The chat will start when you send the first message.
1Musa akawaita Israeli wote, akawaambia:
Ee Israeli, sikilizeni amri na sheria ninazowatangazia leo. Jifunzeni, na mwe na hakika kuzifuata.
2Bwana Mungu wetu alifanya agano nasi katika mlima wa Horebu.
3Si kwamba Bwana alifanya agano na baba zetu, bali alifanya nasi, nasi sote ambao tuko hai hapa leo.
4Bwana alisema nanyi uso kwa uso kutoka kati ya moto juu ya mlima.
5(Wakati huo nilisimama kati ya Bwana na ninyi kuwatangazia neno la Bwana , kwa sababu mliogopa ule moto, nanyi hamkupanda mlimani.)
Naye Mungu alisema:
7“Usiwe na miungu mingine ila mimi.
8Usijitengenezee sanamu katika umbo la kitu chochote kilicho juu mbinguni au duniani chini au ndani ya maji.
9Usivisujudie wala kuviabudu; kwa kuwa Mimi, Bwana Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi za baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanaonichukia,
10lakini ninaonesha upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanaonipenda na kuzishika amri zangu.
11Usilitaje bure jina la Bwana Mungu wako, kwa kuwa Bwana hataacha kumhesabia hatia yeye alitajaye jina lake bure.
12Adhimisha siku ya Sabato na kuiweka takatifu, kama Bwana Mungu wako alivyokuagiza.
13Kwa siku sita utafanya kazi na kutenda shughuli zako zote.
14Lakini siku ya saba ni Sabato kwa Bwana , Mungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yoyote, wewe, wala mwanao au binti yako, wala mtumishi wa kiume au wa kike, wala ngʼombe wako, punda wako au mnyama wako yeyote, wala mgeni aliye malangoni mwako, ili mtumishi wako wa kiume na wa kike wapate kupumzika kama wewe.
15Kumbuka mlikuwa watumwa huko Misri, na Bwana Mungu wenu aliwatoa huko kwa mkono wenye nguvu na kwa mkono ulionyooshwa. Kwa hiyo Bwana Mungu wako amekuagiza kuiadhimisha siku ya Sabato.
16Waheshimu baba yako na mama yako, kama Bwana Mungu wako alivyokuagiza, ili siku zako zipate kuwa nyingi na kufanikiwa katika nchi Bwana Mungu wako anayokupa.
17Usiue.
18Usizini.
19Usiibe.
20Usimshuhudie jirani yako uongo.
21Usitamani mke wa jirani yako. Usitamani nyumba ya jirani yako au shamba lake, mtumishi wake wa kiume au wa kike, ngʼombe au punda wake, wala kitu chochote cha jirani yako.”
22Hizi ndizo amri alizozitangaza Bwana kwa sauti kubwa kwa kusanyiko lenu lote huko mlimani kutoka kati ya moto na wingu na giza nene, wala hakuongeza chochote zaidi. Kisha akaziandika juu ya vibao viwili vya mawe, naye akanipa mimi.
23Mliposikia sauti kutoka kati ya giza, mlima ulipokuwa ukiwaka moto, viongozi wenu wote wa makabila yenu na wazee wenu walinijia mimi.
24Nanyi mkasema, “Bwana Mungu wetu ametuonesha utukufu na enzi yake, nasi tumesikia sauti yake kutoka kati ya moto. Leo tumeona kwamba mwanadamu anaweza kuishi hata kama Mungu akizungumza naye.
25Lakini sasa, kwa nini tufe? Moto huu mkubwa utatuteketeza sisi na tutakufa tukiendelea kusikia sauti ya Bwana Mungu wetu zaidi.
26Ni mtu yupi mwenye mwili ambaye amewahi kuisikia sauti ya Mungu aliye hai akizungumza kutoka kati ya moto, kama sisi tulivyoisikia, naye akaishi?
27Sogea karibu usikie yale yote asemayo Bwana Mungu wetu. Kisha utuambie chochote kile ambacho Bwana Mungu wetu anakuambia. Tutasikiliza na kutii.”
28Bwana aliwasikia wakati mlipozungumza nami, na Bwana akaniambia, “Nimesikia kile hawa watu walichokuambia. Kila kitu walichokisema ni kizuri.
29Laiti kama mioyo yao ingekuwa na mwelekeo wa kuniogopa na kuzishika amri zangu zote daima, ili wafanikiwe wao pamoja na watoto wao milele!
30“Nenda uwaambie warudi kwenye mahema yao.
31Lakini wewe baki hapa pamoja nami ili niweze kukupa maagizo yote, amri na sheria ambazo utawafundisha wazifuate katika nchi ninayoenda kuwapa waimiliki.”
32Hivyo kuweni waangalifu kuyafanya yale Bwana Mungu wenu aliyowaagiza; msigeuke upande wa kuume wala wa kushoto.
33Fuateni yale yote ambayo Bwana Mungu wenu aliwaagiza, ili mpate kuishi, kustawi na kuziongeza siku zenu katika nchi mtakayoimiliki.