Zaburi 141

Zaburi 141

Zaburi 141

Maombi ya kuhifadhiwa dhidi ya uovu

1Ee Mwenyezi Mungu, ninakuita, njoo kwangu hima.

Sikia sauti yangu ninapokuita.

2Maombi yangu na yafike mbele zako kama uvumba;

kuinua mikono yangu juu na kuwe kama dhabihu ya jioni.

3Ee Mwenyezi Mungu, weka mlinzi kinywani mwangu,

weka ulinzi mlangoni mwa midomo yangu.

4Usiuache moyo wangu uvutwe katika jambo baya,

nisije nikashiriki katika matendo maovu

pamoja na watu watendao mabaya,

wala nisije nikala vyakula vyao vya anasa.

5Mtu mwenye haki na anipige: ni jambo la huruma;

na anikemee: ni mafuta kichwani mwangu.

Kichwa changu hakitalikataa.

Hata hivyo, maombi yangu daima

ni kinyume cha watenda maovu.

6Watawala wao watatupwa chini

kutoka majabali,

waovu watajifunza kwamba maneno yangu

yalikuwa kweli.

7Watasema, “Kama mtu anavyolima na kuvunja ardhi,

ndivyo mifupa yetu imetawanywa kwenye mlango wa kaburi.”

8Lakini nimekaza macho yangu kwako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi,

ndani yako nimekimbilia, usiniache nife.

9Niepushe na mitego waliyonitegea,

kutokana na mitego iliyotegwa na watenda maovu.

10Waovu na waanguke kwenye nyavu zao wenyewe,

wakati mimi ninapita salama.

Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™ Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Scriptures™ Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.