Kumbukumbu 23

Kumbukumbu 23

Kutengwa na mkutano

1Asiingie mtu yeyote aliyehasiwa kwa kupondwa makende au kwa kukatwa uume wake katika kusanyiko la Bwana .

2Mtu ambaye amezaliwa kwenye ndoa isiyo halali au wazao wake wasiingie kwenye kusanyiko la Bwana , hata kizazi cha kumi.

3Hapatakuwa na Mwamoni au Mmoabu au yeyote wa wazao wao atakayeruhusiwa kuingia katika kusanyiko la Bwana , hata kizazi cha kumi.

4Kwa kuwa hawakuja kuwalaki wakiwa na mkate na maji mlipokuwa njiani mkitoka Misri; tena walimwajiri Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori iliyo Mesopotamia ili awalaani.

5Hata hivyo, Bwana Mungu wenu hakumsikiliza Balaamu bali aligeuza laana kuwa baraka kwenu kwa sababu Bwana Mungu wenu anawapenda.

6Msitafute mapatano ya urafiki nao maisha yenu yote.

7Usimchukie Mwedomu, kwa kuwa yeye ni ndugu yako. Usimchukie Mmisri, kwa sababu uliishi kama mgeni katika nchi yake.

8Kizazi cha tatu cha watoto watakaozaliwa nao wanaweza kuingia katika kusanyiko la Bwana .

Unajisi katika kambi

9Unapokuwa umepiga kambi dhidi ya adui zako, jitenge na kitu chochote kisicho safi.

10Ikiwa mtu amechafuka kwa sababu ya kutokwa na shahawa usiku, inampasa atoke nje ya kambi na kukaa huko.

11Lakini jioni ikikaribia ataoga, na baada ya jua kuzama ataingia tena kambini.

12Tengeni mahali nje ya kambi ambapo mnaweza kwenda kujisaidia.

13Kama sehemu ya vifaa vyenu kuweni na kitu cha kulimia, nanyi mnapojisaidia, chimba shimo na kisha funika kinyesi chako.

14Kwa kuwa Bwana Mungu wenu hutembea katika kambi yenu ili kuwalinda na kuwaweka adui zenu mikononi mwenu. Kambi yenu ni lazima iwe takatifu, ili asione kitu chochote miongoni mwenu kilicho kichafu, akageuka na kuwaacha.

Sheria mbalimbali

15Ikiwa mtumwa amekimbilia kwako, usimrudishe kwa bwana wake.

16Mwache aishi miongoni mwenu mahali popote anapopapenda na katika mji wowote anaochagua. Usimdhulumu.

17Asiwepo Mwisraeli mwanamke kahaba au mwanaume hanithi wa mahali pa ibada za sanamu.

18Kamwe usilete mapato ya ukahaba ikiwa ni ya mwanamke au ni ya mwanaume katika nyumba ya Bwana Mungu wako kwa ajili ya nadhiri yoyote, kwa sababu Bwana Mungu wako anachukizwa na yote mawili.

19Usimtoze ndugu yako riba, iwe ni fedha ama chakula ama kitu kingine chochote ambacho unaweza kupata riba juu yake.

20Unaweza kumtoza mgeni riba, lakini siyo nduguyo Mwisraeli, ili Bwana Mungu wako akubariki katika kila kitu unachoweka mkono katika nchi unayoingia kuimiliki.

21Ukiweka nadhiri kwa Bwana Mungu wako, usichelewe kuitimiza, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakudai, nawe utakuwa na hatia ya dhambi.

22Lakini ukijizuia kuweka nadhiri, hutakuwa na hatia.

23Chochote kitakachotamkwa kwa midomo yako ni lazima uhakikishe umekifanya, kwa sababu uliweka nadhiri yako kwa hiari mbele za Bwana Mungu wako kwa kinywa chako mwenyewe.

24Ukiingia katika shamba la mizabibu la jirani yako, unaweza kula zabibu kadiri utakavyo, lakini usiweke chochote kwenye kikapu chako.

25Ukiingia katika shamba la nafaka la jirani yako, unaweza kukwanyua kwa mikono yako, lakini usikate kwa mundu nafaka iliyosimama.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.