The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Musa,
2“Haya ndio masharti yanayomhusu mtu mgonjwa wakati wa ibada yake ya utakaso, anapoletwa kwa kuhani:
3Kuhani ataenda kumchunguza nje ya kambi. Kama mtu huyo atakuwa amepona ugonjwa wake wa ngozi wa kuambukiza,
4kuhani ataagiza vitu vifuatavyo viletwe kwa ajili ya mtu atakayetakaswa: ndege wawili safi walio hai, mti wa mwerezi, kitani nyekundu, na hisopo.
5Kisha kuhani ataagiza kwamba mmoja wa ndege wale achinjwe kwenye chungu chenye maji safi.
6Kisha kuhani atamchukua ndege aliye hai na kumtumbukiza pamoja na mti wa mwerezi, kitani nyekundu na hisopo ndani ya damu ya yule ndege aliyechinjiwa kwenye maji safi.
7Atamnyunyizia yule mwenye ugonjwa wa kuambukiza maji hayo mara saba, na kumtangaza kuwa safi. Kisha atamwachia yule ndege aliye hai aende zake kwenye mashamba.
8“Huyo mtu atakayetakaswa ni lazima afue nguo zake, anyoe nywele zake zote, na aoge kwa maji; ndipo atakapotakasika. Baada ya hili anaweza kuingia kambini, lakini ni lazima akae nje ya hema lake kwa siku saba.
9Siku ya saba ni lazima anyoe nywele zake zote; yaani anyoe nywele za kichwa, ndevu zake, kope zake na nywele nyingine zote. Ni lazima afue nguo zake, na aoge kwa maji, naye atakuwa safi.
10“Siku ya nane, ni lazima alete kondoo dume wawili na kondoo jike mmoja, wote wa mwaka mmoja na wasio na dosari, pamoja na sehemu tatu za kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta, kwa ajili ya sadaka ya nafaka, na logi moja ya mafuta.[#14:10 Sehemu tatu za kumi ya efa ni sawa na kilo 3.; #14:10 Kipimo cha ujazo, sawa na lita 0.3.]
11Kuhani anayemtangaza kuwa safi atamkabidhi mtu huyo atakayetakaswa pamoja na sadaka zake zote mbele za Bwana katika ingilio la Hema la Kukutania.
12“Kisha kuhani atamchukua mmoja wa wale kondoo dume na kumtoa kuwa sadaka ya hatia, pamoja na ile logi moja ya mafuta; ataviinua mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa.
13Atamchinja huyo kondoo katika mahali patakatifu ambapo sadaka ya dhambi na ile ya kuteketezwa huchinjiwa. Kama ilivyo sadaka ya dhambi, sadaka ya hatia ni ya kuhani; ni takatifu sana.
14Kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya hatia na kuitia kwenye ncha ya sikio la kuume la yule atakayetakaswa, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume.
15Kisha kuhani atachukua sehemu ya ile logi ya mafuta, ayamimine kwenye kiganja cha mkono wake mwenyewe wa kushoto,
16na achovye kidole chake cha shahada cha mkono wake wa kuume kwenye mafuta yaliyo kwenye kiganja chake, na kwa kidole hicho anyunyize mafuta hayo mara saba mbele za Bwana .
17Kuhani atampaka yule anayetakaswa sehemu ya mafuta yaliyobaki kiganjani kwenye ncha ya sikio lake la kuume, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume, mahali palepale alipompaka damu ya sadaka ya kuondoa hatia.
18Kuhani atayapaka mafuta yaliyobaki kwenye kiganja chake juu ya kichwa cha yule anayetakaswa, na kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana .
19“Kisha kuhani atatoa dhabihu ya sadaka ya dhambi na kufanya upatanisho kwa ajili ya yule atakayetakaswa kutoka unajisi wake. Baada ya hayo, kuhani atachinja sadaka ya kuteketezwa
20na kuitoa juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya nafaka ili kumfanyia upatanisho, naye atakuwa safi.
21“Hata hivyo, kama ni maskini na hawezi kupata vitu hivi, lazima achukue mwana-kondoo wa kiume mmoja kuwa sadaka ya hatia ipate kuinuliwa ili kumfanyia upatanisho, pamoja na sehemu ya kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka, logi moja ya mafuta,[#14:21 Sehemu ya kumi ya efa ni sawa na lita 2.]
22na hua wawili au makinda wawili wa njiwa, kile atakachoweza kupata, mmoja kwa sadaka ya dhambi, na mwingine kwa sadaka ya kuteketezwa.
23“Katika siku ya nane, lazima avilete vitu hivyo kwa kuhani, kwa ajili ya kutakaswa kwake kwenye ingilio la Hema la Kukutania mbele za Bwana .
24Kuhani atamchukua mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya hatia, pamoja na ile logi ya mafuta ya kuinuliwa mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa.
25Atamchinja huyo mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya hatia. Kisha ataichukua sehemu ya damu yake na kuipaka kwenye ncha ya sikio la kuume la yule anayetakaswa, na aipake pia kwenye kidole gumba cha mkono wa kuume wa huyo mtu, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume.
