Zaburi 107

Zaburi 107

Kitabu cha Tano

Zaburi 107

Kumsifu Mwenyezi Mungu kwa wema wake

1Mshukuruni Mwenyezi Mungu, kwa kuwa yeye ni mwema,

fadhili zake zadumu milele.

2Waliokombolewa wa Mwenyezi Mungu na waseme hivi,

wale aliowaokoa kutoka mkono wa adui,

3wale aliowakusanya kutoka nchi mbalimbali,

kutoka mashariki na magharibi,

kutoka kaskazini na kusini.

4Baadhi yao walitangatanga jangwani,

hawakuona njia ya kuwafikisha mji ambao wangeweza kuishi.

5Walikuwa na njaa na kiu,

nafsi zao zikadhoofika.

6Ndipo walipomlilia Mwenyezi Mungu katika shida yao,

naye akawaokoa kutoka taabu yao.

7Akawaongoza kwa njia iliyo sawa

hadi mji ambao wangeweza kuishi.

8Basi na wamshukuru Mwenyezi Mungu kwa upendo wake usiokoma,

na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu,

9kwa maana yeye humtosheleza mwenye kiu,

na kumshibisha mwenye njaa kwa vitu vyema.

10Wengine walikaa gizani na katika huzuni kuu,

wafungwa wakiteseka katika minyororo,

11kwa sababu waliasi dhidi ya maneno ya Mungu,

na kudharau ushauri wa Aliye Juu Sana.

12Aliwatumikisha kwa kazi ngumu;

walijikwaa na hapakuwa na mtu wa kuwasaidia.

13Ndipo walipomlilia Mwenyezi Mungu katika shida yao,

naye akawaokoa kutoka taabu yao.

14Akawatoa katika giza na huzuni kuu

na akavunja minyororo yao.

15Basi na wamshukuru Mwenyezi Mungu kwa upendo wake usiokoma,

na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu,

16kwa kuwa yeye huvunja malango ya shaba

na kukata mapingo ya chuma.

17Wengine wakawa wapumbavu kutokana na uasi wao,

wakapata mateso kwa sababu ya uovu wao.

18Wakachukia kabisa vyakula vyote,

wakakaribia malango ya mauti.

19Ndipo walipomlilia Mwenyezi Mungu katika shida yao,

naye akawaokoa kutoka taabu yao.

20Akalituma neno lake na kuwaponya,

akawaokoa kutoka maangamizi yao.

21Basi na wamshukuru Mwenyezi Mungu kwa upendo wake usiokoma,

na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu.

22Na watoe dhabihu za kushukuru,

na wasimulie matendo yake kwa nyimbo za furaha.

23Wengine walisafiri baharini kwa meli,

walikuwa wafanyabiashara kwenye maji makuu.

24Waliziona kazi za Mwenyezi Mungu,

matendo yake ya ajabu kilindini.

25Kwa maana alisema na kuamsha tufani

iliyoinua mawimbi juu.

26Yakainuka juu mbinguni, yakashuka chini hadi vilindini;

katika hatari hii ujasiri wao uliyeyuka.

27Walipepesuka na kuyumbayumba kama walevi,

ujanja wao ukafikia ukomo.

28Ndipo walipomlilia Mwenyezi Mungu katika shida yao,

naye akawatoa kwenye taabu yao.

29Akatuliza dhoruba kwa mnong’ono,

mawimbi ya bahari yakatulia.

30Walifurahi ilipokuwa shwari,

naye akawaongoza hadi bandari waliyoitamani.

31Basi na wamshukuru Mwenyezi Mungu kwa upendo wake usiokoma,

na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu.

32Na wamtukuze yeye katika kusanyiko la watu,

na wamsifu katika baraza la wazee.

33Yeye aligeuza mito kuwa jangwa,

chemchemi za maji zinazotiririka kuwa ardhi yenye kiu,

34nchi inayozaa ikawa ya chumvi isiyofaa,

kwa sababu ya uovu wa wale walioishi humo.

35Aligeuza jangwa likawa madimbwi ya maji,

nayo ardhi kame kuwa chemchemi za maji zinazotiririka;

36aliwaleta wenye njaa wakaishi humo,

nao wakajenga mji wangeweza kuishi.

37Walilima mashamba na kupanda mizabibu,

nayo ikazaa matunda mengi,

38Mungu aliwabariki, hesabu yao ikaongezeka sana,

wala hakuruhusu mifugo yao kupungua.

39Kisha hesabu yao ilipungua, na walinyenyekeshwa

kwa kuonewa, maafa na huzuni.

40Yeye ambaye huwamwagia dharau wakuu,

aliwafanya watangetange nyikani isiyo na njia.

41Lakini yeye aliwainua wahitaji katika taabu zao,

na kuongeza jamaa zao kama makundi ya kondoo.

42Wanyofu wataona na kufurahi,

lakini waovu wote watafunga vinywa vyao.

43Yeyote aliye na hekima, ayasikie mambo haya,

na atafakari upendo mkuu wa Mwenyezi Mungu.

Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™ Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Scriptures™ Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.