Amosi 7

Amosi 7

Maono ya kwanza: Nzige

1Hili ndilo alilonionesha Bwana Mwenyezi katika maono: Alikuwa anaandaa makundi ya nzige baada ya kuvunwa fungu la mfalme na wakati ule tu mimea ya pili ilipokuwa ikichipua.

2Wakati nzige walikuwa wamekula mimea yote ya nchi, nililia kwa sauti kuu, “Bwana Mwenyezi, samehe! Je, Yakobo atawezaje kuendelea kuishi? Yeye ni mdogo sana!”

3Kwa hiyo Bwana akaghairi.

Kisha Bwana akasema, “Hili halitatokea.”

Maono ya pili: Moto

4Hili ndilo Bwana Mwenyezi alilonionesha katika maono: Bwana Mwenyezi alikuwa akiita hukumu ya moto; nao ulikausha vilindi vikuu, ukateketeza nchi.

5Ndipo nikalia, “Bwana Mwenyezi, nakusihi, zuia! Je, Yakobo atawezaje kuendelea kuishi? Yeye ni mdogo sana!”

6Kwa hiyo Bwana akaghairi.

Bwana Mwenyezi akasema, “Hili nalo halitatokea.”

Maono ya tatu: Timazi

7Hili ndilo alilonionesha katika maono: Bwana alikuwa amesimama karibu na ukuta ambao ulikuwa umejengwa kwa timazi, akiwa na uzi wa timazi mkononi mwake.

8Naye Bwana akaniuliza, “Je, Amosi unaona nini?”

Nikamjibu, “Uzi wa timazi.”

Kisha Bwana akasema, “Tazama, ninaweka uzi wa timazi miongoni mwa watu wangu Israeli; sitawahurumia tena.

9“Mahali pa Isaka pa juu pa kuabudia pataangamizwa,

na mahali patakatifu pa Israeli pa kuabudia pataharibiwa;

kwa upanga wangu nitainuka

dhidi ya nyumba ya Yeroboamu.”

Amosi na Amazia

10Kisha Amazia kuhani wa Betheli akatuma ujumbe kwa Yeroboamu mfalme wa Israeli, akisema: “Amosi analeta fitina juu yako katikati ya Israeli. Nchi haiwezi kuvumilia maneno yake yote.

11Kwa kuwa hili ndilo Amosi analosema:

“ ‘Yeroboamu atakufa kwa upanga,

na kwa hakika Israeli wataenda uhamishoni,

mbali na nchi yao.’ ”

12Kisha Amazia akamwambia Amosi, “Nenda zako, ewe mwonaji! Urudi katika nchi ya Yuda. Ujipatie riziki yako huko na kutoa unabii wako.

13Usiendelee kutoa unabii katika Betheli, kwa sababu hapa ni mahali pa mfalme pa kuabudia na Hekalu la ufalme huu.”

14Amosi akamjibu Amazia, “Mimi sikuwa nabii wala mwana wa nabii, lakini nilikuwa mchungaji wa kondoo na mtunza mikuyu.

15Lakini Bwana akanitoa kutoka kuchunga kondoo na kuniambia, ‘Nenda, ukawatabirie watu wangu Israeli.’

16Sasa basi, sikieni neno la Bwana . Ninyi mnasema,

“ ‘Usitabiri dhidi ya Israeli,

na uache kuhubiri dhidi ya nyumba ya Isaka.’

17“Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana :

“ ‘Mke wako atakuwa kahaba mjini,

nao wana wako wa kiume na wa kike watauawa kwa upanga.

Shamba lako litapimwa na kugawanywa,

na wewe mwenyewe utafia katika nchi ya kipagani.

Nayo Israeli kwa hakika itaenda uhamishoni,

mbali na nchi yao.’ ”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.