Yeremia 9

Yeremia 9

1Laiti kichwa changu kingekuwa chemchemi ya maji

na macho yangu yangekuwa kisima cha machozi!

Ningelia usiku na mchana

kwa kuuawa kwa watu wangu.

2Laiti ningekuwa na nyumba

ya kukaa wasafiri jangwani,

ningewaacha watu wangu

na kwenda mbali nao,

kwa kuwa wote ni wazinzi,

kundi la watu wadanganyifu.

3“Huweka tayari ndimi zao kama upinde,

ili kurusha uongo;

wamekuwa na nguvu katika nchi

lakini si katika ukweli.

Wanatoka dhambi moja hadi nyingine,

hawanitambui mimi,”

asema Bwana .

4“Jihadhari na rafiki zako;

usiwaamini ndugu zako.

Kwa kuwa kila ndugu ni mdanganyifu,

na kila rafiki ni msingiziaji.

5Rafiki humdanganya rafiki,

hakuna yeyote asemaye kweli.

Wamefundisha ndimi zao kudanganya,

wanajichosha wenyewe katika kutenda dhambi.

6Unakaa katikati ya udanganyifu;

katika udanganyifu wao wanakataa kunitambua mimi,”

asema Bwana .

7Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana wa majeshi:

“Tazama, nitawasafisha na kuwajaribu,

kwani ni nini kingine niwezacho kufanya

kwa sababu ya dhambi ya watu wangu?

8Ndimi zao ni mshale wenye sumu,

hunena kwa udanganyifu.

Kwa kinywa chake kila mmoja huzungumza maneno mazuri na jirani yake,

lakini moyoni mwake humtegea mtego.

9Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya jambo hili?”

asema Bwana .

“Je, nisijilipizie kisasi

kwa taifa kama hili?”

10Nitalia na kuomboleza kwa ajili ya milima

na kuomboleza kuhusu malisho ya jangwani.

Yamekuwa ukiwa, wala hakuna apitaye humo,

milio ya ngʼombe haisikiki.

Ndege wa angani wametoroka

na wanyama wamekimbia.

11“Nitaifanya Yerusalemu lundo la magofu,

makao ya mbweha;

nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa,

asiwepo atakayeishi humo.”

12Ni mtu yupi aliye na hekima ya kutosha ayaelewe haya? Ni nani aliyefundishwa na Bwana awezaye kuyaeleza haya? Kwa nini nchi imeharibiwa na kufanywa ukiwa kama jangwa ambapo hakuna awezaye kupita?

13Bwana akasema, “Ni kwa sababu wameiacha sheria yangu, niliyoiweka mbele yao: hawajaniheshimu mimi wala kufuata sheria yangu.

14Badala yake wamefuata ukaidi wa mioyo yao, wamefuata Mabaali, kama baba zao walivyowafundisha.”

15Kwa hiyo, hivi ndivyo asemavyo Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli: “Tazama, nitawafanya watu hawa wale chakula kichungu na kunywa maji yenye sumu.

16Nitawatawanya katika mataifa ambayo wao wala baba zao hawakuyajua, nikiwafuata kwa upanga hadi niwaangamize kabisa.”

17Hivi ndivyo asemavyo Bwana wa majeshi:

“Fikiri sasa! Waite wanawake waombolezaji waje,

waite wale walio na ustadi kati yao.

18Nao waje upesi

waomboleze juu yetu,

hadi macho yetu yatiririke machozi

na kope zetu zibubujike maji.

19Sauti ya kuomboleza imesikika kutoka Sayuni:

‘Tazama jinsi tulivyoangamizwa!

Tazama jinsi aibu yetu ilivyo kubwa!

Ni lazima tuihame nchi yetu

kwa sababu nyumba zetu zimekuwa magofu.’ ”

20Basi, enyi wanawake, sikieni neno la Bwana ;

fungueni masikio yenu msikie maneno ya kinywa chake.

Wafundisheni binti zenu kuomboleza;

fundishaneni kila mmoja na mwenzake maombolezo.

21Mauti imeingia ndani kupitia madirishani,

imeingia kwenye majumba yetu ya fahari;

imewakatilia mbali watoto katika barabara

na vijana wa kiume kutoka viwanja vya miji.

22Sema, “Hili ndilo asemalo Bwana :

“ ‘Mizoga ya watu italala

kama kinyesi katika mashamba,

kama malundo ya nafaka nyuma ya mvunaji,

wala hakuna atakayeikusanya.’ ”

23Hili ndilo asemalo Bwana :

“Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake,

au mwenye nguvu ajisifu katika nguvu zake,

wala tajiri ajisifu katika utajiri wake,

24lakini yeye ajisifuye, na ajisifu kwa sababu hii:

kwamba ananifahamu na kunijua mimi,

kwamba mimi ndimi Bwana , nitendaye wema,

hukumu na haki duniani,

kwa kuwa napendezwa na haya,”

asema Bwana .

25“Siku zinakuja, nitakapowaadhibu wale wote ambao wametahiriwa kimwili tu, asema Bwana ,

26yaani Misri, Yuda, Edomu, Amoni, Moabu na wote wanaoishi jangwani sehemu za mbali. Kwa maana mataifa haya yote hayakutahiriwa mioyo yao, nayo nyumba yote ya Israeli haikutahiriwa.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.