Ezekieli 19

Ezekieli 19

Maombolezo kwa ajili ya wakuu wa Israeli

1“Wewe fanya maombolezo kuhusu wakuu wa Israeli

2na useme:

“ ‘Tazama jinsi gani mama yako alivyokuwa simba jike

miongoni mwa simba!

Alilala katikati ya wana simba

na kulisha watoto wake.

3Alimlea mmoja wa watoto wake,

naye akawa simba mwenye nguvu.

Akajifunza kurarua mawindo

naye akala watu.

4Mataifa wakasikia habari zake,

naye akanaswa katika shimo lao.

Wakamwongoza kwa ndoana

hadi nchi ya Misri.

5“ ‘Mama yake alipongoja na kuona tumaini lake halitimiziki,

nayo matarajio yake yametoweka,

akamchukua mwanawe mwingine

na kumfanya simba mwenye nguvu.

6Alizungukazunguka miongoni mwa simba,

kwa kuwa sasa alikuwa simba mwenye nguvu.

Akajifunza kurarua mawindo

naye akala watu.

7Akabomoa ngome zao

na kuiharibu miji yao.

Nchi na wote waliokuwa ndani yake

wakatiwa hofu kwa kunguruma kwake.

8Kisha mataifa wakaja dhidi yake

kutoka sehemu zilizomzunguka.

Wakatanda nyavu zao kwa ajili yake,

naye akanaswa katika shimo lao.

9Wakamvutia kwenye tundu kwa kutumia ndoana,

wakamleta kwa mfalme wa Babeli.

Wakamfunga gerezani, hivyo kunguruma kwake

hakukusikika tena

katika milima ya Israeli.

10“ ‘Mama yako alikuwa kama mzabibu

katika shamba lako la mizabibu

uliopandwa kando ya maji,

ukiwa unazaa sana na wenye matawi mengi

kwa sababu ya wingi wa maji.

11Matawi yake yalikuwa na nguvu,

yaliyofaa kuwa fimbo ya mtawala.

Ulikuwa mrefu kupita miti mingine

katikati ya matawi manene;

ulionekana kwa urahisi

kwa ajili ya urefu wake

na wingi wa matawi yake.

12Lakini ulingʼolewa kwa hasira kali

na kutupwa chini.

Upepo wa mashariki uliufanya usinyae,

matunda yake yakapukutika,

matawi yake yenye nguvu yakanyauka

na moto ukayateketeza.

13Sasa umepandwa jangwani

katika nchi kame na ya kiu.

14Moto ulienea kuanzia mojawapo ya matawi yake makubwa

na kuteketeza matunda yake.

Hakuna tawi lenye nguvu lililobaki juu yake

linalofaa kuwa fimbo ya mtawala.’

Hili ndilo ombolezo, na litumike kama ombolezo.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.