Yoshua 14

Yoshua 14

Mgawanyo wa nchi magharibi mwa Yordani

1Basi haya ndio maeneo Waisraeli waliyapokea kama urithi katika nchi ya Kanaani, ambayo kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa koo za makabila ya Israeli waliwagawia.

2Urithi wao uligawanywa kwa kura kwa yale makabila tisa na nusu, kama Bwana alivyoamuru Musa.

3Musa alikuwa amewapa yale makabila mawili na nusu urithi wao upande wa mashariki mwa Yordani, lakini Walawi hawakupewa urithi miongoni mwa hao wengine,

4kwa kuwa wana wa Yusufu walikuwa makabila mawili; Manase na Efraimu. Walawi hawakupata mgawo wa ardhi, bali walipewa miji tu kwa ajili ya kuishi, pamoja na maeneo ya malisho kwa ajili ya mifugo yao na mali zao.

5Kwa hiyo Waisraeli wakagawana ile nchi, kama vile Bwana alivyomwagiza Musa.

Kalebu anapewa mji wa Hebroni

6Kisha watu wa Yuda wakamwendea Yoshua huko Gilgali, naye Kalebu mwana wa Yefune yule Mkenizi, akamwambia, “Unajua jambo ambalo Bwana alimwambia Musa mtu wa Mungu huko Kadesh-Barnea kukuhusu wewe na mimi.

7Nilikuwa na umri wa miaka arobaini, wakati Musa mtumishi wa Bwana , aliponituma kutoka Kadesh-Barnea kuipeleleza hiyo nchi. Nami nikamletea taarifa kama kulingana na nilivyosadiki moyoni.

8Lakini ndugu zangu tuliopanda nao waliifanya mioyo ya watu iyeyuke kwa hofu. Bali mimi, nilimfuata Bwana Mungu wangu kwa moyo wote.

9Hivyo katika siku ile, Musa akaniapia, ‘Nchi ambayo umeikanyaga kwa miguu yako itakuwa urithi wako na wa watoto wako milele, kwa sababu umemfuata Bwana Mungu wangu kwa moyo wote.’[#14:9 Kum 1:36]

10“Sasa basi, kama vile Bwana alivyoahidi, ameniweka hai kwa miaka arobaini na tano tangu alipomwambia Musa jambo hili, Waisraeli walipokuwa wanazunguka jangwani. Hivyo mimi hapa leo nina umri wa miaka themanini na tano!

11Bado nina nguvu kama siku ile Musa aliponituma; nina nguvu za kwenda vitani sasa kama nilivyokuwa wakati ule.

12Basi nipe nchi hii ya vilima, ambayo Bwana aliniahidi siku ile. Wewe mwenyewe ulisikia wakati ule kwamba Waanaki walikuwa huko na miji yao ilikuwa mikubwa na yenye ngome, lakini, kwa msaada wa Bwana , nitawafukuza watoke huko kama vile alivyonena.”

13Ndipo Yoshua akambariki Kalebu mwana wa Yefune, na akampa Hebroni kama urithi wake.

14Hivyo Hebroni imekuwa mali ya Kalebu mwana wa Yefune Mkenizi tangu wakati ule, kwa sababu alimwandama Bwana , Mungu wa Israeli, kwa moyo wote.

15(Hebroni uliitwa Kiriath-Arba hapo mwanzo, kuitanishwa na Arba aliyekuwa mtu mkuu kupita wote miongoni mwa Waanaki.)

Kisha nchi ikawa na amani bila vita.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.