The chat will start when you send the first message.
1Maana sifa mbaya huleta aibu na makaripio,
kama yampatayo mwenye dhambi mdanganyifu.
2Usikubali kutawaliwa na tamaa yako,
la sivyo, itakuchana kama fahali,
3itayakwanyua matawi yako ukapoteza matunda yako,
ukaachwa kama mti ulionyauka.
4Tamaa mbaya humwangamiza mwenyewe,
na kumfanya awe kichekesho kwa maadui zake.
5Maneno ya upole humwongezea mtu marafiki
kuongea kwa adabu husababisha hisani.
6Uwe na marafiki wengi wa kukusalimu,
lakini wa kukushauri awe mmoja tu kati ya elfu.
7Ukitaka kupata rafiki mpime kwanza,
usiharakishe kumwamini.
8Maana kuna rafiki aliye rafiki inapomfaa;
siku ya taabu hatakuwako kukutegemeza.
9Pia kuna rafiki abadilikaye kuwa adui,
atazusha ugomvi ili kukuaibisha.
10Pia yuko rafiki ambaye ni rafiki wakati wa mlo;
lakini siku ya taabu hatakuwako kukutegemeza.
11Ukipata fanaka atajifanya sawa nawe,
na kuwaamuru watumishi wako.
12Lakini ukifilisika atakugeuka;
na kujificha mbali nawe.
13Kaa mbali na maadui zako,
na ujihadhari na rafiki zako.
14Rafiki mwaminifu ni kinga imara;
ampataye rafiki kama huyo amepata hazina.
15Rafiki mwaminifu ana thamani kuliko chochote,
hakuna awezaye kupima ubora wake.
16Rafiki mwaminifu ni dawa itiayo nguvu mwilini,
watu wamchao Bwana ndio wanaompata rafiki huyo.
17Amchaye Bwana hupata marafiki wa kweli
maana alivyo mtu ndivyo na rafiki zake.
18Mwanangu, tangu ujana wako, chagua funzo,
na hata uwapo mzee utaendelea kumpata Hekima.
19Fanya bidii kama mkulima na mpanzi kumtafuta Hekima,
na kungojea mavuno yake bora.
Itakubidi kushughulika juu yake kwa muda,
lakini muda si muda utakula mazao yake.
20Watu wasio na nidhamu humwona Hekima kuwa mkali,
wapumbavu hawakai naye kwa muda mrefu.
21Kwao Hekima ni mzito kama jiwe la kupimia,
nao hawakawii kumtupilia mbali.
22Hekima kama jina lake lilivyo
hajijulishi kwa watu wengi.
23Mwanangu, nisikilize na kufuata shauri langu.
Usikatae mawaidha yangu.
24Tia pingu za Hekima miguuni mwako,
na ukosi wake shingoni mwako.
25Beba mzigo wake,
wala usichoke na vifungo vyake.
26Mwendee kwa roho yako yote,
na kushika njia zake kwa nguvu zako zote.
27Mchunguze na kumtafuta, naye atajijulisha kwako.
Ukisha mpata usimwachilie.
28Mwishowe utapata pumziko kwake,
naye atakuwa ndiye furaha yako.
29Pingu zake zitakuwa ngome yako imara,
na ukosi wake utakuwa ushanga wa thamani.
30Nira yake ni pambo la dhahabu
na vifungo vyake ni mkufu wa buluu.
31Hekima atakuwa kwako kama vazi la heshima,
atakuwa kama taji la furaha kichwani pako.
32Mwanangu, ukitaka, utafundishwa;
pania kujifunza nawe utakuwa na akili.
33Ukipenda kusikiliza, utapata maarifa;
ukitega sikio lako, utakuwa mwenye hekima.
34Ukienda kwenye mkutano wa wazee,
akiwako mzee mwenye hekima ambatana naye.
35Uwe tayari kusikiliza kila fundisho,
na usiziache methali za hekima kukuponyoka.
36Ukimwona mwenye hekima, mwendee mapema,
kichakaze kizingiti cha nyumba yake kwa kumtembelea.
37Zitafakari kanuni za Bwana,
jishughulishe na amri zake.
Yeye ataiimarisha akili yako,
na hekima unayotamani utajaliwa.