The chat will start when you send the first message.
1Nayainua macho yangu natazama milima:
msaada wangu utatoka wapi?
2Msaada wangu hutoka kwa Mwenyezi Mungu,
Muumba wa mbingu na dunia.
3Hatauacha mguu wako uteleze,
yeye akulindaye hatasinzia,
4hakika, yeye alindaye Israeli
hatasinzia wala hatalala usingizi.
5Mwenyezi Mungu anakulinda,
Mwenyezi Mungu ni uvuli wako mkono wako wa kuume,
6jua halitakudhuru mchana,
wala mwezi wakati wa usiku.
7Mwenyezi Mungu atakukinga na madhara yote,
atayalinda maisha yako,
8Mwenyezi Mungu atakulinda unapoingia na unapotoka,
tangu sasa na hata milele.