Ayubu 18

Ayubu 18

Bildadi anasema: Mungu huwaadhibu waovu

1Bildadi Mshuhi akajibu:

2“Je, ni lini utafika mwisho wa maneno haya?

Uwe mwenye busara, nasi ndipo tutakapoweza kuongea.

3Kwa nini sisi tunafikiriwa kama wanyama,

na kuonekana wajinga machoni pako?

4Wewe unayejirarua mwenyewe vipande vipande

katika hasira yako,

je, dunia iachwe kwa ajili yako wewe?

Au ni lazima miamba iondolewe mahali pake?

5“Taa ya mwovu imezimwa,

nao mwali wa moto wake umezimika.

6Mwanga kwenye hema lake umekuwa giza;

taa iliyo karibu naye imezimika.

7Nguvu za hatua zake zimedhoofishwa;

hila zake mwenyewe zinamwangusha.

8Miguu yake imemsukumia kwenye wavu,

naye anatangatanga kwenye matundu ya wavu.

9Tanzi litamkamata kwenye kisigino;

mtego utamshikilia kwa nguvu.

10Kitanzi kimefichwa ardhini kwa ajili yake;

mtego uko kwenye njia yake.

11Vitisho vimemtia hofu kila upande,

na adui zake humwandama kila hatua.

12Janga linamwonea shauku;

maafa yako tayari kwa ajili yake aangukapo.

13Nayo yatakula sehemu ya ngozi yake;

mzaliwa wa kwanza wa mauti atakula maungo yake.

14Atangʼolewa kutoka usalama wa hema lake,

na kupelekwa kwa mfalme wa vitisho.

15Moto utakaa katika hema lake;

moto wa kiberiti utamwagwa juu ya makao yake.

16Mizizi yake chini itakauka

na matawi yake juu yatanyauka.

17Kumbukumbu lake litatoweka katika dunia,

wala hatakuwa na jina katika nchi.

18Ameondolewa nuruni na kusukumiwa gizani,

naye amefukuzwa mbali atoke duniani.

19Hana mtoto wala mzao miongoni mwa watu wake,

wala aliyenusurika mahali alipoishi.

20Watu wa magharibi watashangaa yaliyompata;

watu wa mashariki watapatwa na hofu.

21Hakika ndivyo yalivyo makao ya mtu mwovu;

ndivyo palivyo mahali pake mtu asiyemjua Mungu.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.