Yeremia 28

Yeremia 28

Hanania nabii wa uongo

1Katika mwezi wa tano wa mwaka ule ule, yaani mwaka wa nne, mwanzoni mwa utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda, nabii Hanania mwana wa Azuri, ambaye alitoka Gibeoni, akaniambia katika nyumba ya Bwana mbele ya makuhani na watu wote:

2“Hili ndilo Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli asemalo: ‘Nitaivunja nira ya mfalme wa Babeli.

3Katika muda wa miaka miwili nitavirudisha mahali hapa vyombo vyote vya nyumba ya Bwana ambavyo Nebukadneza mfalme wa Babeli aliviondoa kutoka hapa na kuvipeleka Babeli.

4Pia nitamrudisha mahali hapa Yekonia mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, pamoja na wote waliohamishwa kutoka Yuda ambao walienda Babeli,’ asema Bwana , ‘kwa kuwa nitaivunja nira ya mfalme wa Babeli.’ ”[#28:4 au Konia ; pia anaitwa Yehoyakini]

5Ndipo nabii Yeremia akamjibu nabii Hanania mbele ya makuhani na watu wote waliokuwa wamesimama ndani ya nyumba ya Bwana .

6Akasema, “Amen! Bwana na afanye hivyo! Bwana na ayatimize maneno ya unabii uliyoyatoa kwa kuvirudisha mahali hapa kutoka Babeli vyombo vya nyumba ya Bwana na watu wote walio uhamishoni.

7Hata hivyo, nisikilize nikuambie yale nitakayoyasema masikioni mwako na masikioni mwa watu hawa wote:

8Tangu mwanzo, manabii waliokutangulia wewe na mimi walitabiri vita, maafa na tauni dhidi ya nchi nyingi na falme kubwa.

9Lakini nabii atakayetabiri amani atatambuliwa kuwa kweli ametumwa na Bwana ikiwa unabii wake utatimia.”

10Kisha nabii Hanania akaiondoa nira iliyokuwa shingoni mwa Yeremia na kuivunja,

11naye akasema mbele ya watu wote, “Hili ndilo asemalo Bwana : ‘Vivi hivi ndivyo nitakavyoivunja nira ya Nebukadneza mfalme wa Babeli kutoka shingo za mataifa katika muda huu wa miaka miwili.’ ” Alipofanya hivi, nabii Yeremia akaondoka zake.

12Kitambo kidogo baada ya nabii Hanania kuivunja nira kutoka shingo ya nabii Yeremia, neno la Bwana likamjia Yeremia:

13“Nenda ukamwambie Hanania, ‘Hili ndilo asemalo Bwana : Umevunja nira ya mti, lakini badala yake utapata nira ya chuma.

14Hili ndilo asemalo Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli: Nitaweka nira ya chuma kwenye shingo za mataifa haya yote ili kufanya yamtumikie Nebukadneza mfalme wa Babeli, nao watamtumikia. Pia nitampa kutawala hata wanyama pori.’ ”

15Kisha nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, “Sikiliza Hanania! Bwana hajakutuma, lakini wewe umelishawishi taifa hili kuamini uongo.

16Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana : ‘Hivi karibuni nitakuondoa duniani. Mwaka huu utakufa, kwa sababu umetangaza uasi dhidi ya Bwana .’ ”

17Katika mwezi wa saba wa mwaka ule ule, nabii Hanania akafa.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.