Yeremia 48

Yeremia 48

Ujumbe kuhusu Moabu

1Kuhusu Moabu:

Hili ndilo Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asemalo:

“Ole wake Nebo, kwa maana utaharibiwa.

Kiriathaimu utaaibishwa na kutekwa;

Misgabu itaaibishwa na kuvunjavunjwa.

2Moabu haitasifiwa tena;

huko Heshboni watu watapanga jinsi ya kumwangusha:

‘Njooni na tuliangamize taifa lile.’

Wewe nawe, ee Madmena, utanyamazishwa;

upanga utakufuatia.

3Sikiliza kilio kutoka Horonaimu,

kilio cha maangamizi makuu na uharibifu.

4Moabu utavunjwa,

wadogo wake watapiga kelele.

5Wanapanda kwenda njia ya kuelekea Luhithi,

wakilia kwa uchungu wanapotembea,

kwenye njia inayoshuka kwenda Horonaimu,

kilio cha uchungu kwa ajili ya uharibifu kinasikika.

6Kimbieni! Okoeni maisha yenu,

kuweni kama kichaka jangwani.

7Kwa kuwa mmetumainia matendo yenu na mali yenu,

ninyi pia mtachukuliwa mateka,

naye Kemoshi ataenda uhamishoni,

pamoja na makuhani wake na maafisa wake.

8Mwangamizi atakuja dhidi ya kila mji,

wala hakuna mji utakaookoka.

Bonde litaangamizwa na uwanda utaharibiwa,

kwa sababu Bwana amesema.

9Wekeni chumvi kwa ajili ya Moabu,

kwa kuwa ataangamizwa;

miji yake itakuwa ukiwa,

hakutakuwa na mtu atakayeishi ndani yake.

10“Alaaniwe yeye afanyaye kazi ya Bwana kwa ulegevu!

Alaaniwe yeye auzuiaye upanga wake usimwage damu!

11“Moabu amestarehe tangu ujana wake,

kama divai iliyoachwa kwenye machujo yake,

haikumiminwa kutoka chombo kimoja hadi kingine,

hajaenda uhamishoni.

Kwa hiyo ana ladha ile ile kama aliyokuwa nayo,

nayo harufu yake haijabadilika.

12Lakini siku zinakuja,”

asema Bwana ,

“nitakapotuma watu wamiminao kutoka magudulia,

nao watamimina;

wataacha magudulia yake yakiwa matupu

na kuvunja mitungi yake.

13Kisha Moabu atamwonea aibu Kemoshi,

kama vile nyumba ya Israeli walivyoona aibu

walipotegemea Betheli.

14“Mwawezaje kusema, ‘Sisi ni mashujaa,

watu hodari katika vita’?

15Moabu ataangamizwa na miji yake itavamiwa,

vijana wake wa kiume walio bora sana watachinjwa,”

asema Mfalme, ambaye jina lake

ni Bwana wa majeshi.

16“Kuanguka kwa Moabu kumekaribia,

janga kubwa litamjia kwa haraka.

17Ombolezeni kwa ajili yake, ninyi nyote mnaomzunguka,

ninyi nyote mnaojua sifa zake,

semeni, ‘Tazama jinsi ilivyovunjika

fimbo ya kifalme yenye nguvu,

tazama jinsi ilivyovunjika

fimbo iliyotukuka!’

18“Shuka kutoka fahari yako

uketi katika ardhi iliyokauka,

enyi wenyeji wa Binti Diboni,

kwa maana yeye aangamizaye Moabu

atakuja dhidi yako,

na kuangamiza miji yako yenye ngome.

19Simama kando ya barabara na utazame,

wewe unayeishi Aroeri.

Muulize mwanaume anayekimbia

na mwanamke anayetoroka,

waulize, ‘Kumetokea nini?’

20Moabu amefedheheshwa, kwa kuwa amevunjavunjwa.

Lieni kwa huzuni na kupiga kelele!

Tangazeni kando ya Mto Arnoni

kwamba Moabu ameangamizwa.

21Hukumu imefika kwenye uwanda wa juu:

katika Holoni, Yahasa na Mefaathi,

22katika Diboni, Nebo

na Beth-Diblathaimu,

23katika Kiriathaimu, Beth-Gamuli

na Beth-Meoni,

24katika Keriothi na Bosra;

kwa miji yote ya Moabu,

iliyo mbali na karibu.

25Pembe ya Moabu imekatwa,[#48:25 pembe inawakilisha nguvu]

mkono wake umevunjwa,”

asema Bwana .

26“Mleweshe,

kwa kuwa amemdharau Bwana .

