Hesabu 16

Hesabu 16

Kora, Dathani na Abiramu

1Kora mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, pamoja na baadhi ya Wareubeni, yaani Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni mwana wa Pelethi, wakachukua baadhi ya watu,

2wakainuka dhidi ya Musa. Pamoja nao walikuwa wanaume Waisraeli mia mbili na hamsini, watu waliojulikana, viongozi wa jumuiya waliokuwa wameteuliwa kuwa wakuu wa kusanyiko.

3Wakaja kama kikundi kuwapinga Musa na Haruni, wakawaambia, “Ninyi mmejitukuza sana! Kusanyiko hili wote ni watakatifu, kila mmoja wao, naye Bwana yu pamoja nao. Kwa nini basi mmejitukuza wenyewe juu ya kusanyiko la Bwana ?”

4Musa aliposikia jambo hili, akaanguka kifudifudi.

5Kisha akamwambia Kora na wafuasi wake wote: “Asubuhi Bwana ataonesha ni nani aliye wake na ni nani aliye mtakatifu, tena atamtaka mtu huyo aje kwake. Mtu yule ambaye atamchagua atamfanya kuja karibu naye.

6Wewe Kora na wafuasi wako wote mtafanya hivi: Chukueni vyetezo,

7kesho wekeni moto na uvumba kwenye hivyo vyetezo mbele za Bwana . Mtu ambaye Bwana atamchagua atakuwa ndiye mtakatifu. Ninyi Walawi mmejitukuza sana!”

8Pia Musa akamwambia Kora, “Enyi Walawi! Sasa nisikilizeni.

9Haiwatoshi ninyi kwamba Mungu wa Israeli amewateua ninyi kutoka kusanyiko lote la Israeli, na kuwaleta karibu naye mpate kufanya kazi kwenye Maskani ya Bwana , na kusimama mbele ya kusanyiko ili kuwahudumia?

10Amekuleta wewe na ndugu zako Walawi mwe karibu naye; lakini sasa unajaribu kuchukua ukuhani pia.

11Wewe na wafuasi wako wote mmekusanyika pamoja kinyume cha Bwana . Haruni ni nani kwamba ninyi mnungʼunike dhidi yake?”

12Kisha Musa akawaita Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu. Lakini wao wakasema, “Sisi hatuji!

13Haitoshi tu kwamba wewe umetuleta kutoka nchi inayotiririka maziwa na asali ili kutuua sisi jangwani? Nawe sasa pia unataka kuwa mkuu juu yetu?

14Zaidi ya hayo, hujatuingiza katika nchi inayotiririka maziwa na asali, wala hujatupatia urithi wa mashamba na mashamba ya mizabibu. Je, utayangʼoa macho ya watu hawa? Hapana, sisi hatuji!”

15Ndipo Musa akakasirika sana na kumwambia Bwana , “Usiikubali sadaka yao. Mimi sikuchukua chochote, hata punda kutoka kwao, wala sijamkosea hata mmoja wao.”

16Musa akamwambia Kora, “Wewe na wafuasi wako wote kesho mtatokea mbele za Bwana : wewe na hao wenzako, pamoja na Haruni.

17Kila mtu atachukua chetezo chake na kuweka uvumba ndani, vyetezo mia mbili na hamsini kwa jumla, na kukileta mbele za Bwana . Wewe na Haruni mtaleta vyetezo vyenu pia.”

18Kwa hiyo kila mtu akachukua chetezo chake, akaweka moto na uvumba ndani, na kusimama pamoja na Musa na Haruni kwenye mlango wa Hema la Kukutania.

19Kora alipokuwa amekusanya wafuasi wake wote kuwapinga Musa na Haruni kwenye mlango wa Hema la Kukutania, utukufu wa Bwana ukatokea kwa kusanyiko lote.

20Bwana akamwambia Musa na Haruni,

21“Jitengeni na kusanyiko hili ili nipate kuwaangamiza mara moja.”

22Lakini Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi na kulia kwa sauti, wakasema, “Ee Mungu, Mungu wa roho za wanadamu wote, utakuwa na hasira na kusanyiko lote wakati ni mtu mmoja tu ametenda dhambi?”

23Ndipo Bwana akamwambia Musa,

24“Waambie kusanyiko, ‘Ondokeni hapo karibu na mahema ya Kora, Dathani na Abiramu.’ ”

25Musa akainuka na kuwaendea Dathani na Abiramu, nao wazee wa Israeli wakafuatana naye.

26Musa akawaonya kusanyiko, “Sogeeni nyuma mbali na mahema ya hawa watu waovu! Msiguse kitu chochote kilicho mali yao, la sivyo mtafagiliwa mbali kwa sababu ya dhambi zao zote.”

