Yeremia 2

Yeremia 2

Israeli amwacha Mungu

1Neno la Bwana lilinijia kusema,

2“Nenda ukahubiri masikioni mwa watu wa Yerusalemu:

“Hivi ndivyo asemavyo Bwana :

“ ‘Nakumbuka moyo wako wa uchaji katika ujana wako,

jinsi ulivyonipenda kama bibi arusi

na kunifuata katika jangwa lile lote,

katika nchi isiyopandwa mbegu.

3Israeli alikuwa mtakatifu kwa Bwana ,

kama malimbuko ya kwanza ya mavuno yake;

wote waliomwangamiza walihesabiwa kuwa na hatia,

nayo maafa yaliwakumba,’ ”

asema Bwana .

4Sikia neno la Bwana , ee nyumba ya Yakobo,

nanyi nyote jamaa za nyumba ya Israeli.

5Hivi ndivyo asemavyo Bwana :

“Je, baba zenu waliona kosa gani kwangu,

hata wakatangatanga mbali nami hivyo?

Walifuata sanamu batili,

nao wenyewe wakawa batili.

6Hawakuuliza, ‘Yuko wapi Bwana ,

aliyetupandisha kutoka Misri

na kutuongoza kupitia nyika kame,

kupitia nchi ya majangwa na mabonde,

nchi ya ukame na giza,

nchi ambayo hakuna mtu asafiriye ndani yake

wala hakuna mtu aishiye humo?’

7Niliwaleta katika nchi yenye wingi wa vitu

ili mpate kula matunda yake

na utajiri wa mazao yake.

Lakini mkaja na kuinajisi nchi yangu,

na kuufanya urithi wangu chukizo.

8Makuhani hawakuuliza,

‘Yuko wapi Bwana ?’

Wale wanaoshughulikia sheria hawakunijua mimi;

viongozi waliasi dhidi yangu.

Manabii walitabiri kwa jina la Baali,

wakifuata sanamu batili.

9“Kwa hiyo naleta tena mashtaka dhidi yako,”

asema Bwana .

“Nami nitaleta mashtaka dhidi ya watoto wa watoto wako.

10Vuka, nenda ngʼambo hadi pwani ya Kitimu nawe uangalie,[#2:10 yaani Kipro , kisiwa katika Bahari ya Mediterania]

tuma watu waende Kedari, wachunguze kwa makini,

uone kama kumeshawahi kuwa kitu kama hiki.

11Je, taifa limebadili miungu yake wakati wowote?

(Hata ingawa hao si miungu kamwe.)

Lakini watu wangu wamebadili Utukufu wao

kwa sanamu batili.

12Shangaeni katika hili, ee mbingu,

nanyi tetemekeni kwa hofu kuu,”

asema Bwana .

13“Watu wangu wametenda dhambi mbili:

Wameniacha mimi,

niliye chemchemi ya maji yaliyo hai,

nao wamejichimbia visima vyao wenyewe,

visima vilivyobomoka, visivyoweza kuhifadhi maji.

14Je, Israeli ni mtumishi, yaani mtumwa kwa kuzaliwa?

Kwa nini basi amekuwa mateka?

15Simba wamenguruma;

wamemngurumia.

Wameifanya nchi yake kuwa ukiwa;

miji yake imeteketezwa, nayo imeachwa haina watu.

16Pia watu wa Memfisi na Tapanesi[#2:16 yaani Nofu]

wamekupiga fuvu la kichwa.

17Je, hukujiletea hili wewe mwenyewe

kwa kumwacha Bwana , Mungu wako

alipowaongoza njiani?

18Sasa kwa nini uende Misri

kunywa maji ya Shihori?

Nawe kwa nini kwenda Ashuru

kunywa maji ya Mto?

19Uovu wako utakuadhibu;

kurudi nyuma kwako kutakukemea.

Basi kumbuka, utambue

jinsi lilivyo jambo ovu na chungu kwako

unapomwacha Bwana Mungu wako,

na kutokuwa na hofu yangu,”

asema Bwana, Bwana wa majeshi.

