The chat will start when you send the first message.
1Kisha, baada ya miaka kumi na nne, nilipanda tena kwenda Yerusalemu, wakati huu pamoja na Barnaba, na nikamchukua Tito pia.
2Nilienda kwa sababu nilikuwa nimefunuliwa na Mungu, ili nikawaeleze kwa faragha wale walioonekana kuwa viongozi, ile Injili ninayoihubiri kwa watu wa Mataifa. Nilifanya hivyo kwa kuhofia kwamba nisije nikawa nilikuwa ninakimbia au nilikimbia bure.
3Lakini hata Tito aliyekuwa nami, na alikuwa Myunani, hakulazimika kutahiriwa.
4Lakini kwa sababu ya ndugu wa uongo ambao walijiingiza kwa siri katikati yetu ili kupeleleza uhuru tulio nao katika Kristo Yesu, wapate kututia utumwani,
5hatukukubaliana nao hata dakika moja, ili ukweli wa Injili ubaki nanyi.
6Kwa habari ya wale waliokuwa wakubaliwe kuwa viongozi (kwangu mimi sikujali vyeo vyao, maana Mungu hana upendeleo), wale watu hawakuniongezea chochote.
7Badala yake walitambua kwamba nilikuwa nimekabidhiwa kazi ya kuhubiri Injili kwa watu wa Mataifa, kama vile Petro alivyokabidhiwa kuhubiri Injili kwa Wayahudi.
8Kwa maana, Mungu aliyekuwa akitenda kazi katika huduma ya Petro kama mtume kwa Wayahudi, ndiye pia aliyekuwa anatenda kazi katika huduma yangu kama mtume kwa watu wa Mataifa.
9Basi Yakobo, Kefa na Yohana, walioonekana kama nguzo za kanisa, walitupatia mkono wa shirika, mimi na Barnaba, walipotambua ile neema niliyopewa. Wakakubali kwamba sisi twende kwa watu wa Mataifa, na wao waende kwa Wayahudi.[#2:9 yaani Petro]
10Walichotuomba ni kwamba tuendelee kuwakumbuka maskini, jambo ambalo ndilo nililokuwa na shauku ya kulifanya.
11Lakini Petro alipofika Antiokia, mimi nilimpinga ana kwa ana kwa sababu alikuwa amekosea kwa wazi.
12Kabla baadhi ya watu waliotoka kwa Yakobo hawajafika, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa. Lakini hao watu walipofika alianza kujiondoa na kujitenga na watu wa Mataifa kwa sababu aliwaogopa wale wa kundi la tohara.
13Pia Wayahudi wengine waliungana naye katika unafiki huu, hata Barnaba naye akapotoshwa na unafiki wao.
14Nilipoona kwamba hawatendi sawasawa na kweli ya Injili, nilimwambia Petro mbele ya wote, “Wewe ni Myahudi, nawe unaishi kama mtu wa Mataifa na wala si kama Myahudi. Imekuwaje basi, mnawalazimisha watu wa Mataifa kufuata desturi za Kiyahudi?
15“Sisi wenyewe ni Wayahudi kwa kuzaliwa na si watu wenye dhambi kama watu wa Mataifa,
16bado tunajua kwamba mtu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria bali kupitia kwa imani katika Yesu Kristo. Hivyo sisi pia, tumemwamini Kristo Yesu ili tupate kuhesabiwa haki kupitia kwa imani katika Kristo, wala si kwa matendo ya sheria, kwa sababu kwa kushika sheria hakuna hata mtu mmoja atakayehesabiwa haki.
17“Lakini tukitafuta kuhesabiwa haki katika Kristo, inakuwa dhahiri kwamba sisi ni wenye dhambi. Je, ina maana kwamba Kristo amekuwa mtumishi wa dhambi? La hasha!
18Lakini ikiwa mimi ninajenga tena kile ambacho nimekwisha kukibomoa, basi ninaonesha kwamba mimi ni mkosaji.
19Kwa maana mimi kupitia kwa sheria, nimeifia sheria ili nipate kuishi kwa ajili ya Mungu.
20Nimesulubiwa pamoja na Kristo, wala si mimi tena ninayeishi, bali Kristo ndiye aishiye ndani yangu. Uhai nilio nao sasa katika mwili, ninaishi kwa imani katika Mwana wa Mungu, aliyenipenda na kujitoa kwa ajili yangu.
21Siibatilishi neema ya Mungu, kwa maana kama haki ingeweza kupatikana kupitia kwa sheria, basi Kristo alikufa bure!”