26Kuhani atamiminia sehemu ya mafuta kwenye kiganja chake cha mkono wa kushoto,
27na kwa kidole chake cha shahada cha mkono wa kuume, atamnyunyizia yule anayetakaswa yale mafuta yaliyo kwenye kiganja chake mara saba mbele za Bwana .
28Atampaka mafuta yaliyobaki kwenye kiganja chake katika sehemu zote, kama alivyompaka damu ya sadaka ya hatia: yaani kwenye ncha ya sikio la kuume la yule anayetakaswa, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume.
29Kuhani atayapaka mafuta yaliyobaki katika kiganja chake kwenye kichwa cha yule anayetakaswa, na kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana .
30Kisha atatoa dhabihu wale hua ama makinda wa njiwa ambao yule mtu ataweza kuwapata,
31mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa, pamoja na sadaka ya nafaka. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho mbele za Bwana kwa ajili ya yule anayetakaswa.”
32Haya ndio masharti kwa mtu yeyote mwenye ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, na ambaye hana uwezo wa kutoa sadaka za kawaida kwa ajili ya kutakaswa kwake.
33Bwana akawaambia Musa na Haruni,
34“Mtakapoingia katika nchi ya Kanaani ninayowapa kuwa milki yenu, nami nikaweka ukoma unaoenea kwenye nyumba katika nchi ile,[#14:34 ugonjwa wowote wa ngozi wa kuambukiza; pia hutumiwa kwa maambukizi kwenye mawe au matofali ya nyumba]
35ni lazima mwenye nyumba hiyo akamwambie kuhani, ‘Nimeona kitu fulani kinachofanana na ukoma kwenye nyumba yangu.’
36Kuhani ataagiza vitu vyote vitolewe ndani ya nyumba, kabla hajaenda kuchunguza kama ina ukoma huo, ili kitu chochote ndani ya nyumba kisitangazwe kuwa najisi. Baada ya hili, kuhani ataingia ndani na kuikagua hiyo nyumba.
37Atachunguza ukoma huo katika kuta za nyumba hiyo, nazo kama zina rangi ya kijani kibichi au wekundu, na kuna mibonyeo ndani ya ukuta,
38kuhani atatoka na kufunga mlango wa nyumba hiyo kwa siku saba.
39Siku ya saba, kuhani atarudi kuikagua nyumba. Kama ukoma umeenea juu ya kuta,
40ataagiza kwamba mawe yote yaliyoambukizwa yaondolewe na kutupwa katika eneo lililo najisi nje ya mji.
41Kuta zote za ndani ya nyumba hiyo ni lazima zikwanguliwe, na kifusi chake kitupwe mahali najisi nje ya mji.
42Kisha watachukua mawe mengine na kujenga palipobomolewa kwa udongo mpya wa mfinyanzi, na wapake nyumba hiyo chokaa.
43“Ikiwa ukoma huo utatokea tena ndani ya ile nyumba baada ya mawe kuondolewa, na nyumba kukwanguliwa na kupakwa chokaa,
44kuhani ataenda kuikagua, na kama ukoma umeenea ndani ya nyumba, basi ni ukoma unaoharibu; nyumba hiyo ni najisi.
45Ni lazima ibomolewe: mawe yake, mbao na chokaa yote; vyote vikatupwe nje ya mji mahali palipo najisi.
46“Yeyote atakayeingia katika nyumba hiyo ikiwa imefungwa, atakuwa najisi hadi jioni.
47Yeyote atakayelala au kula ndani ya nyumba hiyo ni lazima afue nguo zake.
48“Lakini ikiwa kuhani atakuja kuikagua na kukuta kuwa ukoma haujaenea tena baada ya nyumba kupakwa chokaa, ataitangaza nyumba ile kuwa safi, kwa sababu ukoma umekwisha.
49Ili kuitakasa nyumba hiyo, mwenye nyumba ataleta ndege wawili, mti wa mwerezi, kitani nyekundu na hisopo.
50Atamchinja mmoja wa wale ndege kwenye chungu chenye maji safi.
51Kisha atachukua mti wa mwerezi, hisopo, kitani nyekundu na ndege aliye hai, na kuvitumbukiza ndani ya damu ya ndege aliyechinjwa pamoja na maji safi, na kuinyunyizia nyumba ile mara saba.
52Ataitakasa nyumba kwa damu ya yule ndege, maji safi, ndege aliye hai, mti wa mwerezi, hisopo na uzi mwekundu.
53Kisha atamwachia yule ndege aliye hai huru mashambani nje ya mji. Kwa njia hii atafanya upatanisho kwa ajili ya nyumba ile, nayo itakuwa safi.”
54Haya ndio masharti kuhusu aina yoyote ya ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, kidonda chochote,[#14:54 yaani ukoma ; ni neno lililotumika kueleza magonjwa mbalimbali ya ngozi, ambayo si lazima yawe ni ukoma halisi]
55ukoma katika vazi au ndani ya nyumba,
56kwa uvimbe, upele, au alama nyeupe katika ngozi,
57kupambanua wakati kitu fulani ni safi au najisi.
Haya ndio masharti kuhusu magonjwa ya ngozi ya kuambukiza na ukoma.