Wakolosai 3

Wakolosai 3

Kanuni za kuishi maisha matakatifu

1Basi, kwa kuwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo alikoketi mkono wa kuume wa Mungu.

2Yafikirini mambo yaliyo juu, wala si ya duniani.

3Kwa maana ninyi mlikufa, nao uhai wenu sasa umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.

4Kristo, aliye uzima wenu, atakapofunuliwa, ndipo nanyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu.

5Basi, ueni kabisa chochote kilicho ndani yenu cha asili ya kidunia: yaani uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na ulafi, ambao ni ibada ya sanamu.

6Kwa sababu ya mambo haya, ghadhabu ya Mungu inakuja.

7Ninyi pia zamani mlienenda katika mambo haya mlipoishi maisha hayo.

8Lakini sasa yawekeni mbali nanyi mambo kama haya yote: yaani hasira, ghadhabu, uovu, masingizio na lugha chafu kutoka midomoni mwenu.

9Msiambiane uongo, kwa maana mmevua kabisa utu wenu wa kale pamoja na matendo yake,

10nanyi mmevaa utu mpya, unaofanywa upya katika ufahamu sawasawa na mfano wa Muumba wake.

11Hapa hakuna Myunani wala Myahudi, aliyetahiriwa wala asiyetahiriwa, asiyestaarabika wala aliyestaarabika, mtumwa wala mtu huru, bali Kristo ni yote, na ndani ya yote.

12Basi, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wanaopendwa sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu.

13Vumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi.

14Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.

15Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani.

16Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu.

17Lolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kupitia kwake.

Kanuni katika madaraka ya nyumbani

18Ninyi wake, watiini waume zenu, kama inavyostahili katika Bwana.

19Ninyi waume, wapendeni wake zenu, wala msiwe wakali kwao.

20Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote, kwa maana hii inampendeza Bwana.

21Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.

22Ninyi watumwa, watiini mabwana zenu wa hapa duniani katika mambo yote. Fanyeni hivyo si wakiwepo tu, wala si kwa kujipendekeza tu kwao, bali kwa moyo mnyofu na kumcha Bwana.

23Lolote mfanyalo, fanyeni kwa moyo wote kama watu wanaomtumikia Bwana, na si wanadamu,

24kwa kuwa mnajua kwamba mtapokea urithi wenu kutoka kwa Bwana ukiwa thawabu yenu. Ni Bwana Yesu Kristo mnayemtumikia.

25Yeyote atendaye mabaya atapewa adhabu ya mabaya yake, wala hakuna upendeleo.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.