20“Zamani nilivunja nira yako

na kukatilia mbali vifungo vyako;

ukasema, ‘Sitakutumikia!’

Hakika, kwenye kila kilima kirefu

na chini ya kila mti uliotanda matawi yake

ulijilaza kama kahaba.

21Nilikupanda ukiwa mzabibu ulio bora sana,

mkamilifu na wa mbegu nzuri.

Ilikuwaje basi ukawa kinyume nami,

ukaharibika na kuwa mzabibu mwitu?

22Hata ujisafishe kwa magadi

na kutumia sabuni nyingi,

bado doa la hatia yako liko mbele zangu,”

asema Bwana Mwenyezi.

23“Wawezaje kusema, ‘Mimi si najisi,

sijawafuata Mabaali’?

Kumbuka jinsi ulivyotenda kule bondeni;

fikiri uliyoyafanya.

Wewe ni ngamia jike mwenye mbio

ukikimbia hapa na pale,

24punda-mwitu aliyezoea jangwa,

anayenusa upepo katika tamaa yake kubwa:

wakati wake wa kuhitaji mbegu

ni nani awezaye kumzuia?

Madume yoyote yanayomfuatilia

hayana haja ya kujichosha;

wakati wa kupandwa kwake yatampata tu.

25Usikimbie hadi miguu yako iwe haina viatu,

na koo lako liwe limekauka.

Lakini ulisema, ‘Haina maana!

Ninaipenda miungu ya kigeni,

nami lazima niifuatie.’

26“Kama vile mwizi anavyoaibika akikamatwa,

hivyo ndivyo nyumba ya Israeli inavyoaibishwa:

wao wenyewe, wafalme wao na maafisa wao,

makuhani wao na manabii wao.

27Wanaiambia miti, ‘Wewe ndiwe baba yangu,’

nalo jiwe, ‘Wewe ndiwe uliyenizaa.’

Wamenipa visogo vyao

wala hawakunigeuzia nyuso zao;

lakini wakiwa katika taabu, wanasema,

‘Njoo utuokoe!’

28Iko wapi basi ile miungu mliyojitengenezea?

Yenyewe na ije kama inaweza kuwaokoa

wakati mko katika taabu!

Kwa maana mna miungu mingi

kama mlivyo na miji, ee Yuda.

29“Kwa nini mnaleta mashtaka dhidi yangu?

Ninyi nyote mmeniasi,”

asema Bwana .

30“Nimeadhibu watu wako bure tu,

hawakujirekebisha.

Upanga wako umewala manabii wako

kama simba mwenye njaa.

31“Enyi wa kizazi hiki, tafakarini neno la Bwana :

“Je, nimekuwa jangwa kwa Israeli

au nchi ya giza nene?

Kwa nini watu wangu wanasema, ‘Sisi tuko huru kuzurura,

hatutarudi kwako tena’?

32Je, mwanamwali husahau vito vyake,

au bibi arusi mapambo yake ya arusi?

Lakini watu wangu wamenisahau mimi,

tena kwa siku zisizo na hesabu.

33Je, wewe una ustadi kiasi gani katika kufuatia mapenzi!

Hata wale wanawake wabaya kuliko wote

wanaweza kujifunza kutokana na njia zako.

34Katika nguo zako watu huona

damu ya uhai ya maskini wasio na hatia,

ingawa hukuwakamata wakivunja nyumba.

Lakini katika haya yote

35unasema, ‘Sina hatia;

Mungu hajanikasirikia.’

Lakini nitakuhukumu kwa sababu unasema,

‘Mimi sijatenda dhambi.’

36Kwa nini unatangatanga sana,

ukibadili njia zako?

Utakatishwa tamaa na Misri

kama ulivyokatishwa na Ashuru.

37Pia utaondoka mahali hapo

ukiwa umeweka mikono kichwani,

kwa kuwa Bwana amewakataa wale unaowatumainia;

hutasaidiwa nao.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.