Nehemia 3

Nehemia 3

Wajenzi wa ukuta

1Eliashibu kuhani mkuu na makuhani wenzake walienda kufanya kazi na kulijenga upya Lango la Kondoo. Waliliweka wakfu na kuweka milango mahali pake, wakajenga hadi kufikia Mnara wa Mia, ambao waliuweka wakfu hadi Mnara wa Hananeli.

2Wanaume wa Yeriko wakajenga sehemu zilizopakana nao, naye Zakuri mwana wa Imri akajenga karibu nao.

3Lango la Samaki lilijengwa upya na wana wa Hasenaa. Waliweka boriti zake, na wakaweka milango yake na makomeo na nondo.

4Meremothi mwana wa Uria, mwana wa Hakosi, alikarabati sehemu iliyofuatia. Baada yake Meshulamu mwana wa Berekia, mwana wa Meshezabeli, alifanya ukarabati na aliyemfuatia ni Sadoki mwana wa Baana.

5Sehemu iliyofuatia ilikarabatiwa na watu kutoka Tekoa, lakini wakuu wao walikataa kufanya kazi chini ya wasimamizi wao.

6Lango la Yeshana lilikarabatiwa na Yoyada mwana wa Pasea, na Meshulamu mwana wa Besodeya. Waliweka boriti zake, na wakaweka milango, makomeo na nondo.

7Karibu nao ukarabati ulifanywa na watu kutoka Gibeoni na Mispa, yaani Melati Mgibeoni, na Yadoni Mmeronothi, sehemu hizi zikiwa chini ya mamlaka ya mtawala wa Ngʼambo ya Frati.

8Uzieli mwana wa Harhaya, mmoja wa masonara, alikarabati sehemu iliyofuatia, naye Hanania mmoja wa watengenezaji marashi akakarabati sehemu iliyofuatia. Walitengeneza Yerusalemu kufikia Ukuta Mpana.

9Refaya mwana wa Huri, mtawala wa nusu ya wilaya ya Yerusalemu, alikarabati sehemu iliyofuatia.

10Kupakana na sehemu hii, Yedaya mwana wa Harumafu alikarabati sehemu iliyokuwa mkabala na nyumba yake, naye Hatushi mwana wa Hashabnea akakarabati sehemu iliyofuatia.

11Malkiya mwana wa Harimu, na Hashubu mwana wa Pahath-Moabu walikarabati sehemu nyingine pamoja na Mnara wa Matanuru.

12Shalumu mwana wa Haloheshi, mtawala wa nusu ya wilaya ya Yerusalemu, alikarabati sehemu iliyofuatia akisaidiwa na binti zake.

13Lango la Bondeni lilikarabatiwa na Hanuni na wakazi wa Zanoa. Walilijenga upya, na kuweka milango yake na makomeo na nondo mahali pake. Pia walikarabati ukuta wenye urefu wa dhiraa elfu moja hadi Lango la Samadi.[#3:13 ni kama mita 450]

14Lango la Samadi lilikarabatiwa na Malkiya mwana wa Rekabu, mtawala wa wilaya ya Beth-Hakeremu. Alilijenga upya, na kuweka milango yake, na makomeo na nondo.

15Lango la Chemchemi lilikarabatiwa na Shalumu mwana wa Kolhoze, mtawala wa wilaya ya Mispa. Alilijenga upya, akaliezeka na kuweka milango yake, na makomeo na nondo mahali pake. Pia alikarabati ukuta wa Bwawa la Siloamu karibu na Bustani ya Mfalme, hadi kwenye ngazi zinazoshuka kutoka Mji wa Daudi.

16Baada yake, Nehemia mwana wa Azbuki, mtawala wa nusu ya wilaya ya Beth-Suri, alikarabati kufikia mkabala na makaburi ya Daudi, hadi kwenye bwawa lililotengenezwa, na kufikia Nyumba ya Mashujaa.

17Baada yake, ukarabati ulifanywa na Walawi chini ya uongozi wa Rehumu mwana wa Bani. Aliyefuatia ni Hashabia, mtawala wa nusu ya wilaya ya Keila, aliyekarabati sehemu ya wilaya yake.

18Baada yake, ukarabati ulifanywa na ndugu zao chini ya usimamizi wa Binui mwana wa Henadadi, mtawala wa nusu hiyo ingine ya wilaya ya Keila.

19Baada yao, Ezeri mwana wa Yeshua, mtawala wa Mispa, alikarabati sehemu nyingine, kuanzia ile sehemu inayotazamana na mwinuko wa kuelekea kwenye ghala la kuhifadhia silaha, hadi kwenye pembe ya ukuta.

20Baada yake, Baruku mwana wa Zakai alikarabati kwa bidii sehemu nyingine kuanzia ile pembe, hadi kwenye lango la nyumba ya Eliashibu kuhani mkuu.

21Kupakana naye, Meremothi mwana wa Uria, mwana wa Hakosi, alikarabati sehemu nyingine, kuanzia penye lango la nyumba ya Eliashibu hadi mwisho wake.

22Baada yake, ukarabati ulifanywa na makuhani waliotoka eneo lililouzunguka mji.

23Baada yao Benyamini na Hashubu walikarabati mbele ya nyumba zao, na baada yao Azaria mwana wa Maaseya, mwana wa Anania alifanya ukarabati kando ya nyumba yake.

24Baada yake, Binui mwana wa Henadadi alikarabati sehemu nyingine, kuanzia kwenye nyumba ya Azaria hadi kwenye pembe ya ukuta.

25Naye Palali, mwana wa Uzai alijenga sehemu iliyokuwa mkabala na pembe ya ukuta, hadi kwenye mnara wa juu ambao unachomoka kuanzia kwenye jumba la kifalme, kando ya ua wa walinzi. Baada yake, Pedaya mwana wa Paroshi,

26na watumishi wa Hekalu walioishi juu ya kilima cha Ofeli walikarabati hadi kufikia mkabala na Lango la Maji, kuelekea mashariki na ule mnara uliochomoza.

27Baada yao, watu wa Tekoa walikarabati sehemu nyingine, kuanzia mnara mkubwa unaochomoza hadi ukuta wa Ofeli.

28Makuhani walifanya ukarabati juu ya Lango la Farasi, kila mmoja mbele ya nyumba yake.

29Baada yao, Sadoki mwana wa Imeri alifanya ukarabati mkabala na nyumba yake. Baada yake, Shemaya mwana wa Shekania, mlinzi wa Lango la Mashariki, alifanya ukarabati.

30Baada yake, Hanania mwana wa Shelemia, na Hanuni mwana wa sita wa Salafu walikarabati sehemu nyingine. Baada yao, Meshulamu mwana wa Berekia alikarabati sehemu iliyokuwa mkabala na nyumba zake za kuishi.

31Baada yake Malkiya, mmoja wa masonara, alifanya ukarabati hadi kwenye nyumba za watumishi wa Hekalu na wafanyabiashara, mkabala na Lango la Ukaguzi, hadi kufikia chumba kilicho juu ya pembe.[#3:31 yaani Wanethini.]

32Masonara na wafanyabiashara walifanya ukarabati kutoka chumba kilichoko juu ya pembe hadi Lango la Kondoo.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.