The chat will start when you send the first message.
1Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage na Bethania katika Mlima wa Mizeituni. Yesu akawatuma wawili wa wanafunzi wake,
2akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Na hapo mtakapoingia kijijini, mtampata mwana-punda amefungwa hapo, ambaye hajapandwa na mtu bado. Mfungueni, mkamlete hapa.
3Mtu yeyote akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ mwambieni, ‘Bwana anamhitaji, na atamrudisha hapa baada ya muda mfupi.’ ”
4Wakaenda, wakampata mwana-punda amefungwa kando ya barabara, karibu na mlango wa nyumba.
5Walipokuwa wanamfungua, watu waliokuwa wamesimama karibu wakawauliza, “Kwa nini mnamfungua huyo mwana-punda?”
6Wakawajibu kama vile Yesu alivyokuwa amewaagiza, nao wale watu wakawaruhusu.
7Kisha wakamleta huyo mwana-punda kwa Yesu na kutandika mavazi yao juu yake, naye akampanda.
8Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakatandaza matawi waliyokuwa wamekata mashambani.
9Kisha wale waliokuwa wametangulia mbele na wale waliokuwa wakifuata nyuma wakapaza sauti, wakisema,
“Hosana!”
“Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!”
10“Umebarikiwa ufalme unaokuja wa baba yetu Daudi!”
“Hosana kwake yeye aliye juu!”
11Yesu akaingia Yerusalemu na kwenda Hekaluni. Akaangalia kila kitu kilichokuwamo, lakini kwa kuwa ilishakuwa jioni, akaenda zake Bethania pamoja na wale kumi na wawili.
12Kesho yake walipokuwa wakitoka Bethania, Yesu alikuwa na njaa.
13Akauona mtini kwa mbali, naye akaenda ili aone kama ulikuwa na matunda. Alipoufikia, akakuta una majani tu, kwa kuwa hayakuwa majira ya tini.
14Akauambia ule mti, “Tangu leo mtu yeyote asile kamwe matunda kutoka kwako.” Wanafunzi wake walimsikia akisema hayo.
15Walipofika Yerusalemu, Yesu akaingia katika eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakinunua na kuuza humo. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa,
16wala hakumruhusu mtu yeyote kuchukua bidhaa kupitia ukumbi wa Hekalu.
17Naye alipokuwa akiwafundisha, akasema, “Je, haikuandikwa kuwa:
“ ‘Nyumba yangu itaitwa
nyumba ya sala kwa mataifa yote’?
Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyangʼanyi.’”
18Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria wakapata habari hizi, nao wakaanza kutafuta njia ya kumuua, kwa kuwa walikuwa wakimwogopa, kwa sababu umati wote walishangazwa na mafundisho yake.
19Ilipofika jioni, Yesu na wanafunzi wake wakatoka nje ya mji.
20Kesho yake asubuhi walipokuwa wakipita, wakauona ule mtini umenyauka kutoka juu hadi kwenye mizizi yake.
21Petro akakumbuka na kumwambia Yesu, “Rabi, tazama! Ule mtini ulioulaani umenyauka!”
22Yesu akawajibu, “Mwaminini Mungu.
23Amin, nawaambia, mtu yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ngʼoka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, atatimiziwa.
24Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote mtakayoyaomba mkisali, aminini kwamba mmeyapokea, nayo yatakuwa yenu.
25Nanyi kila msimamapo kusali, sameheni mkiwa na neno na mtu, ili naye Baba yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu. [
26Lakini kama ninyi msiposamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]”[#11:26 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.]
27Wakafika tena Yerusalemu, na Yesu alipokuwa akitembea Hekaluni, viongozi wa makuhani, walimu wa sheria pamoja na wazee wa watu wakamjia.
28Wakamuuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Na ni nani aliyekupa mamlaka ya kufanya hayo?”
29Yesu akawajibu, “Nitawauliza swali moja. Nijibuni, nami nitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya.
30Je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni au kwa wanadamu? Niambieni!”
31Wakahojiana wao kwa wao na kusema, “Tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona hamkumwamini?’
32Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu’ ” (waliwaogopa watu, kwa sababu kila mtu aliamini kwamba Yohana alikuwa nabii wa kweli);
33kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Hatujui.”
Naye Yesu akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.”