Waamuzi 12

Waamuzi 12

Yefta na Efraimu

1Watu wa Efraimu wakaita majeshi yao, wakavuka kwenda Zafoni. Wakamwambia Yefta, “Kwa nini mmeenda kupigana na Waamoni bila kutuita ili twende pamoja nawe? Basi tutaichoma moto nyumba yako, pamoja nawe ukiwa ndani yake.”

2Yefta akajibu, “Mimi na watu wangu tulikuwa na ugomvi mkubwa na Waamoni. Ingawa niliwaita, hamkuniokoa kutoka mkono wao.

3Nilipoona kuwa hamniokoi, nikauhatarisha uhai wangu, nikavuka kupigana na Waamoni. Naye Bwana akanipatia ushindi dhidi yao. Sasa kwa nini mnanijia leo ili kupigana nami?”

4Ndipo Yefta akakusanya wanaume wa Gileadi pamoja na kupigana na Efraimu. Wagileadi wakawashinda Waefraimu, kwa kuwa Waefraimu walisema, “Ninyi Wagileadi ni waasi mliotoroka toka Efraimu na Manase.”

5Wagileadi wakaviteka vivuko vya Mto Yordani kuelekea Efraimu. Kisha ilikuwa yeyote aliyenusurika kutoka Efraimu aliposema, “Niache nivuke,” hao wanaume wa Gileadi walimuuliza, “Je wewe ni Mwefraimu?” Akijibu “Hapana,”

6walimwambia, “Sawa, sema ‘Shibolethi’.” Iwapo alitamka, “Sibolethi”, kwa sababu hakuweza kutamka hilo neno sawasawa, walimkamata na kumuua hapo kwenye vivuko vya Mto Yordani. Waefraimu elfu arobaini na mbili waliuawa wakati huo.

7Yefta akawa mwamuzi wa Waisraeli kwa muda wa miaka sita. Kisha Yefta akafa, akazikwa katika mmoja wa miji ya Gileadi.

Ibzani, Eloni na Abdoni

8Baada yake, Ibzani wa Bethlehemu akawa mwamuzi wa Israeli.

9Alikuwa na wana thelathini na binti thelathini. Akawaoza binti zake kwa watu wengine nje ya ukoo wake, na kuwatwalia wanawe wanawake thelathini toka nje ya ukoo wake. Ibzani akawa mwamuzi wa Israeli kwa muda wa miaka saba.

10Kisha Ibzani akafa, akazikwa huko Bethlehemu.

11Baada yake, Eloni Mzabuloni akawa mwamuzi wa Israeli kwa muda wa miaka kumi.

12Kisha Eloni akafa, akazikwa huko Aiyaloni katika nchi ya Zabuloni.

13Baada yake, Abdoni mwana wa Hileli Mpirathoni akawa mwamuzi wa Israeli.

14Naye alikuwa na wana arobaini, na wajukuu thelathini waliopanda punda sabini. Akawa mwamuzi wa Israeli kwa muda wa miaka nane.

15Kisha Abdoni mwana wa Hileli Mpirathoni akafa, akazikwa Pirathoni huko Efraimu, katika nchi ya vilima ya Waamaleki.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.