Walawi 11

Walawi 11

Vyakula najisi na visivyo najisi

(Kum 14:3‑21)

1Bwana akawaambia Musa na Haruni,

2“Waambieni Waisraeli: ‘Kati ya wanyama wote wanaoishi juu ya nchi, hawa ndio mtakaowala:

3Mwaweza kula mnyama yeyote mwenye kwato zilizogawanyika sehemu mbili na ambaye hucheua.

4“ ‘Kuna wanyama wengine ambao hucheua tu au wenye kwato zilizogawanyika tu, lakini hao kamwe msiwale. Ngamia ingawa hucheua, hana kwato zilizogawanyika; huyo ni najisi kwenu.

5Pelele ingawa hucheua hana kwato zilizogawanyika; huyo ni najisi kwenu.

6Sungura ingawa hucheua hana kwato zilizogawanyika; huyo ni najisi kwenu.

7Naye nguruwe ingawa anazo kwato zilizogawanyika sehemu mbili, hacheui; huyo ni najisi kwenu.

8Kamwe msile nyama yao wala kugusa mizoga yao; wao ni najisi kwenu.

9“ ‘Kuhusu viumbe wote wanaoishi ndani ya maji ya bahari na vijito, mtakula wale wote wenye mapezi na magamba.

10Lakini viumbe wote ndani ya bahari au vijito wasio na mapezi na magamba, wakiwa miongoni mwa makundi au viumbe wote ndani ya maji, hao ni machukizo kwenu.

11Nao watakuwa machukizo kwenu. Msile nyama yao, nayo mizoga yao itakuwa machukizo.

12Chochote kinachoishi ndani ya maji ambacho hakina mapezi na magamba kitakuwa chukizo kwenu.

13“ ‘Wafuatao ndio ndege watakaokuwa machukizo kwenu, hivyo msiwale kwa sababu ni chukizo: tai, furukombe, kipungu,

14mwewe mwekundu, aina zote za mwewe mweusi,

15aina zote za kunguru,

16mbuni, kiruka-njia, dudumizi, kipanga, shakwe, aina zote za kipanga,

17bundi, mnandi, bundi mkubwa,

18mumbi, mwari, nderi,

19korongo, koikoi wa aina yoyote, hudihudi na popo.

20“ ‘Wadudu wote warukao ambao hutembea kwa miguu minne watakuwa chukizo kwenu.

21Lakini kuna viumbe wenye mabawa ambao hutembea kwa miguu minne mtakaowala: wale wenye vifundo katika miguu yao ya kurukaruka juu ya ardhi.

22Miongoni mwa hawa, mtakula nzige wa aina zote, senene, parare au panzi.

23Lakini viumbe wengine wote wenye mabawa na wenye miguu minne ni machukizo kwenu.

Wanyama walio najisi

24“ ‘Mtajinajisi kwa wanyama hawa. Yeyote agusaye mizoga yao atakuwa najisi hadi jioni.

25Yeyote atakayebeba mizoga ya viumbe hawa ni lazima afue nguo zake, naye atakuwa najisi hadi jioni.

26“ ‘Kila mnyama mwenye ukwato ulioachana lakini haukugawanyika kabisa, au yule asiyecheua, huyo ni najisi kwenu; yeyote agusaye mzoga wowote wa hao atakuwa najisi.

27Miongoni mwa wanyama wote wanaotembea kwa miguu minne, wale wanaotembea kwa vitanga vyao ni najisi kwenu; yeyote agusaye mizoga yao atakuwa najisi hadi jioni.

28Yeyote atakayebeba mizoga yao ni lazima afue nguo zake, naye atakuwa najisi hadi jioni. Wanyama hawa ni najisi kwenu.

29“ ‘Kuhusu wanyama watambaao juu ya ardhi, hawa ni najisi kwenu: kicheche, panya, aina yoyote ya mijusi mikubwa,

30guruguru, kenge, mijusi ya ukutani, goromoe na kinyonga.

31Miongoni mwa wanyama wote wanaotambaa juu ya ardhi, hawa ni najisi kwenu. Yeyote agusaye mizoga yao atakuwa najisi hadi jioni.

32Ikiwa mmoja wao atakufa na kuangukia juu ya kitu fulani, chombo hicho, hata kikiwa cha matumizi gani, kitakuwa najisi, kiwe kimetengenezwa kwa mti, nguo, ngozi au gunia. Kiweke ndani ya maji; kitakuwa najisi hadi jioni, kisha kitakuwa safi tena.

33Ikiwa mmoja wa wanyama aliyekufa ataangukia ndani ya chungu, kila kilichomo katika chungu hicho kitakuwa najisi, nawe ni lazima uvunje chungu hicho.

34Chakula chochote ambacho chaweza kuliwa lakini kikawa kimeingia maji kutoka chungu hicho ni najisi, na kitu chochote cha majimaji ambacho chaweza kunyweka kutoka chungu hicho ni najisi.

35Chochote ambacho mzoga utaangukia kitakuwa najisi. Jiko au chungu cha kupikia ni lazima kivunjwe. Ni najisi, nawe ni lazima uvihesabu kuwa najisi.

36Lakini chemchemi au kisima, mahali yanapokusanyika maji, patakuwa safi; lakini yeyote atakayegusa moja ya mizoga hii ni najisi.

37Kama mzoga ukianguka juu ya mbegu zozote ambazo ni za kupanda, zinabaki safi.

38Lakini kama mbegu imetiwa maji na mzoga ukaanguka juu yake, hiyo mbegu ni najisi kwenu.

39“ ‘Kama mnyama ambaye mnaruhusiwa kumla akifa, yeyote atakayeugusa mzoga wake atakuwa najisi hadi jioni.

40Yeyote atakayekula sehemu ya mzoga huo ni lazima afue nguo zake, naye atakuwa najisi hadi jioni. Yeyote atakayebeba mzoga huo ni lazima afue nguo zake, naye atakuwa najisi hadi jioni.

41“ ‘Kila kiumbe kinachotambaa juu ya ardhi ni chukizo; kisiliwe.

42Msile kiumbe chochote kinachotambaa juu ya ardhi, kiwe kinachotambaa kwa tumbo lake, au kinachotambaa kwa miguu minne au kwa miguu mingi; ni chukizo.

43Msijitie unajisi kwa kiumbe chochote kati ya hivi. Msijitie unajisi kwa viumbe hivyo au kutiwa unajisi navyo.

44Mimi ndimi Bwana Mungu wenu; jitakaseni mwe watakatifu, kwa sababu mimi ni mtakatifu. Msijitie unajisi kwa kiumbe chochote kile kiendacho juu ya ardhi.

45Mimi ndimi Bwana niliyewapandisha mtoke Misri ili niwe Mungu wenu. Kwa hiyo kuweni watakatifu kwa sababu Mimi ni mtakatifu.

46“ ‘Haya ndio masharti kuhusu wanyama, ndege, kila kiumbe hai kiendacho ndani ya maji, na kila kiumbe kiendacho juu ya ardhi.

47Ni lazima mpambanue kati ya kilicho najisi na kilicho safi, kati ya viumbe hai vinavyoweza kuliwa na vile visivyoweza kuliwa.’ ”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.