Mika 5

Mika 5

Mtawala aliyeahidiwa kutoka Bethlehemu

1Panga majeshi yako, ee mji wa majeshi,

kwa kuwa kuzingirwa kumepangwa dhidi yetu.

Watampiga mtawala wa Israeli

shavuni kwa fimbo.

2“Lakini wewe, Bethlehemu Efrata,

ingawa u mdogo miongoni mwa koo za Yuda,

kutoka kwako atatokea kwa ajili yangu

yeye atakayekuwa mtawala katika Israeli,

ambaye asili yake ni kutoka zamani,

kutoka milele.”

3Kwa hiyo Israeli utaachwa

hadi mwanamke aliye na uchungu atakapozaa mwana,

na ndugu zake wengine warudi

kujiunga na Waisraeli.

4Atasimama na kulichunga kundi lake

katika nguvu ya Bwana ,

katika utukufu wa jina la Bwana Mungu wake.

Nao wataishi kwa usalama, kwa kuwa wakati huo

ukuu wake utaenea hadi miisho ya dunia.

5Naye atakuwa amani yao.

Ukombozi na uharibifu

Mwashuru atakapovamia nchi yetu

na kupita katika ngome zetu,

tutawainua wachungaji saba dhidi yake,

hata viongozi wanane wa watu.

6Wataitawala nchi ya Ashuru kwa upanga,

nchi ya Nimrodi kwa upanga.

Atatuokoa kutoka kwa Mwashuru

atakapoivamia nchi yetu

na kuingia katika mipaka yetu.

7Mabaki ya Yakobo yatakuwa

katikati ya mataifa mengi

kama umande kutoka kwa Bwana ,

kama manyunyu juu ya majani,

ambayo hayamngoji mtu

wala kukawia kwa mwanadamu.

8Mabaki ya Yakobo yatakuwa miongoni mwa mataifa,

katikati ya mataifa mengi,

kama simba miongoni mwa wanyama wa msituni,

kama mwana simba miongoni

mwa makundi ya kondoo,

ambaye anaumiza vibaya na kuwararua

kila anapopita katikati yao,

wala hakuna awezaye kuokoa.

9Mkono wako utainuliwa juu kwa ushindi juu ya watesi wako,

nao adui zako wote wataangamizwa.

10“Katika siku ile,” asema Bwana ,

“nitaangamiza farasi wenu kati yenu,

na kubomoa magari yenu ya vita.

11Nitaiangamiza miji ya nchi yenu,

na kuziangusha chini ngome zenu zote.

12Nitaangamiza uchawi wenu,

na hamtapiga tena ramli.

13Nitaangamiza sanamu zenu,

na mawe yenu ya ibada yatoke kati yenu;

hamtasujudia tena

kazi ya mikono yenu.

14Nitangʼoa nguzo za Ashera kati yenu,

na kubomoa miji yenu.

15Nitalipiza kisasi kwa hasira na ghadhabu,

kwa mataifa ambayo hayajanitii.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.