Ezekieli 31

Ezekieli 31

1Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa tatu, siku ya kwanza, neno la Bwana likanijia, kusema:

2“Mwanadamu, mwambie Farao mfalme wa Misri na makundi yake hivi:

“ ‘Je, ni nani awezaye kulinganishwa

na wewe katika fahari.

3Angalia Ashuru, zamani ulikuwa mwerezi huko Lebanoni,

ukiwa na matawi mazuri

na kutia msitu kivuli;

ulikuwa mrefu sana, kilele chake

kilipita majani ya miti yote.

4Maji mengi yaliustawisha,

chemchemi zenye maji mengi

ziliufanya urefuke;

vijito vyake vilitiririka pale

ulipoota pande zote

na kupeleka mifereji yake

kwenye miti yote ya shambani.

5Hivyo ukarefuka

kupita miti yote ya shambani;

vitawi vyake viliongezeka

na matawi yake yakawa marefu,

yakitanda kwa sababu ya wingi wa maji.

6Ndege wote wa angani

wakaweka viota kwenye vitawi vyake,

wanyama wote wa shambani

wakazaana chini ya matawi yake,

mataifa makubwa yote

yaliishi chini ya kivuli chake.

7Ulikuwa na fahari katika uzuri,

ukiwa na matawi yaliyotanda,

kwa kuwa mizizi yake iliteremka

hadi kwenye maji mengi.

8Mierezi katika bustani ya Mungu

haikuweza kushindana nao,

wala misunobari haikuweza

kulingana na vitawi vyake,

wala miaramoni

haikulinganishwa na matawi yake,

wala hakukuwa na mti katika bustani ya Mungu

wa kulinganisha na uzuri wake.

9Niliufanya kuwa mzuri,

ukiwa na matawi mengi;

nao ulionewa wivu na miti yote ya Edeni

katika bustani ya Mungu.

10“ ‘Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: Kwa sababu ulikuwa mrefu sana, kilele chake kikiwa juu ya majani manene ya miti na kwa sababu ulikuwa na kiburi cha urefu wake,

11niliutia mikononi mwa mtawala wa mataifa, ili yeye autende sawasawa na uovu wake. Nikaukatilia mbali,

12nayo mataifa mageni yaliyo makatili sana yaliukata huo mti na kuuacha. Matawi yake yalianguka juu ya milima na kwenye mabonde yote, vitawi vyake vikavunjika na kusambaa katika makorongo yote ya nchi. Mataifa yote ya duniani yakaondoka kutoka kivuli chake na kuuacha.

13Ndege wote wa angani wakakaa kwenye ule mti ulioanguka na wanyama pori wote wakakaa katikati ya vitawi vyake.

14Kamwe hakutakuwa na miti mingine kando ya hayo maji itakayorefuka zaidi ya huo, vilele vyake vikiwa juu ya majani yote ya miti. Hakuna miti mingine, hata kama imekunywa maji vizuri namna gani, itakayofikia urefu huo. Yote mwisho wake ni kifo, na kuingia ardhini, kama vile ilivyo kwa wanadamu, pamoja na wale wanaoshuka shimoni.

15“ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: Katika siku ile mwerezi uliposhushwa chini kaburini nilizifunika chemchemi zenye maji mengi kwa maombolezo: Nilivizuia vijito vyake na wingi wa maji yake nikauzuia. Kwa sababu yake niliivika Lebanoni huzuni, nayo miti yote ya shambani ikanyauka.[#31:15 Kaburini maana yake ni Kuzimu ; kwa Kiebrania ni Sheol ; pia 31:16, 17.]

16Niliyafanya mataifa yatetemeke kwa kishindo cha kuanguka kwake wakati nilipoushusha chini kaburini pamoja na wale wanaoshuka shimoni. Ndipo miti yote ya Edeni, miti iliyo bora kuliko yote na iliyo mizuri sana ya Lebanoni, miti yote ile iliyokunywa maji vizuri, ilifarijika hapa duniani.

17Wale walioishi katika kivuli chake, wale walioungana naye miongoni mwa mataifa, nao pia walikuwa wamezikwa pamoja naye, wakiungana na wale waliouawa kwa upanga.

18“ ‘Ni miti ipi ya Edeni inayoweza kulinganishwa nawe kwa fahari na utukufu? Hata hivyo, wewe pia, utashushwa pamoja na miti ya Edeni hadi chini kabisa; utalala miongoni mwa wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga.

“ ‘Huyu ni Farao pamoja na makundi yake yote, asema Bwana Mwenyezi.’ ”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.