The chat will start when you send the first message.
1Mvinyo ni mdhihaki na kileo ni mgomvi;
yeyote apotoshwaye navyo hana hekima.
2Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba;
yeye amkasirishaye hupoteza uhai wake.
3Ni kwa heshima ya mtu kujitenga ugomvi,
bali kila mpumbavu ni mwepesi kugombana.
4Mvivu halimi kwa majira;
kwa hiyo wakati wa mavuno hutazama
lakini hapati chochote.
5Makusudi ya moyo wa mwanadamu ni maji yenye kina,
lakini mtu mwenye ufahamu huyachota.
6Watu wengi hujidai kuwa na upendo usiokoma,
bali mtu mwaminifu ni nani awezaye kumpata?
7Mtu mwenye haki huishi maisha yasiyo na lawama,
wamebarikiwa watoto wake baada yake.
8Mfalme anapoketi kwenye kiti chake cha ufalme kuhukumu,
hupepeta ubaya wote kwa macho yake.
9Ni nani awezaye kusema, “Nimeuweka moyo wangu safi;
mimi ni safi na sina dhambi?”
10Mawe ya kupimia yaliyo tofauti na vipimo tofauti,
Bwana huchukia vyote viwili.
11Hata mtoto hujulikana kwa matendo yake,
kama tabia yake ni safi na adili.
12Masikio yasikiayo na macho yaonayo:
Bwana ndiye alivifanya vyote viwili.
13Usiupende usingizi la sivyo utakuwa maskini,
uwe macho nawe utakuwa na chakula cha akiba.
14“Haifai, haifai!” asema mnunuzi,
kisha huondoka akijisifia ununuzi wake.
15Kuna dhahabu, na marijani kwa wingi,
lakini midomo inayonena maarifa
ni kito cha thamani.
16Chukua vazi la yule awekaye dhamana
kwa ajili ya mgeni;
lishikilie liwe dhamana
kwa ajili ya mgeni.
17Chakula kilichopatikana kwa hila ni kitamu kwa mwanadamu,
bali huishia na kinywa kilichojaa changarawe.
18Fanya mipango kwa kutafuta mashauri,
ukipigana vita, tafuta maelekezo.
19Maneno ya kusengenya husababisha kutokuaminika,
kwa hiyo mwepuke mtu anayezungumza kupita kiasi.
20Ikiwa mtu atamlaani baba yake au mama yake,
taa yake itazimwa katika giza nene.
21Urithi upatikanao haraka mwanzoni,
hautabarikiwa mwishoni.
22Usiseme, “Nitakulipiza kwa ajili ya kosa hili!”
Mngojee Bwana , naye atakuokoa.
23Bwana anachukia sana mawe ya kupimia ya udanganyifu,
nazo mizani zisizo halali hazimpendezi.
24Hatua za mtu huongozwa na Bwana .
Anawezaje basi mtu yeyote kuelewa njia yake mwenyewe?
25Ni mtego kwa mtu kuweka wakfu kitu kwa haraka
na baada ya kitambo kidogo kufikiria tena nadhiri zake.
26Mfalme mwenye hekima hupepeta waovu,
hulipitisha gurudumu la kupuria juu yao.
27Taa ya Bwana huchunguza roho ya mwanadamu,
huchunguza utu wake wa ndani.
28Upendo na uaminifu humweka mfalme salama;
kiti chake cha ufalme huwa salama kwa upendo.
29Utukufu wa vijana ni nguvu zao,
mvi ni fahari ya uzee.
30Mapigo na majeraha huusafisha ubaya,
nayo michapo hutakasa utu wa ndani.