Yeremia 51

Yeremia 51

1Hili ndilo asemalo Bwana :

“Tazama nitaamsha roho ya mwangamizi

dhidi ya Babeli na wenyeji wa Leb-Kamai.

2Nitawatuma wageni Babeli

kumpepeta na kuiharibu nchi yake;

watampinga kila upande

katika siku ya maafa yake.

3Usimwache mpiga upinde afunge kamba upinde wake,

wala usimwache avae silaha zake.

Usiwaonee huruma vijana wake;

angamiza jeshi lake kabisa.

4Wataanguka barabarani waliouawa katika nchi ya Wakaldayo,

wakiwa na majeraha ya kutisha.

5Kwa maana Israeli na Yuda hawajaachwa

na Mungu wao, Bwana wa majeshi,

ingawa nchi yao imejaa uovu

mbele zake yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.

6“Kimbieni kutoka Babeli!

Okoeni maisha yenu!

Msiangamizwe kwa sababu ya dhambi zake.

Ni wakati wa kisasi cha Bwana ,

atamlipa kile anachostahili.

7Babeli alikuwa kikombe cha dhahabu katika mkono wa Bwana ;

aliufanya ulimwengu wote ulewe.

Mataifa walikunywa mvinyo wake;

kwa hiyo sasa wameingiwa na wazimu.

8Babeli ataanguka ghafula na kuvunjika.

Mwombolezeni!

Tafuteni zeri ya kutuliza maumivu yake,

labda anaweza kupona.

9“ ‘Tungemponya Babeli,

lakini hawezi kuponyeka;

tumwacheni, na kila mmoja wetu aende nchi yake mwenyewe,

kwa kuwa hukumu yake inafika angani,

inapanda juu hadi mawinguni.’

10“ ‘Bwana amethibitisha haki yetu;

njooni, tutangaze katika Sayuni

kitu ambacho Bwana Mungu wetu amefanya.’

11“Noeni mishale,

chukueni ngao!

Bwana amewaamsha wafalme wa Wamedi,

kwa sababu nia yake ni kuangamiza Babeli.

Bwana atalipiza kisasi,

kisasi kwa ajili ya Hekalu lake.

12Inueni bendera dhidi ya kuta za Babeli!

Imarisheni ulinzi,

wekeni walinzi,

andaeni waviziaji!

Bwana atatimiza kusudi lake,

amri yake juu ya watu wa Babeli.

13Wewe uishiye kando ya maji mengi

na uliye na wingi wa hazina,

mwisho wako umekuja,

wakati wako wa kukatiliwa mbali.

14Bwana wa majeshi

ameapa kwa nafsi yake mwenyewe:

‘Hakika nitakujaza na watu, kama kundi la nzige,

nao watashangilia kwa ushindi juu yako.’

15“Aliiumba dunia kwa uweza wake;

akaweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake,

na akazitandaza mbingu kwa ufahamu wake.

16Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma;

huyafanya mawingu yainuke kutoka miisho ya dunia.

Hupeleka miali ya radi pamoja na mvua,

naye huuleta upepo kutoka ghala zake.

17“Kila mtu ni mjinga na hana maarifa;

kila sonara ameaibishwa na sanamu zake.

Vinyago vyake ni vya udanganyifu;

havina pumzi.

18Ni ubatili tu, vitu vya kufanyia mzaha;

wakati wa hukumu yao, wataangamia.

19Yeye Aliye Fungu la Yakobo sivyo alivyo,

kwani ndiye Muumba wa vitu vyote,

pamoja na kabila la urithi wake:

Bwana wa majeshi ndilo jina lake.

20“Wewe ndiwe rungu langu la vita,

silaha yangu ya vita:

kwa wewe navunjavunja mataifa,

kwa wewe naangamiza falme,

21kwa wewe navunjavunja

farasi na mpanda farasi,

kwa wewe navunjavunja

gari la vita na mwendeshaji wake,

22kwa wewe napondaponda

mwanaume na mwanamke,

kwa wewe napondaponda

mzee na kijana,

kwa wewe napondaponda

kijana wa kiume na mwanamwali,

23kwa wewe nampondaponda

mchungaji na kundi,

kwa wewe nampondaponda

mkulima na maksai,

kwa wewe nawapondaponda

watawala na maafisa.

24“Mbele ya macho yako nitamlipiza Babeli na wote wanaoishi Ukaldayo kwa ajili ya makosa yote waliyofanya katika Sayuni,” asema Bwana .

25“Mimi niko kinyume nawe, ee mlima unaoharibu,

wewe uangamizaye dunia yote,”

asema Bwana .

“Nitanyoosha mkono wangu dhidi yako,

nikuvingirishe kutoka kilele cha mwamba,

na kukufanya mlima ulioteketezwa kwa moto.

26Hakuna jiwe litakalochukuliwa kutoka kwako

kwa ajili ya kufanywa jiwe la pembeni,

wala jiwe lolote kwa ajili ya msingi,

kwa maana utakuwa ukiwa milele,”

asema Bwana .

27“Inueni bendera katika nchi!

Pigeni tarumbeta katikati ya mataifa!

Andaeni mataifa kwa ajili ya vita dhidi yake,

iteni falme hizi dhidi yake:

Ararati, Mini na Ashkenazi.

Wekeni jemadari dhidi yake,

pelekeni farasi wengi kama kundi la nzige.

28Andaeni mataifa kwa ajili ya vita dhidi yake,

wafalme wa Wamedi,

watawala wao na maafisa wao wote,

pamoja na nchi zote wanazotawala.

29Nchi inatetemeka na kugaagaa,

kwa kuwa makusudi ya Bwana dhidi ya Babeli yanasimama:

yaani kuangamiza nchi ya Babeli

ili pasiwepo atakayeishi humo.

30Mashujaa wa Babeli wameacha kupigana,

wamebaki katika ngome zao.

Nguvu zao zimekwisha,

wamekuwa kama wanawake.

Makazi yake yameteketezwa kwa moto,

makomeo ya malango yake yamevunjika.

31Tarishi mmoja humfuata mwingine,

na mjumbe humfuata mjumbe,

kumtangazia mfalme wa Babeli

kwamba mji wake wote umetekwa,

32Vivuko vya mito vimekamatwa,

mabwawa yenye mafunjo yametiwa moto,

nao askari wameingiwa na hofu kuu.”

33Hili ndilo Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asemalo:

“Binti Babeli ni kama sakafu ya kupuria

wakati inapokanyagwa;

wakati wa kumvuna utakuja upesi.”

34“Nebukadneza mfalme wa Babeli ametula,

ametufanya tuchangayikiwe,

ametufanya tuwe gudulia tupu.

Ametumeza kama mnyama wa baharini,

na kujaza tumbo lake kwa vyakula vyetu vizuri,

kisha akatutapika.

35Jeuri iliyotendewa miili yetu na iwe juu ya Babeli,”[#51:35 au Jeuri tuliyotendewa sisi na watoto wetu]

ndivyo wasemavyo wakaaji wa Sayuni.

“Damu yetu na iwe juu ya wakaaji wa Babeli,”

asema Yerusalemu.

36Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana :

“Tazama, nitakutetea

na kukulipizia kisasi;

nitaikausha bahari yake

na kuzikausha chemchemi zake.

37Babeli utakuwa lundo la magofu

na makao ya mbweha,

kitu cha kutisha na kudharauliwa,

mahali asipoishi mtu.

38Watu wake wote wananguruma kama simba wadogo,

wanakoroma kama wana simba.

39Lakini wakiwa wameamshwa,

nitawaandalia karamu

na kuwafanya walewe,

ili washangilie kwa kicheko,

kisha walale milele na wasiamke,”

asema Bwana .

40“Nitawateremsha kama wana-kondoo

wanaoenda machinjoni,

kama kondoo dume na mbuzi.

41“Tazama jinsi Sheshaki atakavyokamatwa,[#51:41 Sheshaki ni Babeli kwa fumbo.]

majivuno ya dunia yote yatakavyonyakuliwa.

Babeli atakuwa mwenye hofu kiasi gani

kati ya mataifa!

42Bahari itainuka juu ya Babeli;

mawimbi yake yanayonguruma yatamfunika.

43Miji yake itakuwa ukiwa,

kame na jangwa,

nchi isiyokuwa na mtu anayeishi ndani yake,

ambayo hakuna mwanadamu atakayepita humo.

