Isaya 53

Isaya 53

1Ni nani aliyeamini ujumbe wetu,

na mkono wa Bwana umefunuliwa kwa nani?

2Alikua mbele yake kama mche mwororo

na kama mzizi katika nchi kavu.

Hakuwa na uzuri wala utukufu wa kutuvutia kwake,

hakuwa na chochote katika sura yake cha kutufanya tumtamani.

3Alidharauliwa na kukataliwa na wanadamu,

mtu wa huzuni nyingi, ajuaye mateso.

Kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao,

alidharauliwa, wala hatukumhesabu kuwa kitu.

4Hakika alichukua udhaifu wetu

na akajitwika huzuni zetu;

tulidhania kuwa ameadhibiwa na Mungu,

naye akapigwa sana na kujeruhiwa.

5Lakini alijeruhiwa kwa ajili ya makosa yetu,

alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu;

adhabu iliyotuletea sisi amani ilikuwa juu yake,

na kwa majeraha yake sisi tumepona.

6Sisi sote, kama kondoo, tumepotea,

kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe,

naye Bwana aliweka juu yake

maovu yetu sisi sote.

7Alionewa na kuteswa,

hata hivyo hakufungua kinywa chake;

aliongozwa kama mwana-kondoo

apelekwaye machinjoni,

kama vile kondoo anyamazavyo mbele ya wao wamkataye manyoya,

hivyo hakufungua kinywa chake.

8Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa.

Nani awezaye kueleza kuhusu kizazi chake?

Kwa maana alikatiliwa mbali na nchi ya walio hai,

alipigwa kwa ajili ya makosa ya watu wangu.

9Wakamfanyia kaburi pamoja na waovu,

pamoja na matajiri katika kifo chake,

ingawa hakutenda jeuri,

wala hapakuwa na hila kinywani mwake.

10Lakini yalikuwa ni mapenzi ya Bwana

kumchubua na kumsababisha ateseke.

Ingawa Bwana amefanya maisha yake

kuwa sadaka ya hatia,

ataona uzao wake na kuishi siku nyingi,

nayo mapenzi ya Bwana

yatafanikiwa mkononi mwake.

11Baada ya maumivu ya nafsi yake,

ataona nuru ya uzima na kuridhika;

kwa maarifa yake, mtumishi wangu mwenye haki

atawafanya wengi kuwa wenye haki,

naye atayachukua maovu yao.

12Kwa hiyo nitamgawia sehemu miongoni mwa wakuu,

naye atagawana nyara pamoja na wenye nguvu,

kwa sababu aliyamimina maisha yake hadi mauti,

naye alihesabiwa pamoja na wakosaji.

Kwa kuwa alichukua dhambi za wengi,

na kuwaombea wakosaji.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.