The chat will start when you send the first message.
1Baada ya kitambo kidogo, wakati wa mavuno ya ngano, Samsoni akachukua mwana-mbuzi, kwenda kumzuru mkewe. Akasema, “Nataka kuingia chumbani kwa mke wangu.” Lakini baba yake huyo mwanamke hakumruhusu kuingia.
2Baba mkwe wake akamwambia, “Nilikuwa na hakika kwamba ulimchukia, hivyo nikampeana kwa rafiki yako. Je, dada yake mdogo si mzuri kuliko yeye? Mchukue huyo badala yake.”
3Samsoni akawaambia, “Wakati huu, nitakapowadhuru Wafilisti, sitakuwa na lawama.”
4Hivyo Samsoni akaondoka na kuwakamata mbweha mia tatu, akawafunga wawili wawili, mikia kwa mikia. Kisha akafungia mwenge wa moto kwenye kila jozi la mikia hiyo.
5Akawasha ile mienge na kuwaachia wale mbweha katika mashamba ya Wafilisti ya nafaka zilizosimamishwa katika matita. Akateketeza matita ya nafaka, pamoja na mashamba ya mizabibu na mashamba ya mizeituni.
6Wafilisti walipouliza, “Ni nani aliyetenda jambo hili?” Wakaambiwa, “Ni Samsoni, mkwewe yule Mtimna, kwa sababu mkewe alipeanwa kwa rafiki yake.”
Hivyo Wafilisti wakapanda, wakamteketeza kwa moto yeye huyo mwanamke pamoja na baba yake.
7Samsoni akawaambia, “Kwa kuwa mmetenda hivyo, hakika sitatulia hadi niwe nimelipiza kisasi juu yenu.”
8Akawashambulia kwa ukali na kuwaua watu wengi sana. Kisha akateremka na kukaa kwenye pango katika mwamba wa Etamu.
9Wafilisti wakapanda na kupiga kambi huko Yuda na kuenea huko Lehi.
10Watu wa Yuda wakawauliza, “Kwa nini mmekuja kupigana nasi?”
Wakawajibu, “Tumekuja ili kumkamata Samsoni na kumtenda kama alivyotutendea.”
11Ndipo watu elfu tatu wa Yuda waliteremka hadi kwenye pango katika mwamba wa Etamu, wakamwambia Samsoni, “Je, hujatambua kuwa Wafilisti wanatutawala? Ni nini hiki ulichotutendea?”
Akawajibu, “Nimewatendea tu kile walichonitendea.”
12Wakamwambia, “Tumekuja kukufunga na kukutia mikononi mwa Wafilisti.”
Samsoni akawaambia, “Niapieni kuwa hamtaniua ninyi wenyewe.”
13Wakamjibu, “Sisi hatutakuua, bali tutakufunga tu na kukutia mikononi mwao.” Basi wakamfunga kwa kamba mbili mpya na kumchukua toka huko kwenye pango katika mwamba.
14Alipokaribia Lehi, Wafilisti wakamjia wakipiga kelele. Roho wa Bwana akaja juu yake kwa nguvu. Kamba zilizomfunga mikono zikawa kama kitani iliyochomwa kwa moto, na vifungo vyake vikaanguka chini toka mikononi mwake.
15Ndipo akaona mfupa mpya wa taya la punda, akanyoosha mkono, akauchukua na kuua nao Wafilisti wapatao elfu moja.
16Ndipo Samsoni akasema,
“Kwa taya la punda
malundo juu ya lundo,
kwa taya la punda
nimeua watu elfu moja.”
17Alipomaliza kusema, akautupa ule mfupa wa taya; na mahali pale pakaitwa Ramath-Lehi.[#15:17 maana yake Kilima cha Taya]
18Kwa kuwa alihisi kiu sana, akamlilia Bwana , akisema, “Umempa mtumishi wako ushindi huu mkuu. Je, sasa nife kwa kiu na kuangukia mikononi mwa hawa watu wasiotahiriwa?”
19Ndipo Mungu akafunua shimo huko Lehi, na maji yakatoka. Samsoni alipoyanywa maji hayo, nguvu zikamrudia, akahuika. Hivyo chemchemi ile ikaitwa En-Hakore, nayo iko hadi leo huko Lehi.[#15:19 maana yake Chemchemi ya Aliyeita]
20Samsoni akawa mwamuzi wa Waisraeli katika siku za Wafilisti kwa muda wa miaka ishirini.