Zaburi 16

Zaburi 16

Wimbo wa imani na usalama kwa Mungu

1Mungu, unihifadhi mimi,[#Zab 25:20]

Kwa maana nakukimbilia Wewe.

2Nimemwambia BWANA, Ndiwe BWANA wangu;

Sina wema ila utokao kwako.

3Nao watakatifu waliopo duniani, ndio Walio bora,

Hao ndio niliopendezwa nao.

4Huzuni zao zitaongezeka

Wambadilio Mungu kwa mwingine;

Sitazimimina sadaka zao za damu,

Wala kuyataja majina yao midomoni mwangu.

5BWANA ndiye fungu la posho langu,

Na la kikombe changu;

Wewe unayaamua maisha yangu.

6Mipaka yangu imeangukia mahali pema,

Naam, nimepata urithi mzuri.

7Nitamhimidi BWANA aniongozaye,

Wakati wa usiku pia moyo wangu hunishauri.

8Nimemweka BWANA mbele yangu daima,[#Mdo 2:25-28]

Kwa kuwa yuko kuliani mwangu, sitaondoshwa.

9Kwa hiyo moyo wangu unafurahi,

Nayo nafsi yangu inashangilia,

Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.

10Maana hutaitupa kuzimu nafsi yangu,[#Mdo 13:35; Zab 49:15; Mdo 2:27; Dan 9:24; Lk 1:35]

Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu.

11Utanijulisha njia ya uzima;[#Mdo 2:28]

Mbele za uso wako kuna furaha tele;

Na katika mkono wako wa kulia

Mna mema ya milele.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania