Waamuzi 5

Waamuzi 5

Wimbo wa Debora

1Siku hiyo Debora na Baraka mwana wa Abinoamu wakaimba wimbo huu:

2“Wakuu katika Israeli wanapoongoza,

wakati watu wanapojitoa

kwa hiari yao wenyewe:

mhimidini Bwana !

3“Sikieni hili, enyi wafalme!

Sikilizeni, enyi watawala!

Nitamwimbia Bwana , nitaimba;

kwa wimbo nitamhimidi Bwana ,

Mungu wa Israeli.

4“Ee Bwana , ulipotoka katika Seiri,

ulipopita katika mashamba ya Edomu,

nchi ilitetemeka, mbingu nazo zikamwaga,

naam, mawingu yakamwaga maji.

5Milima ilitetemeka mbele za Bwana , Yule wa Sinai,

mbele za Bwana , Mungu wa Israeli.

6“Katika siku za Shamgari mwana wa Anathi,

katika siku za Yaeli,

barabara kuu hazikuwa na watu;

wasafiri walipita njia za kando.

7Mashujaa walikoma katika Israeli,

walikoma hadi mimi, Debora, nilipoinuka,

nilipoinuka kama mama katika Israeli.

8Mungu alichagua viongozi wapya

vita vilipokuja malangoni ya mji;

lakini hapakuonekana ngao wala mkuki

miongoni mwa watu elfu arobaini katika Israeli.

9Moyo wangu u pamoja na wakuu wa Israeli,

u pamoja na wale wanaojitoa kwa hiari yao

miongoni mwa watu.

Mhimidini Bwana !

10“Ninyi mpandao punda weupe,

mkiketi juu ya matandiko ya thamani,

nanyi mnaotembea barabarani,

fikirini

11kuhusu sauti za waimbaji

mahali pa kunyweshea maji.

Wanasimulia matendo ya haki ya Bwana ,

matendo ya haki ya mashujaa wake

katika Israeli.

“Ndipo watu wa Bwana

walipoteremka malangoni pa mji.

12‘Amka, amka! Debora!

Amka, amka, uimbe!

Ee Baraka! Inuka,

chukua mateka wako uliowateka,

ee mwana wa Abinoamu.’

13“Ndipo mabaki ya watu

wakashuka dhidi ya wakuu,

watu wa Bwana wakashuka kwangu

dhidi ya wenye nguvu.

14Baadhi yao walitoka Efraimu,

ambao chimbuko lao ni Amaleki;

Benyamini alikuwa miongoni

mwa watu waliokufuata.

Kutoka Makiri wakashuka viongozi,

na kutoka Zabuloni wale washikao

fimbo ya jemadari.

15Wakuu wa Isakari walikuwa pamoja na Debora;

naam, Isakari alikuwa pamoja na Baraka,

wakija nyuma yake kwa mbio

wakielekea bondeni.

Katika jamaa za Reubeni,

palikuwa na kujihoji kukubwa moyoni.

16Kwa nini ulikaa katikati ya mazizi ya kondoo

kusikiliza sauti ya filimbi zinazoita makundi?

Kwa jamaa za Reubeni,

palikuwa na kujihoji kukubwa moyoni.

17Gileadi alikaa ngʼambo ya Yordani.

Naye Dani, kwa nini alikaa

kwenye merikebu siku nyingi?

Asheri alikaa kwa utulivu ufuoni mwa bahari,

akikaa kwenye ghuba zake ndogo.

18Watu wa Zabuloni walihatarisha maisha yao,

vilevile nao watu wa Naftali.

19“Wafalme walikuja na kufanya vita;

wafalme wa Kanaani walipigana

huko Taanaki, karibu na maji ya Megido,

lakini hawakuchukua nyara za fedha.

20Kutoka mbinguni nyota zilipigana,

nyota kutoka njia zake

zilipigana na Sisera.

21Mto wa Kishoni uliwasomba,

ule mto wa zamani, mto wa Kishoni.

Songa mbele, ee nafsi yangu,

kwa ujasiri!

22Ndipo kwato za farasi zikafanya mshindo:

farasi wake wenye nguvu

huenda mbio kwa kurukaruka.

23Malaika wa Bwana akasema, ‘Laani Merozi.

Laani watu wake kwa uchungu,

kwa kuwa hawakuja kumsaidia Bwana ,

kumsaidia Bwana dhidi ya hao wenye nguvu.’

24“Yaeli abarikiwe kuliko wanawake wote,

mkewe Heberi, Mkeni,

abarikiwe kuliko wanawake wote

wanaoishi kwenye mahema.

25Sisera alimwomba maji, naye akampa maziwa;

kwenye bakuli la heshima

akamletea maziwa mgando.

26Akanyoosha mkono wake

akashika kigingi cha hema,

mkono wake wa kuume

ukashika nyundo ya fundi.

Akampiga Sisera kwa nyundo,

akamponda kichwa chake,

akamvunjavunja na kumtoboa

paji lake la uso.

27Aliinama miguuni pa Yaeli,

akaanguka; akalala hapo.

Alipoinama miguuni pake,

alianguka;

pale alipoinamia, ndipo alipoanguka,

akiwa amekufa.

28“Kupitia dirishani mamaye Sisera alichungulia;

nyuma ya dirisha alilia, akasema,

‘Mbona gari lake la vita linachelewa kufika?

Mbona vishindo vya magari yake ya vita

vimechelewa?’

29Wajakazi wale wenye busara

kuliko wengine wote wanamjibu;

naam, naye anasema moyoni mwake,

30‘Je, hawapati na kugawanya nyara:

msichana mmoja au wawili kwa kila mtu,

mavazi ya rangi mbalimbali kwa Sisera kuwa nyara,

mavazi ya rangi mbalimbali yaliyotariziwa,

mavazi yaliyotariziwa vizuri kwa ajili ya shingo yangu:

haya yote yakiwa nyara?’

31“Adui zako wote na waangamie hivyo, Ee Bwana !

Bali wote wanaokupenda na wawe kama jua

linavyochomoza kwa nguvu zake.”

Hivyo nchi ikawa na amani kwa miaka arobaini.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.