The chat will start when you send the first message.
1Kwa hiyo ndugu watakatifu, mnaoshiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini Yesu, mtume na Kuhani Mkuu wa ukiri wetu.
2Alikuwa mwaminifu kwa yeye aliyemteua, kama Musa alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu.
3Yesu ameonekana anastahili heshima kubwa kuliko Musa, kama vile mjenzi wa nyumba alivyo wa heshima kubwa kuliko nyumba yenyewe.
4Kwa kuwa kila nyumba hujengwa na mtu, lakini Mungu ni mjenzi wa kila kitu.
5Musa, kama mtumishi, alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu, akishuhudia kwa yale Mungu angeyasema baadaye.[#3:5 Hes 12:7]
6Lakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana katika nyumba ya Mungu. Sisi ndio nyumba yake, kama tutashikilia sana ujasiri wetu na tumaini tunalojivunia.
7Kwa hiyo, kama Roho Mtakatifu asemavyo:
“Leo, mkiisikia sauti yake,
8msiifanye mioyo yenu migumu,
kama mlivyofanya katika uasi,
wakati ule wa kujaribiwa jangwani,
9ambapo baba zenu walinijaribu na kunipima,
ingawa kwa miaka arobaini
walikuwa wameyaona matendo yangu.
10Hiyo ndiyo sababu nilikasirikia kizazi kile,
nami nikasema, ‘Siku zote mioyo yao imepotoka,
nao hawajazijua njia zangu.’
11Hivyo nikatangaza kwa kiapo katika hasira yangu,
‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’”
12Ndugu zangu, chungeni asiwepo miongoni mwenu mtu mwenye moyo mwovu usioamini, unaojitenga na Mungu aliye hai.
13Lakini mtiane moyo mtu na mwenzake kila siku, maadamu inaitwa “Leo”, ili asiwepo hata mmoja wenu mwenye kufanywa mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.
14Kwa kuwa tumekuwa washiriki wa Kristo, tukishikamana tu kwa uthabiti na tumaini letu la kwanza hadi mwisho.
15Kama ilivyonenwa:
“Leo, mkiisikia sauti yake,
msiifanye mioyo yenu migumu
kama mlivyofanya wakati wa kuasi.”
16Basi ni nani waliosikia lakini bado wakaasi? Je, si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa?
17Lakini ni nani Mungu aliwakasirikia miaka arobaini? Je, si wale waliofanya dhambi ambao miili yao ilianguka jangwani?
18Ni nani hao ambao Mungu aliapa kuwa kamwe hawataingia rahani mwake isipokuwa ni wale waliokataa kutii?
19Hivyo tunaona kwamba hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.