Yeremia 46

Yeremia 46

Ujumbe kuhusu Misri

1Hili ni neno la Bwana lililomjia nabii Yeremia kuhusu mataifa:

2Kuhusu Misri:

Huu ni ujumbe dhidi ya jeshi la Farao Neko mfalme wa Misri, lililoshindwa huko Karkemishi kwenye Mto Frati na Nebukadneza mfalme wa Babeli, katika mwaka wa nne wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda:

3“Wekeni tayari ngao zenu, kubwa na ndogo,

mtoke kwa ajili ya vita!

4Fungieni farasi lijamu,

pandeni farasi!

Shikeni nafasi zenu

mkiwa mmevaa chapeo!

Isugueni mikuki yenu,

vaeni dirii vifuani!

5Je, ninaona nini?

Wametiwa hofu,

wanarudi nyuma,

mashujaa wao wameshindwa.

Wanakimbia kwa haraka

pasipo kutazama nyuma,

tena kuna hofu kuu kila upande,”

asema Bwana .

6Walio wepesi na wenye mbio hawawezi kukimbia,

wala wenye nguvu hawawezi kutoroka.

Kaskazini, kando ya Mto Frati,

wanajikwaa na kuanguka.

7“Ni nani huyu ajiinuaye kama Mto Naili,

kama mito yenye maji yanayofanya mawimbi?

8Misri hujiinua kama Mto Naili,

kama mito yenye maji yanayofanya mawimbi.

Husema, ‘Nitainuka na kufunika dunia,

nitaiangamiza miji na watu wake.’

9Songeni mbele, enyi farasi!

Endesheni kwa kasi, enyi mnaoendesha magari ya vita!

Endeleeni mbele, enyi mashujaa:

wanaume wa Kushi na Putu mnaobeba ngao,

wanaume wa Ludi mnaovuta upinde.

10Lakini ile siku ni ya Bwana, Bwana wa majeshi,

siku ya kulipiza kisasi,

kisasi juu ya adui zake.

Upanga utakula hata utakapotosheka,

hadi utakapozima kiu yake kwa damu.

Kwa maana Bwana, Bwana wa majeshi,

atatoa dhabihu kwenye nchi ya kaskazini,

kando ya Mto Frati.

11“Panda hadi Gileadi ukapate zeri,

ee Bikira Binti Misri.

Lakini umetumia dawa nyingi bila mafanikio;

huwezi kupona.

12Mataifa yatasikia juu ya aibu yako,

kilio chako kitaijaza dunia.

Shujaa mmoja atajikwaa juu ya mwingine,

nao wataanguka chini pamoja.”

13Huu ndio ujumbe ambao Bwana alimwambia nabii Yeremia kuhusu kuja kwa Nebukadneza, mfalme wa Babeli ili kuishambulia Misri:

14“Tangaza hili katika Misri, nawe ulihubiri katika Migdoli,

hubiri pia katika Memfisi na Tapanesi:

‘Shikeni nafasi zenu na mwe tayari,

kwa kuwa upanga unawala wanaokuzunguka.’

15Kwa nini mashujaa wako wamesombwa

na kupelekwa mbali?

Hawawezi kusimama, kwa maana Bwana

atawasukuma awaangushe chini.

16Watajikwaa mara kwa mara,

wataangukiana wao kwa wao.

Watasema, ‘Amka, turudi

kwa watu wetu na nchi yetu,

mbali na upanga wa mtesi.’

17Huko watu watatangaza,

‘Farao, mfalme wa Misri, ni makelele tu,

muda alioandikiwa umekwisha.’

18“Kwa hakika kama niishivyo,” asema Mfalme,

ambaye jina lake ni Bwana wa majeshi,

“mmoja atakuja ambaye ni kama Tabori miongoni mwa milima,

kama Karmeli kando ya bahari.

19Funga mizigo yako kwenda uhamishoni,

wewe ukaaye Misri,

kwa kuwa Memfisi utaangamizwa

na kuwa magofu pasipo mkazi.

20“Misri ni mtamba mzuri,

lakini mbungʼo anakuja dhidi yake kutoka kaskazini.

21Askari wake waliokodiwa katika safu zake

wako kama ndama walionenepeshwa.

Wao pia watageuka na kukimbia pamoja,

hawataweza kuhimili vita,

kwa maana siku ya msiba inakuja juu yao,

wakati wao wa kuadhibiwa.

22Misri atatoa sauti kama ya nyoka anayekimbia

kadiri adui anavyowasogelea na majeshi,

watakuja dhidi yake wakiwa na mashoka,

kama watu wakatao miti.

23Wataufyeka msitu wake,”

asema Bwana ,

“hata kama umesongamana kiasi gani.

Ni wengi kuliko nzige,

hawawezi kuhesabika.

24Binti Misri ataaibishwa,

atatiwa mikononi mwa watu wa kaskazini.”

25Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema: “Ninakaribia kuleta adhabu juu ya Amoni mungu wa Thebesi, na juu ya Farao, juu ya Misri na miungu yake, na wafalme wake, pamoja na wanaomtegemea Farao.[#46:25 kwa Kiebrania ni No (au No-Amoni )]

26Nitawatia mikononi mwa wanaoutafuta uhai wao, yaani Nebukadneza mfalme wa Babeli na maafisa wake. Mwishowe, hata hivyo, Misri itakaliwa kama nyakati zilizopita,” asema Bwana .

27“Usiogope, ee Yakobo mtumishi wangu,

usifadhaike, ee Israeli.

Hakika nitakuokoa kutoka nchi za mbali,

uzao wako kutoka nchi walioishi uhamishoni.

Yakobo atakuwa tena na amani na salama,

wala hakuna hata mmoja atakayewatia hofu.

28Usiogope, ee Yakobo mtumishi wangu,

kwa maana mimi niko pamoja nawe,”

asema Bwana .

“Ingawa nitayaangamiza kabisa mataifa yote

ambayo miongoni mwake nimekutawanya,

sitakuangamiza wewe kabisa.

Nitakurudi, lakini kwa haki tu,

wala sitakuacha kabisa bila kukuadhibu.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.