Moabu atagaagaa katika matapishi yake,

awe kichekesho.

27Je, Israeli hakuwa kitu chako cha kudhihakiwa?

Je, alikamatwa miongoni mwa wezi,

kiasi cha kutikisa kichwa chako kwa dharau

kila mara unapozungumza juu yake?

28Ondokeni miji yenu, mkaishi katikati ya miamba,

enyi mnaoishi Moabu.

Kuweni kama njiwa ambaye hutengeneza kiota chake

kwenye mlango wa pango.

29“Tumesikia kuhusu kiburi cha Moabu:

kutakabari kwake kwa kiburi na majivuno,

kiburi chake na ufidhuli wake,

na kujivuna kwa moyo wake.

30Ninaujua ujeuri wake, lakini ni bure,”

asema Bwana ,

“nako kujisifu kwake hakumsaidii chochote.

31Kwa hiyo namlilia Moabu,

kwa ajili ya Moabu yote ninalia,

ninaomboleza kwa ajili

ya watu wa Kir-Haresethi.

32Ninalia machozi kwa ajili yenu, kama Yazeri aliavyo,

enyi mizabibu ya Sibma.

Matawi yako yameenea hadi baharini;

yamefika hadi bahari ya Yazeri.

Mwangamizi ameyaangukia

matunda yako yaliyoiva

na mizabibu yako iliyoiva.

33Shangwe na furaha vimetoweka

kutoka bustani na mashamba ya Moabu.

Nimekomesha kutiririka kwa divai kutoka mashinikizo;

hakuna hata mmoja ayakanyagaye kwa kelele za shangwe.

Ingawa kuna kelele,

sio kelele za shangwe.

34“Sauti ya kilio chao inapanda

kutoka Heshboni hadi Eleale na Yahazi,

kutoka Soari hadi Horonaimu na Eglath-Shelishiya,

kwa kuwa hata maji ya Nimrimu yamekauka.

35Nitakomesha wote katika Moabu

watoao sadaka mahali pa juu pa kuabudia,

na kufukiza uvumba kwa miungu yao,”

asema Bwana .

36“Kwa hiyo moyo wangu unaomboleza kwa ajili ya Moabu kama filimbi;

unaomboleza kama filimbi kwa ajili ya watu wa Kir-Haresethi.

Utajiri waliojipatia umetoweka.

37Kila kichwa kimenyolewa

na kila mwenye ndevu zimekatwa;

kila mkono umekatwa

na kila kiuno kimevalishwa gunia.

38Juu ya mapaa yote katika Moabu

na katika viwanja

hakuna kitu isipokuwa maombolezo,

kwa kuwa nimemvunja Moabu

kama gudulia lisilotakiwa na mtu yeyote,”

asema Bwana .

39“Tazama jinsi alivyovunjikavunjika!

Jinsi wanavyolia kwa huzuni!

Tazama jinsi Moabu anavyogeuka kwa aibu!

Moabu amekuwa kitu cha kudhihakiwa,

kitu cha kutisha kwa wale wote

wanaomzunguka.”

40Hili ndilo asemalo Bwana :

“Tazama! Tai anashuka chini,

akitanda mabawa yake juu ya Moabu.

41Miji itatekwa na ngome zake

zitatwaliwa.

Katika siku hiyo, mioyo ya mashujaa wa Moabu

itakuwa kama moyo wa mwanamke katika uchungu wa kuzaa.

42Moabu ataangamizwa kama taifa

kwa sababu amemdharau Bwana .

43Hofu kuu, shimo na mtego vinawangojea,

enyi watu wa Moabu,”

asema Bwana .

44“Yeyote atakayeikimbia hiyo hofu kuu

ataanguka ndani ya shimo,

yeyote atakayepanda kutoka shimoni,

atanaswa katika mtego,

kwa sababu nitailetea Moabu

mwaka wa adhabu yake,”

asema Bwana .

45“Katika kivuli cha Heshboni,

wakimbizi wamesimama pasipo msaada,

kwa kuwa moto umezimika huko Heshboni,

Mwali wa moto kutoka katikati ya Sihoni;

unaunguza paji za nyuso za Wamoabu,

mafuvu ya wanaojivuna kwa kelele.

46Ole wako, ee Moabu!

Watu wa Kemoshi wameangamizwa;

watoto wako wa kiume wamepelekwa uhamishoni,

na binti zako wamechukuliwa mateka.

47“Lakini nitarudisha mateka wa Moabu,

katika siku zijazo,”

asema Bwana .

Huu ndio mwisho wa hukumu ya Moabu.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.