The chat will start when you send the first message.
1Hili ndilo neno la Bwana lililomjia nabii Yeremia kuhusu Wafilisti, kabla Farao hajaishambulia Gaza:
2Hili ndilo asemalo Bwana :
“Tazama jinsi maji yanavyoinuka huko kaskazini,
yatakuwa mafuriko yenye nguvu sana.
Yataifurikia nchi na vitu vyote vilivyo ndani yake,
miji na wanaoishi ndani yake.
Watu watapiga kelele;
wote wanaoishi katika nchi wataomboleza
3kwa sauti ya kwato za farasi wanaoenda mbio,
kwa sauti ya magari ya vita ya adui,
na mngurumo wa magurudumu yake.
Baba hawatageuka kuwasaidia watoto wao,
mikono yao italegea.
4Kwa maana siku imewadia
kuwaangamiza Wafilisti wote
na kuwakatilia mbali walionusurika wote
ambao wangeweza kusaidia Tiro na Sidoni.
Bwana anakaribia kuwaangamiza Wafilisti,
mabaki toka pwani za Kaftori.
5Gaza atanyoa kichwa chake katika kuomboleza,
Ashkeloni atanyamazishwa.
Enyi mabaki kwenye tambarare,
mtajikatakata wenyewe hadi lini?
6“Mnalia, ‘Aa, upanga wa Bwana ,
utaendelea hadi lini ndipo upumzike?
Rudi ndani ya ala yako;
acha na utulie.’
7Lakini upanga utatuliaje
wakati Bwana ameuamuru,
wakati ameuagiza kuishambulia Ashkeloni
pamoja na pwani yake?”