Walawi 23

Walawi 23

Sikukuu zilizoamriwa

1Bwana akamwambia Musa,

2“Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Hizi ndizo sikukuu zangu zilizoamriwa, sikukuu zilizoamriwa za Bwana , ambazo mtazitangaza kuwa makusanyiko matakatifu.

3“ ‘Kuna siku sita mnazoweza kufanya kazi, lakini siku ya saba ni Sabato ya kupumzika, siku ya kusanyiko takatifu. Hamtafanya kazi yoyote. Popote mnapoishi, ni Sabato kwa Bwana .

(Hes 28:16‑25)

4“ ‘Hizi ni sikukuu za Bwana zilizoamriwa, makusanyiko matakatifu mtakayoyatangaza kwa nyakati zilizoamriwa:

5Pasaka ya Bwana huanza jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza.

6Siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa kwanza, Sikukuu ya Bwana ya Mikate Isiyotiwa Chachu huanza; kwa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu.

7Katika siku ya kwanza, mtakuwa na kusanyiko takatifu, na msifanye kazi zenu za kawaida.

8Kwa siku saba mtamletea Bwana sadaka ya kuteketezwa kwa moto. Kwenye siku hiyo ya saba mtafanya kusanyiko takatifu, na msifanye kazi zenu za kawaida.’ ”

9Bwana akamwambia Musa,

10“Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Mtakapoingia katika nchi nitakayowapa na kuvuna mazao ya nchi hiyo, leteni kwa kuhani mganda wa nafaka ya kwanza mtakayovuna.

11Naye atauinua huo mganda mbele za Bwana ili ukubaliwe kwa niaba yenu; kuhani ataupunga siku inayofuata Sabato.

12Siku hiyo mtakapoinua huo mganda, lazima mtoe kwa Bwana dhabihu ya kuteketezwa kwa moto ya mwana-kondoo wa mwaka mmoja asiye na dosari,

13pamoja na sadaka yake ya nafaka ya sehemu mbili za kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta, sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa kuteketezwa kwa moto; hii itakuwa sadaka iliyo harufu nzuri ya kupendeza, na sadaka yake ya kinywaji ya robo ya hini ya divai.[#23:13 Sehemu mbili za kumi ya efa ni sawa na kilo mbili.; #23:13 Robo ya hini ni sawa na lita moja.]

14Kamwe msile mkate wowote, au nafaka iliyokaangwa au nafaka mpya, hadi siku ile mtakayomletea Mungu wenu sadaka hii. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo, popote mnapoishi.

(Hes 28:26‑31)

15“ ‘Tangu siku ile iliyofuata Sabato, siku mliyotoa sadaka ya mganda wa kuinuliwa, hesabuni majuma saba kamili.

16Mtahesabu siku hamsini hadi siku inayofuata Sabato ya saba, ndipo mtatoa sadaka ya nafaka mpya kwa Bwana .

17Kutoka popote mnapoishi, mtaleta mikate miwili iliyotengenezwa kwa sehemu mbili za kumi ya efa moja ya unga laini, uliookwa kwa chachu, kuwa sadaka ya kuinuliwa ya malimbuko kwa Bwana .

18Toeni pamoja na hiyo mikate wana-kondoo saba, kila mmoja wa mwaka mmoja asiye na dosari, na fahali mchanga, na kondoo dume wawili. Watakuwa sadaka ya kuteketezwa kwa moto iliyotolewa kwa Bwana , pamoja na sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji, sadaka iliyotolewa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Bwana .

19Kisha toeni dhabihu ya beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na wana-kondoo wawili, kila mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya amani.

20Kuhani atawainua hao wana-kondoo wawili mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa, pamoja na mkate wa malimbuko. Ni sadaka takatifu kwa Bwana kwa ajili ya kuhani.

21Siku hiyo hiyo mtatangaza kusanyiko takatifu, na msifanye kazi zenu za kawaida. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo, popote mtakapoishi.

22“ ‘Mnapovuna mavuno ya ardhi yenu, msivune hadi mpakani mwa shamba lenu, au kukusanya masazo ya mavuno yenu. Hayo utayaacha kwa ajili ya maskini na mgeni. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.’ ”

(Hes 29:1‑6)

23Bwana akamwambia Musa,

24“Waambie Waisraeli: ‘Katika siku ya kwanza ya mwezi wa saba mtakuwa na Sabato ya mapumziko, kusanyiko takatifu la ukumbusho litakaloadhimishwa kwa kupiga tarumbeta.

25Msifanye kazi zenu zozote za kawaida, lakini toeni sadaka kwa Bwana iliyoteketezwa kwa moto.’ ”

(Hes 29:7‑11)

26Bwana akamwambia Musa,

27“Siku ya kumi ya mwezi huu wa saba ni Siku ya Upatanisho. Mtafanya kusanyiko takatifu, mfunge, na kutoa sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Bwana .

28Msifanye kazi siku hiyo, kwa sababu ni Siku ya Upatanisho, ambapo upatanisho unafanyika kwa ajili yenu mbele za Bwana Mungu wenu.

29Mtu ambaye hatafunga siku hiyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.

30Mtu atakayefanya kazi siku hiyo nitamwangamiza kutoka miongoni mwa watu wake.

31Hamtafanya kazi kamwe. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo popote mnapoishi.

32Ni Sabato ya mapumziko kwenu, na lazima mfunge. Tangu jioni ya siku ya tisa ya mwezi hadi jioni inayofuata, mtaishika Sabato yenu.”

(Hes 29:12‑40)

33Bwana akamwambia Musa,

34“Waambie Waisraeli: ‘Katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, Sikukuu ya vibanda itaanza, nayo itaadhimishwa kwa siku saba kwa Bwana .

35Siku ya kwanza ni kusanyiko takatifu, msifanye kazi zenu za kawaida.

36Kwa siku saba toeni sadaka kwa Bwana za kuteketezwa kwa moto. Kwenye siku ya nane fanyeni kusanyiko takatifu, na kutoa sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Bwana . Ni kusanyiko la mwisho, msifanye kazi zenu za kawaida.

37(“ ‘Hizi ni sikukuu za Bwana zilizoamriwa, ambazo mtazitangaza kuwa makusanyiko matakatifu kwa kuleta sadaka kwa Bwana za kuteketeza kwa moto: sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka, dhabihu na sadaka za vinywaji zitahitajika kila siku.

38Sadaka hizi ni nyongeza ya zile mnazozitoa katika Sabato za Bwana , na pia ni nyongeza ya matoleo yenu ya chochote mlichoweka nadhiri, na sadaka zenu zote za hiari mnazozitoa kwa Bwana .)

39“ ‘Basi kuanzia siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, baada ya kuvuna mazao yote ya nchi, mtaadhimisha sikukuu kwa Bwana kwa siku saba; siku ya kwanza ni Sabato ya mapumziko, na pia siku ya nane ni Sabato ya mapumziko.

40Siku ya kwanza mtachukua matunda mazuri ya miti, matawi ya mitende, matawi yenye majani mengi, na matawi ya mirebi, nanyi mtashangilia mbele za Bwana Mungu wenu kwa siku saba.

41Mtaadhimisha siku hii kuwa sikukuu kwa Bwana kwa siku saba kila mwaka. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo; iadhimisheni mwezi wa saba.

42Mtaishi katika vibanda kwa siku saba: Wazawa wote wa Waisraeli wataishi katika vibanda,

43ili wazao wenu wajue kuwa niliwafanya Waisraeli waishi kwenye vibanda nilipowatoa Misri. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.’ ”

44Kwa hiyo Musa akawatangazia Waisraeli sikukuu zilizoamriwa na Bwana .

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.