The chat will start when you send the first message.
1Akiwa ndani ya tumbo la samaki, Yona alimwomba Bwana Mungu wake.
2Akasema:
“Katika shida yangu nalimwita Bwana ,
naye akanijibu.
Kutoka kina cha kaburi niliomba msaada,
nawe ukasikiliza kilio changu.
3Ulinitupa kwenye kilindi,
ndani kabisa ya moyo wa bahari,
mikondo ya maji ilinizunguka;
mawimbi yako yote na viwimbi
vilipita juu yangu.
4Nikasema, ‘Nimefukuziwa
mbali na uso wako,
hata hivyo nitatazama tena
kuelekea Hekalu lako takatifu.’
5Maji yaliyonimeza yalinitisha,
kilindi kilinizunguka;
mwani ulijisokota kichwani pangu.
6Nilizama chini sana hata pande za mwisho za milima,
makomeo ya hiyo nchi yalinifungia hata milele.
Lakini uliuleta uhai wangu kutoka shimoni,
Ee Bwana Mungu wangu.
7“Uhai wangu ulipokuwa unatoka,
nilikukumbuka wewe, Bwana ,
nayo maombi yangu yalikufikia wewe,
katika Hekalu lako takatifu.
8“Wale watu wanaoshikilia sanamu batili
hupoteza neema yao.
9Lakini mimi nitakutolea dhabihu,
kwa sauti za shukrani na shangwe.
Lile nililowekea nadhiri nitalitimiza.
Wokovu watoka kwa Bwana .”
10Basi Bwana akamwamuru yule samaki, naye akamtapika Yona katika nchi kavu.