, ili kupitia kwangu lile Neno lihubiriwe kwa ukamilifu, watu wote Mataifa wapate kulisikia. Mimi niliokolewa kutoka kinywa cha simba.

18Bwana ataniokoa katika kila shambulio baya na kunileta salama katika ufalme wake wa mbinguni. Atukuzwe milele na milele. Amen.

Salamu za mwisho

19Wasalimu Prisila na Akila, na wote wa nyumbani mwa Onesiforo.[#4:19 kwa Kiyunani ni Priska]

20Erasto alibaki Korintho, nami nikamwacha Trofimo huko Mileto akiwa mgonjwa.

21Jitahidi ufike huku kabla ya majira ya baridi.

Eubulo anakusalimu, vivyo hivyo Pude, Lino, Klaudia na ndugu wote.

22Bwana awe pamoja na roho yako. Neema iwe pamoja nanyi.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.