Yeremia 14

Yeremia 14

Ukame, njaa na upanga

1Hili ndilo neno la Bwana kwa Yeremia kuhusu ukame:

2“Yuda anaomboleza,

kudhoofika kwa miji yake;

wanaomboleza kwa ajili ya nchi,

nacho kilio kinapanda kutoka Yerusalemu.

3Wakuu wanawatuma watumishi wao maji;

nao wanakwenda visimani

lakini huko hakuna maji.

Wanarudi na vyombo bila maji;

wakiwa na hofu na kukata tamaa,

wanafunika vichwa vyao.

4Ardhi imepasuka nyufa

kwa sababu hakuna mvua katika nchi;

wakulima wana hofu

na wanafunika vichwa vyao.

5Hata kulungu kondeni

anaacha kinda lake lililotoka kutotolewa

kwa sababu hakuna majani.

6Punda-mwitu wanasimama juu ya miinuko iliyo kame

na kutweta kama mbweha;

macho yao yanakosa nguvu za kuona

kwa sababu ya kukosa malisho.”

7Ingawa dhambi zetu zinashuhudia dhidi yetu,

Ee Bwana , tenda jambo kwa ajili ya jina lako.

Kwa kuwa kukengeuka kwetu ni kukubwa,

nasi tumetenda dhambi dhidi yako.

8Ee Tumaini la Israeli,

Mwokozi wake wakati wa taabu,

kwa nini unakuwa kama mgeni katika nchi,

kama msafiri anayekaa kwa usiku mmoja tu?

9Mbona unakuwa kama mtu aliyeshtukizwa,

kama shujaa asiye na uwezo wa kuokoa?

Wewe uko katikati yetu, Ee Bwana ,

nasi tunaitwa kwa jina lako;

usituache!

10Hili ndilo asemalo Bwana kuhusu watu hawa:

“Wanapenda sana kutangatanga,

hawaizuii miguu yao.

Hivyo Bwana hawakubali;

sasa ataukumbuka uovu wao

na kuwaadhibu kwa ajili ya dhambi zao.”

11Kisha Bwana akaniambia, “Usiombe kwa ajili ya mafanikio ya watu hawa.

12Ingawa wanafunga, sitasikiliza kilio chao; hata wakitoa dhabihu za kuteketezwa na dhabihu za nafaka, sitazikubali. Badala yake, nitawaangamiza kwa upanga, njaa na tauni.”

13Lakini nikasema, “Aa, Bwana Mwenyezi, manabii wanaendelea kuwaambia, ‘Hamtaona upanga wala kukabiliwa na njaa. Naam, nitawapa amani ya kudumu mahali hapa.’ ”

14Ndipo Bwana akaniambia, “Manabii wanatabiri uongo kwa jina langu. Sikuwatuma, wala sikuwachagua, wala sikusema nao. Wanawatabiria maono ya uongo, uaguzi usio na faida, udanganyifu wa mioyo yao, na ubatili.

15Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana kuhusu manabii wanaotabiri kwa jina langu: Mimi sikuwatuma, lakini wanasema, ‘Hakuna upanga wala njaa itakayoigusa nchi hii.’ Manabii hao hao watakufa kwa upanga na njaa.

16Nao watu hao wanaowatabiria watatupwa nje katika barabara za Yerusalemu kwa sababu ya njaa na upanga. Hapatakuwa na mtu wa kuwazika wao au wake zao, watoto wao wa kiume au wa kike. Nitawamwagia maafa wanayostahili.

17“Nena nao neno hili:

“ ‘Macho yangu na yatiririkwe na machozi

usiku na mchana bila kukoma;

kwa kuwa binti yangu aliye bikira, yaani watu wangu,

amepata jeraha baya,

pigo la kuangamiza.

18Ninapokwenda shambani,

ninaona wale waliouawa kwa upanga;

ninapokwenda mjini,

huko ninaona maangamizi ya njaa.

Nabii na kuhani kwa pamoja

wameenda katika nchi wasiyoijua.’ ”

19Je, umemkataa Yuda kabisa?

Umemchukia Sayuni kabisa?

Kwa nini umetuumiza

hata hatuwezi kuponyeka?

Tulitarajia amani,

lakini hakuna jema lililotujia;

tulitarajia wakati wa kupona

lakini kuna hofu kuu tu.

20Ee Bwana , tunatambua uovu wetu

na kosa la baba zetu;

kweli tumetenda dhambi dhidi yako.

21Kwa ajili ya jina lako usituchukie kabisa;

usikidharau kiti chako cha enzi kilichotukuka.

Kumbuka agano lako nasi

na usilivunje.

22Je, kuna sanamu batili yoyote ya mataifa

iwezayo kuleta mvua?

Je, anga peke yake zinaweza kuleta mvua?

La hasha! Ni wewe peke yako,

Ee Bwana , Mungu wetu.

Kwa hiyo tumaini letu liko kwako,

kwa kuwa wewe ndiwe ufanyaye haya yote.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.