Yoshua Mwana wa Sira 36

Yoshua Mwana wa Sira 36

Sala kwa ajili ya watu wa Mungu

1Ee Bwana, Mungu wa watu wote, utuokoe; uangalie uwatishe mataifa yote; uuinue mkono wako juu ya watu wageni;

2na kuwaonesha nguvu zako zilizo kuu.

3Kama vile ulivyojitakasa kati yetu mbele yao, vivyo hivyo ujitukuze kati yao mbele yetu;

4nao wakujue Wewe kama sisi tukujuavyo, ya kwamba hakuna Mungu ila Wewe peke yako.

5Tuonyeshe ishara tena, na kufanya mambo ya ajabu uutukuze mkono wako, naam, mkono wako wa kuume;

6uuamshe ukali wako na kumimina hasira; umtiishe mtesi, na kumwangamiza adui.

7Uuhimize wakati na kuuamuru mihula;

8ni nani atakayekuambia Wewe, Unafanyaje?

9Uwaponde kichwa wakuu wa maadui, wanaosema, Hakuna ila sisi.

10Uwakusanye kabila zote za Yakobo, na kuwafanya urithi wako kama siku za kale.

11Ee BWANA, uwarehemu watu walioitwa kwa jina lako, na Israeli uliyemwita mzaliwa wako wa kwanza.

12Uuonee huruma mji wa patakatifu pako, Yerusalemu, mahali pako pa raha;

13Uujaze Sayuni adhama yako, na patakatifu pako utukufu wako.

14Uwashuhudie wale waliokuwa viumbe vyako tangu awali, na kuyathibitisha maneno ya unabii yaliyonenwa kwa jina lako.

15Uwajazi wakungojao, na watu watawasadiki manabii wako.

16Ee BWANA, uisikilize sala yao wakuombao, sawasawa na kibali chako kwa watu wako;

17na wote wakaao duniani watajua ya kwamba Wewe ndiwe BWANA, Mungu wa milele.

Kutofautisha

18Tumbo litapokea kila namna ya chakula.

Lakini namna moja hupita nyingine;

19Kinywa chaonja vyakula vya mawindo;

Na moyo wa ufahamu maneno ya hila.

20Moyo wenye hila huleta machukizo;

Bali mwelekevu ataurudishia hayo.

Kumchagua mke

21Mwanamke atamkubali mume yeyote,

Ila binti mmoja ni mzuri kuliko mwingine.

22Uzuri wa mwanamke huuburudisha uso, wala mwanamume hatamani neno lolote kuliko huo;

23aidha, akiwa anao ulimi wa unyenyekevu, mume wake si mfano wa wanadamu.

24Apataye mke hujipatia mali iliyo bora; msaidizi wa kumfaa, na nguzo ya kumtegemeza.

25Pasipo ukuta shamba la mizabibu litafanyika ukiwa; naye asiye na mke atapata kuwa mtoro asiye na kikao.

26Ni nani atakayewaamini kundi la wanyang'anyi warukao huku na huko?

27Kadhalika mtu asiye na kiota, mwenye kulala ovyo wakati wa usiku popote alipo.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania