Marko 2

Marko 2

Yesu amponya mtu aliyepooza

(Mt 9:1‑8; Lk 5:17‑26)

1Baada ya siku kadhaa Yesu alirudi Kapernaumu, watu wakasikia kwamba yupo nyumbani.

2Watu wengi wakakusanyika, kiasi kwamba hapakubaki nafasi yoyote hata mlangoni! Naye akawahubiria Neno.

3Ndipo baadhi ya watu wakaja wakamletea Yesu mtu aliyepooza, akiwa amebebwa na watu wanne.

4Kwa kuwa hawakuweza kumfikisha kwa Yesu kwa sababu ya umati wa watu, walitoboa tundu kwenye paa juu ya mahali Yesu alikuwa, wakamshusha mtu aliyepooza akiwa amelalia mkeka wake.

5Yesu alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, dhambi zako zimesamehewa.”

6Basi baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa wameketi pale wakawaza mioyoni mwao,

7“Kwa nini mtu huyu anasema hivi? Huyu anakufuru! Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”

8Mara moja Yesu akatambua rohoni mwake kile walichokuwa wanawaza mioyoni mwao, naye akawaambia, “Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu?

9Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kumwambia huyu aliyepooza, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uchukue mkeka wako, uende’?

10Lakini ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani ya kusamehe dhambi”: Yesu akamwambia yule aliyepooza,

11“Nakuambia, inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.”

12Yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama, akachukua mkeka wake, akatembea machoni pao wote! Jambo hili likawashangaza wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, “Hatujapata kuona jambo kama hili kamwe!”

Yesu amwita Lawi

(Mt 9:9‑13; Lk 5:27‑32)

13Yesu akaenda tena kandokando ya Bahari ya Galilaya. Umati mkubwa wa watu wakamfuata, naye akaanza kuwafundisha.

14Alipokuwa akitembea, akamwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi forodhani mahali pa kutoza ushuru. Yesu akamwambia, “Nifuate.” Naye Lawi akaondoka, akamfuata Yesu.

15Yesu alipokuwa ameketi akila chakula nyumbani mwa Lawi, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuwa wakila pamoja naye na wanafunzi wake, kwa maana ni watu wengi waliokuwa wakimfuata.

16Walimu wa sheria waliokuwa Mafarisayo walipomwona akila pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi, wakawauliza wanafunzi wake: “Mbona Yesu anakula na watoza ushuru na wenye dhambi?”

17Yesu aliposikia haya akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”

Yesu aulizwa kuhusu kufunga

(Mt 9:14‑17; Lk 5:33‑39)

18Basi wanafunzi wa Yohana pamoja na Mafarisayo walikuwa wakifunga. Watu wakamjia Yesu na kumuuliza, “Mbona wanafunzi wa Yohana na wa Mafarisayo hufunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?”

19Yesu akawajibu, “Wageni wa bwana arusi wawezaje kufunga wakati angali pamoja nao? Wakati bwana arusi bado yuko pamoja nao, hawawezi kufunga.

20Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Siku hiyo ndipo watakapofunga.

21“Hakuna mtu ashoneaye kiraka cha nguo mpya kwenye nguo iliyochakaa. Akifanya hivyo, kile kiraka kipya kitachanika kutoka ile nguo iliyochakaa, nayo itachanika zaidi.

22Wala hakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, ile divai mpya itavipasua hivyo viriba, nayo hiyo divai itamwagika na viriba vitaharibika. Lakini divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya.”

Yesu ni Bwana wa Sabato

(Mt 12:1‑8; Lk 6:1‑5)

23Siku moja ya Sabato, Yesu pamoja na wanafunzi wake walikuwa wakipita katikati ya mashamba ya nafaka. Walipokuwa wakitembea, wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke.

24Mafarisayo wakamwambia, “Tazama, mbona wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato?”

25Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma alivyofanya Daudi yeye na wenzake walipokuwa na njaa, wakahitaji chakula?

26Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu, Abiathari alipokuwa kuhani mkuu, akaila ile mikate iliyowekwa wakfu, ambayo ni halali kuliwa na makuhani tu. Naye pia akawapa wenzake.”

27Kisha Yesu akawaambia, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, lakini si mwanadamu kwa ajili ya Sabato.

28Hivyo, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.