The chat will start when you send the first message.
1Kisha Ayubu akajibu:
2“Laiti uchungu wangu ungeweza kupimwa,
nayo taabu yangu yote ingewekwa kwenye mizani!
3Kwa kuwa hakika ingekuwa nzito kuliko mchanga wa bahari zote,
kwa hiyo si ajabu maneno yangu yamekuwa ya haraka.
4Mishale ya Mwenyezi iko ndani yangu,
roho yangu inakunywa sumu yake;
vitisho vya Mungu vimejipanga dhidi yangu.
5Je, punda-mwitu hulia akiwa na majani,
au fahali hulia akiwa na chakula?
6Je, chakula kisicho na ladha huliwa bila chumvi,
au upo utamu katika ute mweupe wa yai?
7Ninakataa kuvigusa;
vyakula vya aina hii hunichukiza.
8“Laiti ningepata haja yangu,
kwamba Mungu angenijalia hilo nililotarajia,
9kwamba Mungu angekuwa radhi kuniponda,
kuuachia mkono wake na kunikatilia mbali!
10Ndipo bado ningekuwa na hii faraja,
furaha yangu katika maumivu makali:
kwamba sikuwa nimeyakana maneno yake yeye Aliye Mtakatifu.
11“Nina nguvu gani, hata niendelee kutumaini?
Matazamio yangu ni nini,
hata niendelee kuwa mvumilivu?
12Je, mimi nina nguvu za jiwe?
Je, mwili wangu ni shaba?
13Je, ninao uwezo wowote wa kujisaidia mimi mwenyewe,
wakati mafanikio yamefukuziwa mbali nami?
14“Mtu anayekata tamaa angetazamia moyo wa kujitoa wa rafiki zake,
hata akiacha uchaji wa Mwenyezi.
15Lakini ndugu zangu sio wa kutegemewa,
ni kama vijito vya msimu,
ni kama vijito ambavyo hufurika
16wakati vimefunikwa barafu iyeyukayo,
ambavyo hujazwa na theluji inayoyeyuka,
17lakini hukauka majira ya ukame,
na wakati wa hari hutoweka katika mikondo yake.
18Misafara hugeuka kutoka njia zake;
hukwea kwenda kwenye nchi ya ukiwa na kuangamia.
19Misafara ya Tema inatafuta maji,
wafanyabiashara wa Sheba wanaosafiri
hutazama kwa matarajio.
20Wamedhikika, kwa sababu walikuwa na matumaini;
wanafika huko, lakini wanahuzunika
kwa kukosa walichotarajia.
21Sasa nanyi mmethibitika
kwamba hamna msaada wowote;
mnaona jambo la kutisha,
nanyi mnaogopa.
22Je, nimewahi kusema, ‘Toeni kitu kwa ajili yangu,
au mnilipie fidia kutoka mali yenu,
23au niokoeni mikononi mwa adui,
au nikomboeni kutoka makucha ya wasio na huruma’?
24“Nifundisheni, nami nitakaa kimya;
nionesheni nilikokosea.
25Tazama yalivyo ya kuumiza maneno ya kweli!
Lakini mabishano yenu yanathibitisha nini?
26Je, mna maana ya kuyasahihisha ninayosema,
na kuyafanya maneno ya mtu anayekata tamaa kama upepo?
27Mngeweza hata kupiga kura kwa ajili ya yatima,
na kubadilishana rafiki yenu na mali.
28“Lakini sasa kuweni na huruma mkaniangalie mimi.
Je, ningeweza kusema uongo mbele zenu?
29Tulizeni hasira, msiwe wadhalimu;
angalieni tena, kwa maana nimehatarisha uadilifu wangu.
30Je, pana uovu wowote mdomoni mwangu?
Je, kinywa changu hakiwezi kupambanua hila?