27Hivyo wakaondoka karibu na mahema ya Kora, Dathani na Abiramu. Dathani na Abiramu walikuwa wametoka nje, nao walikuwa wamesimama pamoja na wake zao, watoto wao na wale wanyonyao kwenye mlango wa mahema yao.

28Ndipo Musa akasema, “Hivi ndivyo mtakavyojua kuwa Bwana amenituma kufanya mambo haya, na kwamba halikuwa wazo langu.

29Ikiwa watu hawa watakufa kifo cha kawaida na kupatwa na yale ya kawaida yanayowapata wanadamu, basi Bwana hakunituma mimi.

30Lakini ikiwa Bwana ataleta jambo jipya kabisa, ardhi ikifunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na kila kitu kilicho mali yao, nao washuke chini kaburini wakiwa hai, ndipo mtafahamu kuwa watu hawa wamemdharau Bwana .”[#16:30 Kaburini maana yake ni Kuzimu ; kwa Kiebrania ni Sheol.]

31Mara Musa alipomaliza kusema haya yote, ardhi iliyokuwa chini yao ikapasuka,

32nchi ikafunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na jamaa zao, na watu wote wa Kora na mali yao yote.

33Wakashuka chini kaburini wakiwa hai, pamoja na kila kitu walichokuwa nacho; nchi ikajifunika juu yao, nao wakaangamia wakatoweka kutoka kwa kusanyiko.

34Kutoka kilio chao, Waisraeli wote waliowazunguka walikimbia, wakipaza sauti, “Nchi inatumeza na sisi pia!”

35Moto ukaja kutoka kwa Bwana , ukawateketeza wale watu mia mbili na hamsini waliokuwa wakifukiza uvumba.

36Bwana akamwambia Musa,

37“Mwambie Eleazari mwana wa kuhani Haruni, atoe vyetezo kwenye mabaki ya moto na kutawanya makaa mbali kiasi, kwa maana vyetezo ni vitakatifu:

38vyetezo vya watu waliofanya dhambi iliyowagharimu maisha yao. Fua vyetezo hivyo kuwa bamba ili kufunika madhabahu, kwa maana vimeletwa mbele za Bwana na vimekuwa vitakatifu. Navyo viwe ishara kwa Waisraeli.”

39Hivyo kuhani Eleazari akavikusanya vile vyetezo vya shaba vilivyoletwa na wale waliokuwa wameteketezwa kwa moto, naye akavifua kufunika madhabahu,

40kama vile Bwana alivyomwelekeza kupitia Musa. Hili lilikuwa kuwakumbusha Waisraeli kwamba hakuna mtu hata mmoja, isipokuwa mzao wa Haruni, awezaye kuja kufukiza uvumba mbele za Bwana , la sivyo, angekuwa kama Kora na wafuasi wake.

41Siku iliyofuata jumuiya yote ya Waisraeli wakanungʼunika dhidi ya Musa na Haruni, wakisema, “Mmewaua watu wa Bwana .”

42Lakini kusanyiko walipokusanyika kupingana na Musa na Haruni, nao wakageuka kuelekea Hema la Kukutania, ghafula wingu likafunika Hema, nao utukufu wa Bwana ukatokea.

43Ndipo Musa na Haruni wakaenda mbele ya Hema la Kukutania,

44naye Bwana akamwambia Musa,

45“Jitenge mbali na kusanyiko hili ili niweze kuwaangamiza mara moja.” Wakaanguka kifudifudi.

46Kisha Musa akamwambia Haruni, “Chukua chetezo chako na uweke uvumba ndani, pamoja na moto kutoka madhabahuni, nawe uende haraka kwenye kusanyiko ili kufanya upatanisho kwa ajili yao. Ghadhabu imekuja kutoka kwa Bwana , na tauni imeanza.”

47Hivyo Haruni akafanya kama Musa alivyosema, akakimbilia katikati ya kusanyiko. Tauni ilikuwa tayari imeanza miongoni mwa watu, lakini Haruni akafukiza uvumba na kufanya upatanisho kwa ajili yao.

48Haruni akasimama kati ya waliokuwa hai na waliokufa, nayo tauni ikakoma.

49Lakini walikufa watu elfu kumi na nne na mia saba kutokana na tauni hiyo, licha ya wale waliokuwa wamekufa kwa sababu ya Kora.

50Ndipo Haruni akamrudia Musa kwenye mlango wa Hema la Kukutania, kwa maana tauni ilikuwa imekoma.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.