Hekima ya 9

Hekima ya 9

Sala ya Sulemani kwa ajili ya Hekima

1Ee Mungu wa baba zetu, BWANA, mwenye kuihifadhi rehema yako, umevifanya vitu vyote kwa neno lako;[#1 Fal 3:6-9; Hek 7:7]

2na kwa Hekima yako ukamuumba mwanadamu, ili avitawale viumbe vilivyoumbwa nawe,

3na kumiliki ulimwengu katika utakatifu na kwa haki, na kutoa hukumu kwa unyofu wa moyo.

4Nakusihi unipe Hekima, ambayo huketi karibu nawe katika kiti chako cha enzi, wala usinikatae mimi miongoni mwa watumishi wako;

5mimi niliye mtumwa wako, na mwana wa mjakazi wako, mtu dhaifu asiye wa siku nyingi, wala sina nguvu ya kufahamu hukumu na sheria.

6Kwa maana mtu ajapokuwa ni mkamilifu miongoni mwa wanadamu, pasipo Hekima itokayo kwako atahesabiwa kuwa si kitu.

7Wewe umenichagua mbele ya ndugu zangu kuwa mfalme wa watu wako na kutoa hukumu kwa wana wako.

8Wewe umeniamuru kujenga hekalu katika mlima wako mtakatifu, na madhabahu katika mji ukaapo, nakala ya maskani takatifu uliyoifanya tayari tangu awali.

9Na pamoja nawe hukaa Hekima, ijuayo matendo yako, ikiwapo hapo ulipoumba ulimwengu, ikayatambua yakupendezayo na yaliyo mema sawasawa na amri zako.

10Uipeleke kutoka mbingu takatifu, na kutoka kwenye kiti chako kitukufu; ili ikae nami na kutenda kazi pamoja nami, nijifunze yale yakupendezayo.

11Kwa maana huyajua mambo yote na kuyafahamu; na katika kutenda kwangu itaniongoza kwa njia za kiasi, na kunilinda katika utukufu wake.

12Hivyo matendo yangu yatakubalika, nami nitawahukumu watu wako kwa haki, na kustahili kukipokea kiti cha baba yangu.

13Ni mtu yupi awezaye kulijua shauri la Mungu?

Au ni nani atakayeelewa na mapenzi yake?

14Kwa kuwa mawazo ya wanadamu yana woga, na makusudi yetu yanaelekea kushindwa;

15na mwili wenye uharibifu huigandamiza roho, na kiwiliwili cha kidunia huzilemea akili zilizosongwa na masumbufu.

16Kwa shida tu twayapambanua yaliyoko duniani, na yaliyo karibu nasi ni kazi kuyaona; lakini yaliyoko mbinguni ni nani aliyeyagundua?

17Naye ni yupi aliyeyavumbua mashauri yako, isipokuwa ulimpa Hekima na kumpelekea Roho yako takatifu kutoka juu?

18Ndivyo miendo yao wakaao duniani ilivyosafishwa, na wanadamu walivyofundishwa yakupendezayo; hata na kwa Hekima wao wenyewe waliponywa.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania