The chat will start when you send the first message.
1Chipukizi litatokea kutoka shina la Yese,
kutoka mizizi yake Tawi litazaa tunda.
2Roho wa Bwana atakaa juu yake,
Roho wa hekima na wa ufahamu,
Roho wa shauri na wa uweza,
Roho wa maarifa na wa kumcha Bwana
3naye atafurahia kumcha Bwana .
Hatahukumu kwa yale ayaonayo kwa macho yake,
wala kuamua kwa yale ayasikiayo kwa masikio yake,
4bali kwa uadilifu atahukumu wahitaji,
kwa haki ataamua wanyenyekevu wa dunia.
Ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake,
kwa pumzi ya midomo yake atawaua waovu.
5Haki itakuwa mkanda wake
na uaminifu utakuwa mshipi kiunoni mwake.
6Mbwa-mwitu ataishi pamoja na mwana-kondoo,
naye chui atalala pamoja na mbuzi,
ndama, mwana simba na ngʼombe wa mwaka mmoja
watakaa pamoja,
naye mtoto mdogo atawaongoza.
7Ngʼombe na dubu watalisha pamoja,
watoto wao watalala pamoja,
na simba atakula majani makavu kama maksai.
8Mtoto mchanga atacheza karibu na shimo la nyoka,
naye mtoto mdogo ataweka mkono wake
kwenye kiota cha fira.
9Hawatadhuru wala kuharibu
juu ya mlima wangu mtakatifu wote,
kwa kuwa dunia itajawa na kumjua Bwana
kama maji yajazavyo bahari.
10Katika siku hiyo, Shina la Yese atasimama kama bendera kwa ajili ya mataifa. Mataifa yatakusanyika kwake, na mahali pake pa kupumzikia patakuwa utukufu.
11Katika siku hiyo Bwana atanyoosha mkono wake mara ya pili kurudisha mabaki ya watu wake waliosalia kutoka Ashuru, Misri, Pathrosi, Kushi, Elamu, Babeli, Hamathi, na kutoka visiwa vya baharini.[#11:11 yaani Misri ya Juu]
12Atainua bendera kwa mataifa
na kuwakusanya Waisraeli walio uhamishoni;
atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika
kutoka pembe nne za dunia.
13Wivu wa Efraimu utatoweka,
na adui wa Yuda watakatiliwa mbali;
Efraimu hatamwonea Yuda wivu,
wala Yuda hatakuwa na uadui na Efraimu.
14Watawashukia katika miteremko ya Wafilisti
hadi upande wa magharibi,
kwa pamoja watawateka watu nyara
hadi upande wa mashariki.
Watawapiga Edomu na Moabu,
na Waamoni watatawaliwa nao.
15Bwana atakausha
ghuba ya bahari ya Misri;
kwa upepo mkavu ataupeleka mkono wake
juu ya Mto Frati.
Ataugawanya katika vijito saba
ili watu waweze kuuvuka wakiwa wamevaa viatu.
16Kutakuwa na njia kuu kwa mabaki ya watu wake
wale waliosalia kutoka Ashuru,
kama ilivyokuwa kwa Israeli
walipopanda kutoka Misri.