44Nitamwadhibu Beli katika Babeli,

na kumfanya atapike kitu alichokimeza.

Mataifa hayatamiminika tena kwake.

Nao ukuta wa Babeli utaanguka.

45“Tokeni ndani yake, enyi watu wangu!

Okoeni maisha yenu!

Ikimbieni hasira kali ya Bwana .

46Msikate tamaa wala msiogope tetesi

zitakaposikika katika nchi;

tetesi moja inasikika mwaka huu,

nyingine mwaka unaofuata;

tetesi juu ya jeuri katika nchi,

na ya mtawala dhidi ya mtawala.

47Kwa kuwa hakika wakati utawadia

nitakapoziadhibu sanamu za Babeli;

nchi yake yote itatiwa aibu,

na watu wake wote waliouawa

wataangukia ndani yake.

48Ndipo mbingu na dunia na vyote vilivyomo

vitapiga kelele za shangwe juu ya Babeli,

kwa kuwa kutoka kaskazini

waangamizi watamshambulia,”

asema Bwana .

49“Babeli ni lazima aanguke kwa sababu ya kuwaua Waisraeli,

kama vile waliouawa duniani kote

walivyoanguka kwa sababu ya Babeli.

50Wewe uliyepona upanga,

ondoka wala usikawie!

Mkumbuke Bwana ukiwa katika nchi ya mbali,

na utafakari juu ya Yerusalemu.”

51“Tumetahayari, kwa sababu tumetukanwa

na aibu imefunika nyuso zetu,

kwa sababu wageni wameingia

mahali patakatifu pa nyumba ya Bwana .”

52“Lakini siku zinakuja,” asema Bwana ,

“nitakapoziadhibu sanamu zake,

na katika nchi yake yote

waliojeruhiwa watalia kwa maumivu makali.

53Hata kama Babeli ikifika angani

na kuziimarisha ngome zake ndefu,

nitatuma waangamizi dhidi yake,”

asema Bwana .

54“Sauti ya kilio inasikika kutoka Babeli,

sauti ya uharibifu mkuu

kutoka nchi ya Wakaldayo.

55Bwana ataiangamiza Babeli,

atanyamazisha makelele ya kishindo chake.

Mawimbi ya adui yatanguruma kama maji makuu,

ngurumo ya sauti zao itavuma.

56Mwangamizi atakuja dhidi ya Babeli;

mashujaa wake watakamatwa,

nazo pinde zao zitavunjwa.

Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa kisasi,

yeye atalipiza kikamilifu.

57Nitawafanya maafisa wake na wenye busara walewe,

watawala wao, maafisa, pamoja na mashujaa wao;

watalala milele na hawataamka,”

asema Mfalme, ambaye jina lake ni Bwana wa majeshi.

58Hili ndilo asemalo Bwana wa majeshi:

“Ukuta mnene wa Babeli utasawazishwa,

na malango yaliyoinuka yatateketezwa kwa moto;

mataifa yanajichosha bure,

taabu ya mataifa ni nishati tu ya miali ya moto.”

59Huu ndio ujumbe ambao nabii Yeremia alimpa msimamizi wa nyumba ya mfalme, Seraya mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, alipokwenda Babeli pamoja na Sedekia mfalme wa Yuda, katika mwaka wa nne wa utawala wake.

60Yeremia alikuwa ameandika ndani ya kitabu kuhusu maafa yote yatakayoipata Babeli, yaani yote yaliyokuwa yameandikwa kuhusu Babeli.

61Yeremia akamwambia Seraya, “Utakapofika Babeli, hakikisha kwamba umesoma maneno haya yote kwa sauti kubwa.

62Kisha sema, ‘Ee Bwana , umesema utaangamiza mahali hapa ili mtu wala mnyama asiishi ndani yake, napo patakuwa ukiwa milele.’

63Utakapomaliza kusoma hiki kitabu, kifungie jiwe kisha ukitupe ndani ya Mto Frati.

64Kisha sema, ‘Hivi ndivyo Babeli utakavyozama na usiinuke tena, kwa sababu ya maafa nitakayoleta juu yake. Nao watu wake wataanguka.’ ”

Maneno ya Yeremia yanaishia hapa.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.