Ezekieli 28

Ezekieli 28

Unabii dhidi ya mfalme wa Tiro

1Neno la Bwana likanijia kusema:

2“Mwanadamu, mwambie mfalme wa Tiro, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“ ‘Kwa sababu moyo wako umejivuna

na umesema, “Mimi ni mungu;

nami ninaketi kwenye kiti cha enzi cha mungu

katika moyo wa bahari.”

Lakini wewe ni mwanadamu, wala si mungu,

ingawa unafikiri kuwa una hekima kama mungu.

3Je, wewe una hekima kuliko Danieli?

Je, hakuna siri iliyofichika kwako?

4Kwa hekima yako na ufahamu wako,

umejipatia utajiri,

nawe umejikusanyia dhahabu

na fedha katika hazina zako.

5Kwa werevu wako mwingi katika biashara,

umeongeza utajiri wako

na kwa sababu ya utajiri wako

moyo wako umekuwa na kiburi.

6“ ‘Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“ ‘Kwa sababu unafikiri una hekima,

mwenye hekima kama mungu,

7mimi nitawaleta wageni dhidi yako,

taifa katili kuliko yote;

watafuta panga zao dhidi ya uzuri wa hekima yako,

na kuchafua fahari yako inayongʼaa.

8Watakushusha chini shimoni,

nawe utakufa kifo cha kikatili

katika moyo wa bahari.

9Je, wakati huo utasema, “Mimi ni mungu,”

mbele ya wale wanaokuua?

Utakuwa mwanadamu tu, wala si mungu,

mikononi mwa hao wanaokuua.

10Utakufa kifo cha wasiotahiriwa

kwa mkono wa wageni.

Kwa kuwa mimi nimenena, asema Bwana Mwenyezi.’ ”

11Neno la Bwana likanijia kusema:

12“Mwanadamu, mfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, nawe umwambie: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“ ‘Ulikuwa kipeo cha ukamilifu, ukiwa umejaa hekima

na mkamilifu katika uzuri.

13Ulikuwa ndani ya Edeni,

bustani ya Mungu;

kila kito cha thamani kilikupamba:

akiki nyekundu, yakuti manjano na zumaridi,

krisolitho, shohamu na yaspi,

yakuti samawi, almasi na zabarajadi.

Kuwekwa kwa hayo mapambo na kushikizwa kwake

kulifanywa kwa dhahabu;

siku ile ulipoumbwa yaliandaliwa tayari.

14Ulipakwa mafuta kuwa kerubi mlinzi,

kwa kuwa hivyo ndivyo nilivyokuweka wakfu.

Ulikuwa kwenye mlima mtakatifu wa Mungu;

ulitembea katikati ya vito vya moto.

15Ulikuwa mnyofu katika njia zako

tangu siku ile ya kuumbwa kwako,

hadi uovu ulipoonekana ndani yako.

16Kutokana na biashara yako iliyoenea,

ulijazwa na dhuluma,

nawe ukatenda dhambi.

Hivyo nilikuondoa kwa aibu kutoka mlima wa Mungu,

nami nikakufukuza, ee kerubi mlinzi,

kutoka katikati ya vito vya moto.

17Moyo wako ukawa na kiburi

kwa ajili ya uzuri wako,

nawe ukaiharibu hekima yako

kwa sababu ya fahari yako.

Kwa hiyo nikakutupa chini;

nimekufanya kioja mbele ya wafalme.

18Kwa dhambi zako nyingi na biashara yako ya dhuluma,

umenajisi mahali pako patakatifu.

Kwa hiyo nilifanya moto utoke ndani yako,

nao ukakuteketeza,

nami nikakufanya majivu juu ya nchi,

machoni pa wote waliokuwa wakitazama.

19Mataifa yote yaliyokujua

yanakustaajabia;

umefikia mwisho wa kutisha

na hutakuwepo tena milele.’ ”

Unabii dhidi ya Sidoni

20Neno la Bwana likanijia kusema:

21“Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Sidoni, ukatabiri dhidi yake,

22nawe useme: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“ ‘Mimi ni kinyume chako, ee Sidoni,

nami nitapata utukufu ndani yako.

Nao watajua kwamba Mimi ndimi Bwana ,

nitakapotekeleza hukumu zangu

na kuonesha utakatifu wangu ndani yake.

23Nitapeleka tauni ndani yake

na kufanya damu itiririke katika barabara zake.

Waliochinjwa wataanguka ndani yake,

kwa upanga dhidi yake kila upande.

Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Bwana .

24“ ‘Nyumba ya Israeli hawatakuwa tena na majirani wenye nia ya kuwadhuru, wanaoumiza kama michongoma na miiba mikali. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Bwana Mwenyezi.

25“ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: Nitakapoikusanya nyumba ya Israeli kutoka mataifa ambako wametawanyika, nitajionesha kuwa mtakatifu miongoni mwao machoni pa mataifa. Ndipo watakapoishi katika nchi yao wenyewe, niliyompa mtumishi wangu Yakobo.

26Wataishi humo kwa salama na watajenga nyumba na kupanda mashamba ya mizabibu, wataishi kwa salama nitakapowaadhibu majirani zao wote ambao waliwafanyia uovu. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Bwana Mungu wao.’ ”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.