Mika 5

Mika 5

Mtawala kutoka Bethlehemu

1Sasa utajikusanya vikosi vikosi, Ee binti wa vikosi; yeye amemhusuru; watampiga mwamuzi wa Israeli shavuni mwake kwa fimbo.[#Ayu 16:10; Omb 3:30; Mt 27:30]

2Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye asili yake imekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.[#Mwa 35:19; 49:10; Zab 132:6; Isa 9:6; Zab 90:2; Mit 8:22; Yn 1:1; Mt 2:6; Yn 7:42]

3Kwa sababu hiyo atawatoa, hata wakati wa kuzaa kwake aliye na uchungu; ndipo hayo mabaki ya nduguze watawarudia wana wa Israeli.

4Naye atasimama, na kulisha kundi lake kwa nguvu za BWANA, kwa enzi ya jina la BWANA, Mungu wake; nao watakaa; maana sasa atakuwa mkuu hadi miisho ya dunia.[#Zab 72:8; Isa 52:13; Zek 9:10; Lk 1:32]

5Na mtu huyu atakuwa amani yetu; wakati Mwashuri atakapoingia katika nchi yetu, na kuyakanyaga majumba yetu, hapo mtawaleta wachungaji saba juu yake, na wakuu wanane.[#Isa 9:6; Lk 2:14; Efe 2:14; Kol 1:20]

6Nao wataiharibu nchi ya Ashuru kwa upanga, na nchi ya Nimrodi katika malango yake; naye atatuokoa na Mwashuri, atakapoingia katika nchi yetu, na kukanyaga ndani ya mipaka yetu.[#Lk 1:71; Mwa 10:8-11]

Wajibu wa mabaki

7Na hayo mabaki ya Yakobo yatakuwa kati ya kabila nyingi mfano wa umande utokao kwa BWANA, mfano wa manyunyu katika nyasi; yasiyowategemea watu, wala kuwangojea wanadamu.[#Zab 110:3]

8Na hayo mabaki ya Yakobo yatakuwa kati ya mataifa, kati ya kabila nyingi, mfano wa simba kati ya wanyama wa msituni, kama mwanasimba kati ya makundi ya kondoo, ambaye, akiwa anapita katikati, hukanyagakanyaga na kuraruararua, wala hakuna wa kuokoa.

9Mkono wako na uinuliwe juu ya adui zako, na adui zako wote wakauawe mbali.

10Kisha itakuwa katika siku hiyo, asema BWANA, nitawakatilia mbali farasi wako watoke kati yako, nami nitayaharibu magari yako ya vita;[#Zek 9:10]

11nami nitaikatilia mbali miji ya nchi yako, na ngome zako zote nitaziangusha;

12nami nitakatilia mbali uchawi, usiwe mkononi mwako; wala hutakuwa tena na watu wenye kutabana;

13nami nitakatilia mbali sanamu zako na nguzo zako, zitoke kati yako; wala hutaiabudu tena kazi ya mikono yako.[#Zek 13:2; Isa 2:8]

14Nami nitayang'oa maashera yenu, yasiwe kati yako; nami nitaiangamiza miji yako.

15Nami nitajilipiza kisasi katika hasira na ghadhabu kwa mataifa yasiyonitii.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania