Yeremia 50

Yeremia 50

Ujumbe kuhusu Babeli

1Hili ndilo neno alilosema Bwana kupitia nabii Yeremia kuhusu Babeli na nchi ya Wakaldayo:

2“Tangazeni! Hubirini katikati ya mataifa,

Inueni bendera na mkahubiri;

msiache kitu chochote, bali semeni,

‘Babeli utatekwa;

Beli ataaibishwa,

Merodaki atajazwa na hofu kuu.

Sanamu zake zitaaibishwa

na vinyago vyake vitajazwa hofu kuu.’

3Taifa kutoka kaskazini litamshambulia,

na kuifanya nchi yake ukiwa.

Hakuna atakayeishi ndani yake,

watu na wanyama wataikimbia.

4“Katika siku hizo, wakati huo,”

asema Bwana ,

“watu wa Israeli pamoja na watu wa Yuda

wataenda wakilia ili kumtafuta Bwana Mungu wao.

5Wataulizia njia iendayo Sayuni

na kuelekeza nyuso zao huko.

Watakuja na kuambatana na Bwana

katika agano la milele

ambalo halitasahaulika.

6“Watu wangu wamekuwa kondoo waliopotea;

wachungaji wao wamewapotosha

na kuwafanya wazurure mlimani.

Walitangatanga juu ya mlima na kilima,

na kusahau mahali pao pa kupumzikia.

7Yeyote aliyewakuta aliwala;

adui zao walisema, ‘Sisi hatuna hatia,

kwa kuwa wao walitenda dhambi dhidi ya

Bwana , malisho yao halisi,

Bwana , aliye tumaini la baba zao.’

8“Kimbieni kutoka Babeli;

ondokeni katika nchi ya Wakaldayo,

kuweni kama mbuzi wale waongozao kundi.

9Kwa maana nitaamsha na kuleta dhidi ya Babeli

muungano wa mataifa makubwa kutoka nchi ya kaskazini.

Watashika nafasi zao dhidi yake,

naye kutokea kaskazini atatekwa.

Mishale yao itakuwa kama mishale ya mashujaa walio hodari,

ambao hawawezi kurudi mikono mitupu.

10Kwa hiyo Ukaldayo utatekwa nyara;

wote wanaouteka, watapata nyara za kutosha,”

asema Bwana .

11“Kwa sababu hushangilia na kufurahi,

wewe utekaye urithi wangu,

kwa sababu unachezacheza kama mtamba anayepura nafaka,

na kulia kama farasi dume,

12mama yako ataaibika mno,

yeye aliyekuzaa atatahayari.

Atakuwa mdogo kuliko mataifa mengine yote,

atakuwa nyika, nchi kame na jangwa.

13Kwa sababu ya hasira ya Bwana hatakaliwa na mtu,

lakini ataachwa ukiwa kabisa.

Wote watakaopita Babeli watatiwa hofu na kudhihaki

kwa sababu ya majeraha yake yote.

14“Shikeni nafasi zenu kuzunguka Babeli,

enyi nyote mvutao upinde.

Mpigeni! Msibakize mshale wowote,

kwa kuwa ametenda dhambi dhidi ya Bwana .

15Piga kelele dhidi yake kila upande!

Anajisalimisha, minara yake inaanguka,

kuta zake zimebomoka.

Kwa kuwa hiki ni kisasi cha Bwana ,

mlipizeni kisasi;

mtendeeni kama alivyowatendea wengine.

16Katilieni mbali mpanzi kutoka Babeli,

pamoja na mvunaji na mundu wake akivuna.

Kwa sababu ya upanga wa mdhalimu

kila mmoja na arejee kwa watu wake mwenyewe,

kila mmoja na akimbilie

kwenye nchi yake mwenyewe.

17“Israeli ni kundi lililotawanyika

ambalo simba wamelifukuzia mbali.

Wa kwanza kumla alikuwa mfalme wa Ashuru,

wa mwisho kuponda mifupa yake

alikuwa Nebukadneza mfalme wa Babeli.”

18Kwa hiyo hili ndilo Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asemalo:

“Nitamwadhibu mfalme wa Babeli na nchi yake

kama nilivyomwadhibu mfalme wa Ashuru.

19Lakini nitamrudisha Israeli katika malisho yake mwenyewe

naye atalisha huko Karmeli na Bashani;

njaa yake itashibishwa

juu ya vilima vya Efraimu na Gileadi.

20Katika siku hizo, wakati huo,”

asema Bwana ,

“uchunguzi utafanyika kwa ajili ya kosa la Israeli,

lakini halitaonekana,

na kwa ajili ya dhambi za Yuda,

lakini haitapatikana hata moja,

kwa kuwa nitawasamehe

mabaki nitakaowaacha.

21“Shambulieni nchi ya Merathaimu

na wale wanaoishi huko Pekodi.

Wafuatieni, waueni

na kuwaangamiza kabisa,”

asema Bwana .

“Fanyeni kila kitu nilichowaamuru.

22Kelele ya vita iko ndani ya nchi,

kelele ya maangamizi makuu!

23Tazama jinsi nyundo ya dunia yote

ilivyovunjika na kuharibika!

Tazama jinsi Babeli ilivyokuwa ukiwa

miongoni mwa mataifa!

24Nimetega mtego kwa ajili yako, ee Babeli,

nawe ukakamatwa kabla hujafahamu;

ulipatikana na ukakamatwa

kwa sababu ulimpinga Bwana .

25Bwana amefungua ghala lake la silaha

na kuzitoa silaha za ghadhabu yake,

kwa kuwa Bwana, Bwana wa majeshi,

anayo kazi ya kufanya

katika nchi ya Wakaldayo.

26Njooni dhidi yake kutoka mbali.

Zifungueni ghala zake za nafaka;

mlundikeni kama lundo la nafaka.

Mwangamizeni kabisa

na msimwachie mabaki yoyote.

27Waueni mafahali wake wachanga wote;

waacheni washuke machinjoni!

Ole wao! Kwa kuwa siku yao imewadia,

wakati wao wa kuadhibiwa.

28Wasikilizeni watoro na wakimbizi kutoka Babeli

wakitangaza katika Sayuni

jinsi Bwana Mungu wetu alivyolipiza kisasi,

kisasi kwa ajili ya Hekalu lake.

29“Waiteni wapiga mishale dhidi ya Babeli,

wote wavutao upinde.

Pigeni kambi kumzunguka kabisa,

asitoroke mtu yeyote.

Mlipizeni kwa matendo yake;

mtendeeni kama alivyotenda.

Kwa kuwa alimdharau Bwana ,

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.

30Kwa hiyo, vijana wake wanaume wataanguka barabarani;

askari wake wote watanyamazishwa siku ile,”

asema Bwana .

31“Tazama, niko kinyume nawe, ewe mwenye majivuno,”

asema Bwana, Bwana wa majeshi,

“kwa kuwa siku yako imewadia,

yaani wakati wako wa kuadhibiwa.

32Mwenye majivuno atajikwaa na kuanguka,

wala hakuna yeyote atakayemuinua;

nitawasha moto katika miji yake,

utakaowateketeza wote wanaomzunguka.”

33Hili ndilo asemalo Bwana wa majeshi:

“Watu wa Israeli wamedhulumiwa,

hata watu wa Yuda pia.

Wote waliowateka wamewashikilia sana,

wanakataa kuwaachia waende.

34Lakini Mkombozi wao ana nguvu;

Bwana wa majeshi ndilo jina lake.

Atatetea shauri lao kwa nguvu

ili alete amani nchini mwao,

lakini ataleta msukosuko

kwa wale wanaoishi Babeli.

35“Upanga dhidi ya Wakaldayo!”

asema Bwana ,

“dhidi ya wale wanaoishi Babeli,

na dhidi ya maafisa wake na wenye busara!

36Upanga dhidi ya manabii wake wa uongo!

Watakuwa wapumbavu.

Upanga dhidi ya mashujaa wake!

Watajazwa na hofu kuu

37Upanga dhidi ya farasi na magari yake ya vita

pamoja na askari wake wote wa kigeni katika safu zake!

Wao watakuwa kama wanawake.

Upanga dhidi ya hazina zake!

Hizo zitatekwa nyara.

38Ukame juu ya maji yake!

Nayo yatakauka.

Kwa kuwa ni nchi ya sanamu,

wao wanaenda wazimu kwa ajili ya sanamu.

39“Kwa hiyo, viumbe vya jangwani na fisi wataishi humo,

nao bundi watakaa humo.

Kamwe haitakaliwa tena

wala watu hawataishi humo kizazi hadi kizazi.

40Kama Mungu alivyoangamiza Sodoma na Gomora

pamoja na miji iliyokuwa jirani nayo,”

asema Bwana ,

“vivyo hivyo hakuna mtu atakayeishi humo.

Naam, hakuna mtu atakayekaa humo.

41“Tazama! Jeshi linakuja kutoka kaskazini;

taifa kubwa na wafalme wengi

wanaamshwa kutoka miisho ya dunia.

42Wamejifunga pinde na mikuki;

ni wakatili na hawana huruma.

Wanatoa sauti kama bahari inayounguruma

wanapoendesha farasi wao;

wanakuja kama watu waliojipanga tayari kwa vita

ili kukushambulia, ee Binti Babeli.

43Mfalme wa Babeli amesikia habari kuwahusu,

nayo mikono yake imelegea.

Uchungu umemshika,

maumivu kama ya mwanamke katika uchungu wa kuzaa.

44Kama simba anayepanda kutoka vichaka vya Yordani

kuja kwenye nchi ya malisho mengi,

ndivyo nitakavyomfukuza Babeli kutoka nchi yake ghafula.

Ni nani aliye mteule,

nitakayemweka kwa ajili ya jambo hili?

Ni nani aliye kama mimi,

na ni nani awezaye kunipinga?

Tena ni mchungaji yupi

awezaye kusimama kinyume nami?”

45Kwa hiyo, sikia ambacho Bwana amepanga dhidi ya Babeli,

kile alichokusudia dhidi ya nchi ya Wakaldayo:

Aliye mchanga katika kundi ataburutwa mbali.

Yeye ataharibu kabisa malisho yao kwa sababu yao.

46Kwa sauti ya kutekwa kwa Babeli, dunia itatetemeka;

kilio chake kitasikika pote miongoni mwa mataifa.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.