Isaya 24

Isaya 24

Hukumu ijayo ya dunia

1Tazama, BWANA ameifanya dunia kuwa tupu, aifanya ukiwa, aipindua, na kuwatawanya wakaao ndani yake.

2Na itakuwa kama ilivyo hali ya watu, ndivyo itakavyokuwa hali ya kuhani; kama ilivyo hali ya mtumwa, ndivyo itakavyokuwa hali ya bwana wake; kama ilivyo hali ya mjakazi, ndivyo itakavyokuwa hali ya bibi yake; kama ilivyo hali yake anunuaye, ndivyo itakavyokuwa hali yake auzaye; kama ilivyo hali yake akopeshaye, ndivyo itakavyokuwa hali yake akopaye; kama ilivyo hali yake atwaaye faida, ndivyo itakavyokuwa hali yake ampaye faida.[#Eze 7:12]

3Dunia hii itafanywa tupu kabisa, na kuharibiwa kabisa; maana BWANA amenena neno hilo.

4Dunia inaomboleza, inazimia; ulimwengu unadhoofika, unazimia; watu wakuu wa dunia wanadhoofika.

5Tena dunia imetiwa unajisi kwa watu wanaoikaa; kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele.[#Mwa 3:17; Law 18:25; Hes 35:33]

6Ndiyo sababu laana imeila dunia hii, na hao wanaoikaa wameonekana kuwa na hatia, ndiyo sababu watu wanaoikaa dunia wameteketea, watu waliosalia wakawa wachache tu.[#Law 26:15; Kum 28:15; Dan 9:11; Mal 2:2]

7Divai mpya inaomboleza, mzabibu umedhoofika, watu wote waliochangamka moyo wanaugua.

8Sauti ya furaha ya matoazi inakoma; kelele yao wafurahio imekwisha; furaha ya kinubi inakoma.

9Hawatakunywa divai pamoja na nyimbo; kileo kitakuwa uchungu kwao wakinywao.

10Mji wa machafuko umebomolewa; kila nyumba imefungwa, asipate kuingia mtu awaye yote.

11Pana kilio katika njia kuu kwa sababu ya divai; furaha yote imetiwa giza, na changamko la nchi limetoweka.

12Ndani ya mji umebaki ukiwa, na lango lake limepigwa kwa uharibifu.

13Maana katikati ya dunia, katikati ya mataifa, itakuwa hivi; kama wakati utikiswapo mzeituni, kama wakati waokotapo zabibu baada ya mavuno yake.

14Hawa watainua sauti zao, watapiga kelele; kwa sababu ya utukufu wa BWANA watapiga kelele toka baharini.

15Basi, mtukuzeni BWANA katika mashariki, litukuzeni jina la BWANA, Mungu wa Israeli, katika visiwa vya bahari.[#Mal 1:11; Isa 66:19]

16Toka pande za mwisho wa dunia tumesikia nyimbo, Atukuzwe mwenye haki. Ndipo niliposema, Kukonda kwangu! Kukonda kwangu! Ole wangu! Watenda hila wametenda hila, naam, watendao hila wametenda hila sana.[#Yer 3:20]

17Hofu, na shimo, na mtego, viko juu yako, Ee mwenye kukaa duniani.[#Yer 48:43,44; Amo 5:19]

18Itakuwa kila akimbiaye sauti ya hofu ataanguka katika shimo; na kila apandaye na kutoka shimoni atanaswa na mtego; kwa maana madirisha yaliyo juu yamewekwa wazi, na misingi ya dunia inatikisika.[#Mwa 7:11; Zab 18:7]

19Dunia kuvunjika, inavunjika sana; dunia kupasuka, imepasuka sana; dunia kutikisika, imetikisika sana.[#Yer 4:23]

20Dunia inalewalewa kama mlevi, nayo inawayawaya kama machela; na mzigo wa dhambi zake utailemea; nayo itaanguka, wala haitainuka tena.

21Tena itakuwa katika siku hiyo, BWANA ataliadhibu jeshi la mahali palipo juu katika mahali palipo juu, na wafalme wa dunia katika dunia;[#Zab 76:12]

22nao watakusanywa pamoja kama vile wakusanywavyo wafungwa katika shimo nao watafungwa katika gereza; na baada ya muda wa siku nyingi wataadhibiwa.

23Ndipo mwezi utatahayari, na jua litaona haya; kwa kuwa BWANA wa majeshi atatawala katika mlima wa Sayuni, na katika Yerusalemu, na mbele ya wazee wake kwa utukufu.[#Ebr 12:22; Ufu 19:4]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania