The chat will start when you send the first message.
1Bwana anatawala, nchi na ifurahi,
visiwa vyote vishangilie.
2Mawingu na giza nene vinamzunguka,
haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake cha enzi.
3Moto hutangulia mbele zake
na huteketeza adui zake pande zote.
4Umeme wake wa radi humulika dunia,
nchi huona na kutetemeka.
5Milima huyeyuka kama nta mbele za Bwana ,
mbele za Bwana wa dunia yote.
6Mbingu zinatangaza haki yake,
na mataifa yote huona utukufu wake.
7Wote waabuduo sanamu waaibishwa,
wale wajisifiao sanamu:
mwabuduni yeye, enyi miungu yote!
8Sayuni husikia na kushangilia,
vijiji vya Yuda vinafurahi
kwa sababu ya hukumu zako, Ee Bwana .
9Kwa kuwa wewe, Ee Bwana , ndiwe Uliye Juu Sana kuliko dunia yote;
umetukuka sana juu ya miungu yote.
10Wale wanaompenda Bwana na wauchukie uovu,
kwa maana yeye hulinda maisha ya waaminifu wake
na kuwaokoa kutoka mkononi mwa mwovu.
11Nuru huangaza wenye haki
na furaha kwa watu wanyofu wa moyo.
12Furahini katika Bwana , enyi wenye haki,
lisifuni jina lake takatifu.