Maombolezo 2

Maombolezo 2

1Tazama jinsi Bwana alivyomfunika Binti Sayuni

kwa wingu la hasira yake!

Ameitupa chini fahari ya Israeli

kutoka mbinguni hadi duniani,

hakukumbuka kiti chake cha kuwekea miguu

katika siku ya hasira yake.

2Bila huruma Bwana ameyameza

makao yote ya Yakobo;

katika ghadhabu yake amebomoa

ngome za Binti Yuda.

Ameuangusha ufalme wake na wakuu wake

chini kwa aibu.

3Katika hasira kali amevunja

kila pembe ya Israeli.

Ameuondoa mkono wake wa kuume

alipokaribia adui.

Amemteketeza Yakobo kama moto uwakao

ule uteketezao kila kitu kinachouzunguka.

4Ameupinda upinde wake kama adui,

mkono wake wa kuume uko tayari.

Kama vile adui amewaua

wote waliokuwa wanapendeza jicho,

amemwaga ghadhabu yake kama moto

juu ya hema la Binti Sayuni.

5Bwana ni kama adui;

amemmeza Israeli.

Ameyameza majumba yake yote ya kifalme

na kuangamiza ngome zake.

Ameongeza huzuni na maombolezo

kwa Binti Yuda.

6Ameharibu maskani yake kama bustani,

ameharibu mahali pake pa mkutano.

Bwana amemfanya Sayuni kusahau

sikukuu zake zilizoamriwa na Sabato zake;

katika hasira yake kali amewadharau

mfalme na kuhani.

7Bwana amekataa madhabahu yake

na kuacha mahali patakatifu pake.

Amemkabidhi adui kuta

za majumba yake ya kifalme;

wameshangilia katika nyumba ya Bwana

kama katika siku ya sikukuu iliyoamriwa.

8Bwana alikusudia kuangusha

ukuta uliomzunguka Binti Sayuni.

Ameinyoosha kamba ya kupimia

na hakuuzuia mkono wake usiangamize.

Alifanya maboma na kuta ziomboleze,

vyote vikaharibika pamoja.

9Malango yake yamezama ardhini,

makomeo yake ameyavunja na kuyaharibu.

Mfalme wake na wakuu wake wamepelekwa uhamishoni

miongoni mwa mataifa,

sheria haipo tena,

na manabii wake hawapati tena

maono kutoka kwa Bwana .

10Wazee wa Binti Sayuni

wanaketi chini kimya,

wamenyunyiza mavumbi kwenye vichwa vyao

na kuvaa gunia.

Wanawali wa Yerusalemu

wameinamisha vichwa vyao hadi chini.

11Macho yangu yamedhoofika kwa kulia,

nina maumivu makali ndani,

moyo wangu umemiminwa ardhini

kwa sababu watu wangu wameangamizwa,

kwa sababu watoto na wanyonyao wanazimia

kwenye barabara za mji.

12Wanawaambia mama zao,

“Wapi mkate na divai?”

wazimiapo kama watu waliojeruhiwa

katika barabara za mji,

maisha yao yadhoofikavyo

mikononi mwa mama zao.

13Ninaweza kusema nini kwa ajili yako?

Nikulinganishe na nini,

ee Binti Yerusalemu?

Nitakufananisha na nini,

ili nipate kukufariji,

ee Bikira Binti Sayuni?

Jeraha lako lina kina kama bahari.

Ni nani awezaye kukuponya?

14Maono ya manabii wako

yalikuwa ya uongo na yasiyofaa kitu,

hawakuifunua dhambi yako

ili kukuzuilia kwenda utumwani.

Maneno waliyokupa

yalikuwa ya uongo na ya kupotosha.

15Wote wapitiao njia yako

wanakupigia makofi,

wanakudhihaki na kutikisa vichwa vyao

kwa Binti Yerusalemu:

“Huu ndio ule mji ulioitwa

mkamilifu wa uzuri,

furaha ya dunia yote?”

16Adui zako wote wanapanua

vinywa vyao dhidi yako,

wanadhihaki na kusaga meno yao

na kusema, “Tumemmeza.

Hii ndiyo siku tuliyoingojea,

tumeishi na kuiona.”

17Bwana amefanya lile alilolipanga;

ametimiza neno lake

aliloliamuru siku za kale.

Amekuangusha bila huruma,

amewaacha adui wakusimange,

ametukuza pembe ya adui yako.

18Mioyo ya watu

inamlilia Bwana.

Ee ukuta wa Binti Sayuni,

machozi yako na yatiririke kama mto

usiku na mchana;

usijipe nafuu,

macho yako yasipumzike.

19Inuka, lia usiku,

zamu za usiku zianzapo;

mimina moyo wako kama maji

mbele za Bwana.

Mwinulie yeye mikono yako

kwa ajili ya maisha ya watoto wako,

ambao wanazimia kwa njaa

kwenye kila mwanzo wa barabara.

20“Tazama, Ee Bwana , ufikirie:

Ni nani ambaye umepata kumtendea namna hii?

Je, wanawake wale wazao wao,

watoto waliowalea?

Je, kuhani na nabii auawe

mahali patakatifu pa Bwana?

21“Vijana na wazee hujilaza pamoja

katika mavumbi ya barabarani,

wasichana wangu na wavulana wangu

wameanguka kwa upanga.

Umewaua katika siku ya hasira yako,

umewachinja bila huruma.

22“Kama ulivyoita siku ya karamu,

ndivyo ulivyoagiza mapigo dhidi yangu kila upande.

Katika siku ya hasira ya Bwana

hakuna yeyote aliyekwepa au kupona;

wale niliowatunza na kuwalea,

adui yangu amewaangamiza.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.